74 Bible Verses About Repentance
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.
-
18 Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Kristo atateswa. 19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu. 21 Ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa vinywa vya manabii wake watakatifu.
-
17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19 Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.
“Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.
21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’
-
8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu, 9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.
10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. 11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo. 12 Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu.
-
27 Lakini mtu mwovu akigeuka kutoka maovu aliyoyatenda na kufanya yaliyo haki na sawa, ataokoa maisha yake. 28 Kwa kuwa anayafikiria na kugeuka kutoka makosa yake yote aliyoyatenda na kuyaacha, hakika ataishi, hatakufa. 29 Lakini nyumba ya Israeli inasema, ‘Njia za Bwana si haki.’ Je, njia zangu si za haki, ee nyumba ya Israeli? Je, si njia zenu ndizo ambazo si za haki?”
30 “Kwa hiyo, ee nyumba ya Israeli, nitawahukumu, kila mmoja sawasawa na njia zake, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni! Geukeni kutoka makosa yenu yote, ndipo dhambi haitakuwa anguko lenu. 31 Tupilieni mbali makosa yenu yote mliyoyatenda, nanyi mpate moyo mpya na roho mpya. Kwa nini mfe, ee nyumba ya Israeli? 32 Kwa maana sifurahii kifo cha mtu awaye yote afaye katika uovu, asema Bwana Mwenyezi. Tubuni basi, mkaishi!
-
1 Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa. 2 Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote? 3 La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo. 4 Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu? 5 Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”
-
1 Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, 2 “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” 3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema:
“Sauti ya mtu aliaye huko nyikani,
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana,
yanyoosheni mapito yake.’ ”
-
14 Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu, 15 akisema, “Wakati umewadia, Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema.”
-
29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”
-
9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
-
46 Akawaambia, “Haya ndiyo yaliyoandikwa: Kristo atateswa na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu. 47 Toba na msamaha wa dhambi zitatangaziwa mataifa yote kupitia jina lake kuanzia Yerusalemu. 48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
-
19 “Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni, 20 bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Uyahudi na pia kwa watu wa Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao.
-
15 “Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16 Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”
18 Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”
-
4 “Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena;
nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’
5 Masikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako,
lakini sasa macho yangu yamekuona.
6 Kwa hiyo najidharau mwenyewe,
na kutubu katika mavumbi na majivu.”
-
7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka mawe haya. 9 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti. Basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”
10 Ule umati wa watu ukamuuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”
11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”
12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamuuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”
13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”
14 Askari nao wakamuuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”
Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”
-
30 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Yesu, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
31 Yesu akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. 32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”
-
4 “Ikiwa mmoja wenu ana kondoo mia moja, naye akapoteza mmoja wao, je, hawaachi wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta huyo aliyepotea mpaka ampate? 5 Naye akishampata, humbeba mabegani mwake kwa furaha 6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’ 7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”
8 “Au ikiwa mwanamke ana sarafu za fedha kumi, naye akapoteza moja, je, hawashi taa na kufagia nyumba na kuitafuta kwa bidii mpaka aipate? 9 Naye akiisha kuipata, huwaita rafiki zake na majirani na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimeipata ile sarafu yangu ya fedha iliyopotea.’ 10 Vivyo hivyo, nawaambia, kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu juu ya mwenye dhambi mmoja atubuye.”
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.
1 Ee Mungu, unihurumie,
kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,
kwa kadiri ya huruma yako kuu,
uyafute makosa yangu.
2 Unioshe na uovu wangu wote
na unitakase dhambi yangu.
3 Kwa maana ninajua makosa yangu,
na dhambi yangu iko mbele yangu daima.
4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi
na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,
ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,
na kuwa na haki utoapo hukumu.
-
13 “Wakati nitakapofunga mbingu ili isiwepo mvua, au nikiamuru nzige kula mazao ya nchi au nikituma tauni miongoni mwa watu wangu, 14 kama watu wangu, wanaoitwa kwa Jina langu, watajinyenyekesha na kuomba na kuutafuta uso wangu na kuacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na nitaiponya nchi yao.
-
3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu? 4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?
5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.
-
12 “Hata sasa,” asema Bwana,
“nirudieni kwa mioyo yenu yote,
kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.”
13 Rarueni mioyo yenu
na siyo mavazi yenu.
Mrudieni Bwana, Mungu wenu,
kwa maana yeye ndiye mwenye neema
na mwingi wa huruma,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,
huona huruma, hujizuia kuleta maafa.
-
1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika:
“Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu. 2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo. 3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.
4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza. 5 Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake.
-
5 Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa nguo za gunia.
6 Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha enzi, akavua majoho yake ya kifalme, akajifunika nguo ya gunia kisha akaketi chini mavumbini. 7 Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote:
“Kwa amri ya mfalme na wakuu wake:
“Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ngʼombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa. 8 Bali wanadamu na wanyama wafunikwe kwa nguo za gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. 9 Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.”
10 Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.
-
23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.
-
30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi.
-
4 Yohana alikuja, akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. 5 Watu kutoka Uyahudi wote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.
-
6 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Tubuni! Geukeni kutoka kwenye sanamu zenu na mkatae matendo yenu yote ya machukizo!
-
6 Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana;
mwiteni maadamu yu karibu.
7 Mtu mwovu na aiache njia yake,
na mtu mbaya na ayaache mawazo yake.
Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu,
arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa.
-
28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.
30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda, bwana,’ lakini hakwenda.
31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”
Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”
Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu. 32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.
-
22 Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako.
-
19 “Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.
-
9 Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu.
10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu, 11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.
-
3 Kwa hiyo, jilindeni.
“Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. 4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”
-
8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.
-
21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki. 22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake. 23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.
-
13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,
bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
-
20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu. 21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwepo hadi leo. 24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”
-
1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. 2 Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.
3 Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4 Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”
Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”
5 Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.
-
11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
-
5 Bwana akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu. 6 Bwana akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”
-
18 “Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu:
‘Ulinirudi kama ndama mkaidi,
nami nimekubali kutii.
Unirudishe, nami nitarudi,
kwa sababu wewe ndiwe Bwana, Mungu wangu.
19 Baada ya kupotea, nilitubu;
baada ya kuelewa, nilijipiga kifua.
Niliaibika na kuona haya
kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’
20 Je, Efraimu si mwanangu mpendwa,
mtoto ninayependezwa naye?
Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake,
bado ninamkumbuka.
Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku,
nina huruma kubwa kwa ajili yake,”
asema Bwana.
-
21 “Lakini mtu mwovu akiacha dhambi zake zote alizozitenda na kushika amri zangu zote na kufanya lililo haki na sawa, hakika ataishi, hatakufa. 22 Hakuna kosa lolote alilotenda litakalokumbukwa juu yake. Kwa ajili ya mambo ya haki aliyoyatenda, ataishi. 23 Je, mimi ninafurahia kifo cha mtu mwovu? Asema Bwana Mwenyezi. Je, si mimi ninafurahi wanapogeuka kutoka njia zao mbaya na kuishi?
-
9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
-
6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:
“Mungu huwapinga wenye kiburi,
lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni. 10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.
-
16 Basi tubu! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.
-
2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. 3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.
4 “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili.
-
20 Wanadamu waliosalia, ambao hawakuuawa katika mapigo hayo, bado walikataa kutubia kazi za mikono yao na hawakuacha kuabudu mashetani na sanamu za dhahabu, za fedha, za shaba, za mawe na za miti, ambazo haziwezi kuona, kusikia wala kutembea. 21 Wala hawakutubu na kuacha matendo yao ya uuaji, uchawi, uasherati wala wizi wao.
-
2 “Hili ndilo Bwana asemalo: Simama katika ua wa nyumba ya Bwana na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya Bwana. Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno. 3 Huenda watasikiliza, na kila mmoja akageuka kutoka njia yake mbaya. Kisha nitawahurumia na kuacha kuwaletea maafa niliyokuwa ninapanga kwa sababu ya maovu waliyofanya. 4 Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu ambayo nimeiweka mbele yenu, 5 nanyi ikiwa hamtayasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza), 6 ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”
-
10 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.
11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12 Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”
-
12 Kwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi.
-
7 “Mwanadamu, nimekufanya wewe kuwa mlinzi kwa ajili ya nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo na uwape maonyo kutoka kwangu. 8 Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Ewe mtu mwovu, hakika utakufa,’ nawe hukusema neno la kumwonya ili atoke katika njia zake, yule mtu mwovu atakufa kwa ajili ya dhambi yake, mimi nitaitaka damu yake mkononi mwako. 9 Lakini kama utamwonya huyo mtu mwovu aache njia zake mbaya naye hafanyi hivyo, atakufa kwa ajili ya dhambi yake, lakini utakuwa umejiokoa mwenyewe.
10 “Mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo mnalosema: “Makosa yetu na dhambi zetu zimetulemea, nasi tunadhoofika kwa sababu ya hayo. Tutawezaje basi kuishi?” ’ 11 Waambie, ‘Hakika kama mimi niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, sifurahii kifo cha watu waovu, bali kwamba wageuke kutoka njia zao mbaya wapate kuishi. Geukeni! Geukeni kutoka njia zenu mbaya! Kwa nini mkafe, ee nyumba ya Israeli?’
12 “Kwa hiyo, mwanadamu, waambie watu wako, ‘Haki ya mtu mwenye haki haitamwokoa wakati anapoacha kutii, wala uovu wa mtu mwovu hautamsababisha yeye kuanguka anapotubu na kuacha uovu. Mtu mwenye haki, kama akitenda dhambi, hataishi kwa sababu ya uadilifu wake wa awali.’
-
15 Angalieni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. 16 Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza. 17 Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
-
13 Ndipo Daudi akamjibu Nathani, “Nimefanya dhambi dhidi ya Bwana.”
Nathani akamjibu, “Bwana amekuondolea dhambi yako. Hutakufa. 14 Lakini kwa sababu kwa kufanya hili umefanya adui za Bwana kuonyesha dharau kabisa, mwana atakayezaliwa kwako atakufa.”
-
16 jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu
mbele zangu!
Acheni kutenda mabaya,
17 jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
18 “Njooni basi tuhojiane,”
asema Bwana.
“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,
zitakuwa nyeupe kama theluji;
ingawa ni nyekundu sana kama damu,
zitakuwa nyeupe kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi,
20 lakini kama mkikataa na kuasi,
mtaangamizwa kwa upanga.”
Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.
-
6 Kwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema:
“Watu wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru. 7 Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona. 8 Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Bwana. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Bwana Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi. 9 Kama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”
-
18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. 19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 za fedha.
-
1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tukisonga mbele ili tufikie utimilifu, sio kuweka tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, 2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu, na hukumu ya milele. 3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.
4 Kwa kuwa ni vigumu kwa wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu, 5 ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao, 6 kisha wakianguka, kuwarejesha tena katika toba. Kwa kuwa wanamsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani, nayo ikawa hasara kwao.
-
27 Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. Bwana ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji. 28 Mwombeni Bwana, kwa kuwa tumepata ngurumo na mvua za mawe za kututosha. Nitawaachia mwondoke; hamtahitaji kungoja zaidi.”
29 Mose akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba Bwana. Ngurumo zitakoma na hapatakuwepo mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa, nchi ni mali ya Bwana. 30 Lakini ninajua kuwa wewe na maafisa wako bado hammwogopi Bwana Mungu.”
31 (Kitani na shayiri viliharibiwa, kwa kuwa shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa katika kutoa maua. 32 Hata hivyo, ngano na jamii nyingine ya ngano hazikuharibiwa kwa sababu zilikuwa hazijakomaa bado.)
33 Kisha Mose akaondoka kwa Farao akaenda nje ya mji. Mose akanyoosha mikono yake kuelekea kwa Bwana, ngurumo na mvua ya mawe vikakoma, mvua haikuendelea tena kunyesha nchini. 34 Farao alipoona kwamba mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akafanya dhambi tena. Yeye na maafisa wake wakafanya mioyo yao kuwa migumu. 35 Kwa hiyo moyo wa Farao ukawa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waende, kama vile Bwana alivyokuwa amesema kupitia Mose.
-
14 Kisha Bwana akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.
-
5 Kwa nini basi watu hawa walipotea?
Kwa nini Yerusalemu inapotea kila mara?
Wanangʼangʼania udanganyifu
na wanakataa kurudi.
6 Nimewasikiliza kwa makini,
lakini hawataki kusema lililo sawa.
Hakuna anayetubia makosa yake
akisema, “Nimefanya nini?”
Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe
kama farasi anayekwenda vitani.
7 Hata korongo aliyeko angani
anayajua majira yake yaliyoamriwa,
nao njiwa, mbayuwayu na koikoi
hufuata majira yao ya kurudi.
Lakini watu wangu hawajui
Bwana anachotaka kwao.
-
1 “Njooni, tumrudie Bwana.
Ameturarua vipande vipande
lakini atatuponya;
ametujeruhi lakini
atatufunga majeraha yetu.
2 Baada ya siku mbili atatufufua;
katika siku ya tatu atatuinua,
ili tuweze kuishi mbele zake.
3 Tumkubali Bwana,
tukaze kumkubali yeye.
Kutokea kwake ni hakika kama vile
kuchomoza kwa jua;
atatujia kama mvua za masika,
kama vile mvua za vuli
ziinyweshavyo nchi.”
4 “Nifanye nini nawe, Efraimu?
Nifanye nini nawe, Yuda?
Upendo wako ni kama ukungu wa asubuhi,
kama umande wa alfajiri utowekao.
-
3 “Heri walio maskini wa roho,
maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.
4 Heri wale wanaohuzunika,
maana hao watafarijiwa.
5 Heri walio wapole,
maana hao watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya haki,
maana hao watatoshelezwa.
-
24 Ndipo Sauli akamwambia Samweli, “Nimetenda dhambi. Nimevunja amri ya Bwana na maagizo yako. Niliwaogopa watu na kwa hiyo nikafanya walivyotaka. 25 Sasa ninakusihi usamehe dhambi yangu, nawe urudi pamoja nami, ili nipate kumwabudu Bwana.”
26 Lakini Samweli akamwambia, “Sitarudi pamoja nawe. Umelikataa neno la Bwana, naye Bwana amekukataa wewe, usiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli!”
-
27 Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu.
28 Ndipo neno la Bwana lilipomjia Eliya Mtishbi kusema, 29 “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”
-
36 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu yeyote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi iliyo mbali au karibu 37 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya utumwa na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa na tumetenda uovu’; 38 kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 39 basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na kuitetea haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako.
-
18 Naungama uovu wangu,
ninataabishwa na dhambi yangu.
-
12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:
“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana,
‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana,
‘Sitashika hasira yangu milele.
13 Ungama dhambi zako tu:
kwamba umemwasi Bwana Mungu wako,
umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni
chini ya kila mti unaotanda,
nawe hukunitii mimi,’ ”
asema Bwana.
14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Bwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni.
-
41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
-
75 Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
-
16 Baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na “wenye dhambi,” wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Yesu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”
17 Yesu aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
-
25 “Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26 Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’
27 “Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu, 28 maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 “Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Mose na Manabii, wawasikilize hao.’
30 “Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’
31 “Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”
-
19 Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejezwa na mtu mwingine, 20 hamna budi kujua kwamba yeyote amrejezaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kusitiri wingi wa dhambi.
-
26 Humwomba Mungu, akapata kibali kwake,
huuona uso wa Mungu na kushangilia kwa furaha;
Mungu humrudisha katika hali yake ya uadilifu.
27 Ndipo huja mbele za watu na kusema,
‘Nilitenda dhambi na kupotosha kilichokuwa haki,
lakini sikuadhibiwa kama nilivyostahili.
28 Alinikomboa nafsi yangu nisitumbukie shimoni,
nami nitaishi ili kuufurahia mwanga.’
-
8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”
Shows Read in context, Share and Copy.