65 Bible Verses About Judgment Day

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Judgment Day
  1. 11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana. 12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. 13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda. 14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. 15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.

  2. 1 Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. 2 Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.

    3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya. 4 Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

    8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

    10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

    11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

  3. 31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.

    34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

    37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

    40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

    41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  4. 9 Kwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.

    11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia.

  5. 24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

    29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

  6. 5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

  7. 9 “Nilipoendelea kutazama,

    “viti vya enzi vikawekwa,

    naye Mzee wa Siku akaketi.

    Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji;

    nywele za kichwa chake zilikuwa nyeupe kama sufu.

    Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka kwa miali ya moto,

    nayo magurudumu yake yote yalikuwa yanawaka moto.

    10 Mto wa moto ulikuwa unatiririka,

    ukipita mbele yake.

    Maelfu elfu wakamhudumia;

    kumi elfu mara kumi elfu wakasimama mbele zake.

    Mahakama ikakaa kuhukumu,

    na vitabu vikafunguliwa.

  8. 47 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. 48 Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. 49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

  9. 36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. 37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

    38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”

    39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. 41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”

  10. 1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, 2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. 3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

  11. 27 Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu, 28 vivyo hivyo Kristo alitolewa mara moja tu kuwa dhabihu ili azichukue dhambi za watu wengi. Naye atakuja mara ya pili, sio kuchukua dhambi, bali kuwaletea wokovu wale wanaomngoja kwa shauku.

  12. 4 Sikilizeni kelele juu ya milima,

    kama ile ya umati mkubwa wa watu!

    Sikilizeni, makelele katikati ya falme,

    kama mataifa yanayokusanyika pamoja!

    Bwana Mwenye Nguvu Zote anakusanya

    jeshi kwa ajili ya vita.

    5 Wanakuja kutoka nchi za mbali sana,

    kutoka miisho ya mbingu,

    Bwana na silaha za ghadhabu yake,

    kuangamiza nchi yote.

    6 Ombolezeni, kwa maana siku ya Bwana i karibu,

    itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.

    7 Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,

    moyo wa kila mtu utayeyuka.

    8 Hofu itawakamata,

    uchungu na maumivu makali yatawashika,

    watagaagaa kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa.

    Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,

    nyuso zao zikiwaka kama moto.

    9 Tazameni, siku ya Bwana inakuja,

    siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,

    kuifanya nchi kuwa ukiwa

    na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake.

    10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota

    havitatoa mwanga wake.

    Jua linalochomoza litatiwa giza

    na mwezi hautatoa nuru yake.

    11 Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,

    waovu kwa ajili ya dhambi zao.

    Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi,

    na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.

    12 Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi,

    watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri.

    13 Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke,

    nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake

    katika ghadhabu ya Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    katika siku ya hasira yake iwakayo.

  13. 9 Mwana-kondoo alipoivunja ile lakiri ya tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. 10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, “Hata lini, Ee Bwana Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi juu ya watu waishio duniani kwa ajili ya damu yetu?” 11 Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, mpaka idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.

    12 Nikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

    15 Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. 16 Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! 17 Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”

  14. 10 Basi kwa nini wewe wamhukumu ndugu yako? Au kwa nini wewe unamdharau ndugu yako? Kwa kuwa sote tutasimama mbele ya kiti cha Mungu cha hukumu. 11 Kwa kuwa imeandikwa:

    “ ‘Kama vile niishivyo,’ asema Bwana,

    ‘kila goti litapigwa mbele zangu,

    na kila ulimi utakiri kwa Mungu.’ ”

    12 Hivyo basi kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe kwa Mungu.

  15. 4 Ndiyo sababu miongoni mwa makanisa ya Mungu, tunajivuna kuhusu saburi yenu na imani mliyo nayo katika mateso yote na dhiki mnazostahimili.

    5 Haya yote ni uthibitisho kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na kwa sababu hiyo ninyi mtahesabiwa kwamba mnastahili kuwa wa Ufalme wa Mungu, mnaoteswa kwa ajili wake. 6 Mungu ni mwenye haki: yeye atawalipa mateso wale wawatesao ninyi 7 na kuwapa ninyi mnaoteseka raha pamoja na sisi, wakati Bwana Yesu atakapodhihirishwa kutoka mbinguni katika mwali wa moto pamoja na malaika wake wenye nguvu. 8 Atawaadhibu wale wasiomjua Mungu na ambao hawakuitii Injili ya Bwana wetu Yesu. 9 Wataadhibiwa kwa uangamivu wa milele na kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa uweza wake, 10 siku hiyo atakapokuja kutukuzwa katika watakatifu wake na kustaajabiwa miongoni mwa wote walioamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwa hawa kwa sababu mliamini ushuhuda wetu kwenu.

  16. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.

    26 Kama tukiendelea kutenda dhambi kwa makusudi baada ya kupokea ufahamu wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi. 27 Lakini kinachobaki ni kungoja kwa hofu hukumu ya moto uwakao, utakaowaangamiza adui za Mungu. 28 Yeyote aliyeikataa sheria ya Mose alikufa pasipo huruma kwa ushahidi wa watu wawili au watatu. 29 Je, mnadhani ni adhabu kali kiasi gani anayostahili kupewa mtu aliyemkanyaga Mwana wa Mungu chini ya nyayo zake, yeye aliyeifanya damu ya Agano iliyomtakasa kuwa kitu najisi na kumtendea maovu Roho wa neema? 30 Kwa kuwa tunamjua yeye aliyesema, “Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.” Tena asema, “Bwana atawahukumu watu wake.” 31 Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai.

  17. 12 “Mataifa na yaamshwe;

    na yasonge mbele kuelekea Bonde la Yehoshafati,

    kwa kuwa nitaketi mahali pale

    kuhukumu mataifa yote yaliyoko kila upande.

    13 Tia mundu,

    kwa kuwa mavuno yamekomaa.

    Njooni, mkanyage zabibu,

    kwa kuwa shinikizo la kukamua zabibu limejaa

    na mapipa yanafurika:

    kwa kuwa uovu wao ni mkubwa!”

    14 Umati mkubwa, umati mkubwa

    katika bonde la uamuzi!

    Kwa kuwa siku ya Bwana ni karibu

    katika bonde la uamuzi.

    15 Jua na mwezi vitatiwa giza,

    na nyota hazitatoa mwanga wake tena.

    16 Bwana atanguruma kutoka Sayuni

    na mshindo wa ngurumo kutoka Yerusalemu;

    dunia na mbingu vitatikisika.

    Lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake,

    ngome imara kwa ajili ya watu wa Israeli.

    17 “Ndipo mtakapojua kwamba Mimi, Bwana Mungu wenu,

    nakaa Sayuni, mlima wangu mtakatifu.

    Yerusalemu utakuwa mtakatifu;

    kamwe wageni hawatavamia tena.

    18 “Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya,

    na vilima vitatiririka maziwa;

    mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji.

    Chemchemi itatiririka kutoka kwenye nyumba ya Bwana

    na kunywesha Bonde la Shitimu.

    19 Lakini Misri itakuwa ukiwa,

    Edomu itakuwa jangwa tupu,

    kwa sababu ya jeuri waliofanya kwa watu wa Yuda,

    ambao katika nchi yao

    walimwaga damu isiyo na hatia.

    20 Yuda itakaliwa na watu milele

    na Yerusalemu itadumu vizazi vyote.

    21 Hatia yao ya damu, ambayo sijasamehe,

    nitasamehe.”

    Bwana anakaa Sayuni!

  18. 14 “Siku kubwa ya Bwana iko karibu:

    iko karibu na inakuja haraka.

    Sikilizeni! Kilio katika siku ya Bwana

    kitakuwa kichungu,

    hata shujaa atapiga kelele.

    15 Siku ile ni siku ya ghadhabu,

    siku ya fadhaa na dhiki,

    siku ya uharibifu na ukiwa,

    siku ya giza na utusitusi,

    siku ya mawingu na giza nene,

    16 siku ya tarumbeta na mlio wa vita

    dhidi ya miji yenye ngome

    na dhidi ya minara mirefu.

    17 Nitawaletea watu dhiki,

    nao watatembea kama vipofu,

    kwa sababu wametenda dhambi

    dhidi ya Bwana.

    Damu yao itamwagwa kama vumbi

    na matumbo yao kama taka.

    18 Fedha yao wala dhahabu yao

    hazitaweza kuwaokoa

    katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana.

    Katika moto wa wivu wake

    dunia yote itateketezwa,

    kwa maana ataleta mwisho

    wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”

  19. 22 Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23 ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.

  20. 5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

  21. 39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.

    40 “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

  22. 29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

    “ ‘jua litatiwa giza,

    nao mwezi hautatoa nuru yake;

    nazo nyota zitaanguka kutoka angani,

    na nguvu za anga zitatikisika.’

    30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. 31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

    32 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 33 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. 34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

    36 “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. 39 Nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.

  23. 15 Yachukieni maovu, yapendeni mema;

    dumisheni haki mahakamani.

    Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote

    atawahurumia mabaki ya Yosefu.

    16 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo:

    “Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote

    na vilio vya uchungu katika njia kuu zote.

    Wakulima wataitwa kuja kulia,

    na waombolezaji waje kuomboleza.

    17 Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,

    kwa kuwa nitapita katikati yenu,”

    asema Bwana.

    18 Ole wenu ninyi mnaoitamani

    siku ya Bwana!

    Kwa nini mnaitamani siku ya Bwana?

    Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.

    19 Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba

    kumbe akakutana na dubu,

    kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake

    na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta,

    kumbe akaumwa na nyoka.

    20 Je, siku ya Bwana haitakuwa giza, na si nuru:

    giza nene, bila mwonzi wa mwanga?

  24. 47 “Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa. 48 Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho.

  25. 15 Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) 16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.

  26. 13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

  27. 17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu.

  28. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu.

  29. 1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.

  30. 6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yao, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu Siku ile kuu. 7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.

  31. 14 Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, 15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.”

  32. 14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,

    pamoja na kila neno la siri,

    likiwa jema au baya.

  33. 11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa

    na kiburi cha wanadamu kitashushwa,

    Bwana peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.

    12 Bwana Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba

    kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,

    kwa wote wanaojikweza

    (nao watanyenyekezwa),

    13 kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana,

    na mialoni yote ya Bashani,

    14 kwa milima yote mirefu

    na vilima vyote vilivyoinuka,

    15 kwa kila mnara ulio mrefu sana

    na kila ukuta wenye ngome,

    16 kwa kila meli ya biashara,

    na kila chombo cha baharini cha fahari.

    17 Majivuno ya mwanadamu yatashushwa,

    na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,

    Bwana peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,

    18 nazo sanamu zitatoweka kabisa.

  34. 1 “Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa. 2 Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele. 3 Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.

  35. 1 Pigeni tarumbeta katika Sayuni;

    pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu.

    Wote waishio katika nchi na watetemeke,

    kwa kuwa siku ya Bwana inakuja. Iko karibu,

    2 siku ya giza na huzuni,

    siku ya mawingu na utusitusi.

    Kama mapambazuko yasambaavyo

    toka upande huu wa milima

    hata upande mwingine

    jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja.

    Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani

    wala halitakuwepo tena kamwe

    kwa vizazi vijavyo.

    3 Mbele yao moto unateketeza,

    nyuma yao miali ya moto

    inawaka kwa nguvu.

    Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni,

    nyuma yao ni jangwa lisilofaa:

    hakuna kitu kinachowaepuka.

    4 Wanaonekana kama farasi;

    wanakwenda mbio

    kama askari wapanda farasi.

  36. 32 “Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 33 Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia. 34 Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe.

    35 “Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko. 36 Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala. 37 Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’ ”

  37. 17 Nikafikiri moyoni mwangu,

    “Mungu atawaleta hukumuni

    wote wawili wenye haki na waovu,

    kwa maana kutakuwako na wakati kwa ajili ya kila jambo,

    wakati kwa ajili ya kila tendo.”

  38. 12 Kama mtu yeyote akijenga juu ya msingi huu kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, miti, majani au nyasi, 13 kazi yake itaonekana ilivyo, kwa kuwa Siku ile itaidhihirisha. Itadhihirishwa kwa moto, nao moto utapima ubora wa kazi ya kila mtu. 14 Kama kile alichojenga kitabaki, atapokea thawabu yake. 15 Kama kazi kitateketea, atapata hasara, ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini tu kama mtu aliyenusurika kwenye moto.

  39. 7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho. 8 Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia. 9 Ndugu zangu, msinungʼunikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

    10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wabarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.

  40. 1 “Hakika siku inakuja, itawaka kama tanuru. Wote wenye kiburi na kila mtenda mabaya watakuwa mabua makavu, na siku ile inayokuja itawawasha moto,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Hakuna mzizi wala tawi litakalosalia kwao.

  41. 20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu. 21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwepo hadi leo. 24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”

  42. 42 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. 43 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. 44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.

    45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

  43. 11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.

    13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”

  44. 24 “Amin, amin nawaambia, yeyote anayesikia maneno yangu na kumwamini yeye aliyenituma, anao uzima wa milele, naye hatahukumiwa, bali amepita kutoka mautini, na kuingia uzimani.

  45. 32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

  46. 16 La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

    17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,

    nitamimina Roho wangu

    juu ya wote wenye mwili.

    Wana wenu na binti zenu watatabiri,

    vijana wenu wataona maono,

    na wazee wenu wataota ndoto.

    18 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,

    katika siku zile nitamimina Roho wangu,

    nao watatabiri.

    19 Nami nitaonyesha maajabu juu mbinguni,

    na ishara chini duniani:

    damu, moto, na mawimbi ya moshi.

    20 Jua litakuwa giza

    na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,

    kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana

    iliyo tukufu.

    21 Na kila mtu atakayeliitia

    jina la Bwana, ataokolewa.’

    22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo.

  47. 9 vyote na viimbe mbele za Bwana,

    kwa maana yuaja kuhukumu dunia.

    Atahukumu dunia kwa haki

    na mataifa kwa haki.

  48. 15 “Siku ya Bwana iko karibu

    kwa mataifa yote.

    Kama ulivyofanya, nawe utafanyiwa vivyo hivyo,

    matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako.

    16 Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu,

    vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo,

    watakunywa na kunywa,

    nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo.

  49. 21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

    24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

  50. 14 Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.

  51. 1 Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? 2 Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? 3 Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya?

  52. 12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Frati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki. 13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. 14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

    15 “Tazama, naja kama mwizi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”

    16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedoni kwa Kiebrania.

  53. 27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

  54. 1 Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. 2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. 3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu?

  55. 8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine. 9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu; 10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake. 11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.

    12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

    14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  56. 12 “Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda.

  57. 21 Katika siku ile Bwana ataadhibu

    nguvu zilizoko mbinguni juu,

    na wafalme walioko duniani chini.

    22 Watakusanywa pamoja

    kama wafungwa waliofungwa gerezani,

    watafungiwa gerezani

    na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.

  58. 14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari.

  59. 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;

    bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;

    12 mashamba na yashangilie,

    pamoja na vyote vilivyomo ndani yake.

    Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;

    13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,

    anakuja kuihukumu dunia.

    Ataihukumu dunia kwa haki,

    na mataifa katika kweli yake.

  60. 5 “Tazama, nitawapelekea nabii Eliya kabla ya kuja siku ile iliyo kuu na ya kutisha ya Bwana.

  61. 38 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

  62. 1 Wakati huo, umati mkubwa wa watu maelfu, walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu akaanza kuzungumza kwanza na wanafunzi wake, akawaambia: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani, unafiki wao. 2 Hakuna jambo lolote lililositirika ambalo halitafunuliwa, au lililofichwa ambalo halitajulikana. 3 Kwa hiyo, lolote mlilosema gizani litasikiwa nuruni. Na kile mlichonongʼona masikioni mkiwa kwenye vyumba vya ndani, kitatangazwa juu ya paa.

    4 “Nawaambieni rafiki zangu, msiwaogope wale wauao mwili, lakini baada ya hilo hawawezi kufanya lolote zaidi. 5 Lakini nitawaambia nani wa kumwogopa: Mwogopeni yule ambaye baada ya kuua mwili, ana mamlaka ya kuwatupa motoni. Naam, nawaambia, mwogopeni huyo!

  63. 8 “Ninawaambia kwamba yeyote atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri mbele za malaika wa Mungu. 9 Lakini yeye atakayenikana mimi mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkana mbele ya malaika wa Mungu.

  64. 17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanzia katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianzia kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?

  65. 1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika:

    “Haya ndiyo maneno ya aliye na zile Roho saba za Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa. 2 Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu. 3 Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.

    4 “Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili. 5 Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.