89 Bible Verses About Encouraging Others
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.
14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.
-
11 Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.
12 Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya. 13 Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi. 14 Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote. 15 Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.
-
23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu. 24 Tuangaliane na kuhimizana sisi kwa sisi katika upendo na katika kutenda mema. 25 Wala tusiache kukutana pamoja, kama wengine walivyo na desturi, bali tuhimizane sisi kwa sisi kadiri tuonavyo Siku ile inakaribia.
-
1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. 2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. 3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”
-
19 Kwa hiyo na tufanye bidii kutafuta yale yaletayo amani na kujengana sisi kwa sisi. 20 Usiiharibu kazi ya Mungu kwa ajili ya chakula. Hakika vyakula vyote ni safi, lakini ni kosa kula kitu chochote kinachomsababisha ndugu yako ajikwae. 21 Ni afadhali kutokula nyama wala kunywa divai au kufanya jambo lingine lolote litakalomsababisha ndugu yako ajikwae.
-
29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.
-
3 Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. 4 Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa. 5 Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili kanisa lipate kujengwa.
-
13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.
-
11 Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuweka juu yenu karama za rohoni ili mwe imara, 12 au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi.
-
32 “Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa.
-
13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.
-
23 “Vitu vyote ni halali,” lakini si vitu vyote vilivyo na faida. “Vitu vyote ni halali,” lakini si vyote vinavyojenga. 24 Mtu yeyote asitafute yaliyo yake mwenyewe, bali kila mtu atafute yale yanayowafaa wengine.
-
12 Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kulijenga kanisa.
-
26 Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. 27 Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. 28 Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu.
29 Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. 30 Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze.
-
19 Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Kristo. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu.
-
31 Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu, na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.
-
10 Hii ndiyo sababu nawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa.
-
3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.
-
2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo.
-
20 Lakini ninyi wapendwa, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu. 21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.
-
4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.
-
1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:
6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
kuwa kitu cha kushikilia,
7 bali alijifanya si kitu,
akachukua hali hasa na mtumwa,
naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
-
15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.
-
32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.
36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.
-
21 Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.”
-
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.
-
33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”
-
22 Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23 Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote.
-
1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.
-
6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.
-
4 Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5 kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. 6 Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo. 7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.
-
3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu,
yafanyeni imara magoti yaliyolegea,
4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu,
“Kuweni hodari, msiogope;
tazama, Mungu wenu atakuja,
pamoja na malipo ya Mungu,
atakuja na kuwaokoa ninyi.”
-
10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;
usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.
Nitakutia nguvu na kukusaidia;
nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
11 “Wote walioona hasira dhidi yako
hakika wataaibika na kutahayarika,
wale wakupingao
watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.
12 Ingawa utawatafuta adui zako,
hutawaona.
Wale wanaopigana vita dhidi yako
watakuwa kama vile si kitu kabisa.
-
25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
-
58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.
-
19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni. 21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana. 22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.
-
16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu.
-
1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri.
-
8 Elikana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?”
-
6 kila mmoja humsaidia mwingine
na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!”
7 Fundi humtia moyo sonara,
yeye alainishaye kwa nyundo
humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe,
Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.”
Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike.
-
5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, 6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.
-
9 Lakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu. 10 Kwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 Kwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 Mnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Kristo. 13 Kwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.
-
8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”
-
9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”
-
Wimbo wa kwenda juu.
1 Nayainua macho yangu nitazame vilima,
msaada wangu utatoka wapi?
2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.
-
28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”
-
Safari Ya Pili Ya Paulo Kueneza Injili
36 Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.” 37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye. 38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye. 39 Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro. 40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana. 41 Akapitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa ya huko.
-
1 Hata kama nitasema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa kengele inayolialia au toazi livumalo. 2 Ningekuwa na karama ya unabii na kujua siri zote na maarifa yote, hata kama nina imani kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, mimi si kitu. 3 Kama nikitoa mali yote niliyo nayo na kama nikijitolea mwili wangu uchomwe moto, kama sina upendo, hainifaidi kitu.
4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.
8 Upendo haushindwi kamwe. Lakini ukiwepo unabii, utakoma; zikiwepo lugha, zitakoma; yakiwepo maarifa, yatapita.
-
4 Mnapokuja kwake, yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake, 5 ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mnajengwa kuwa nyumba ya kiroho, ili mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
-
3 Fikiri jinsi ambavyo umewafundisha watu wengi,
jinsi ambavyo umeitia nguvu
mikono iliyokuwa dhaifu.
4 Maneno yako yamewategemeza wale waliojikwaa;
umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu.
-
4 Hata kama nikipita katikati
ya bonde la uvuli wa mauti,
sitaogopa mabaya,
kwa maana wewe upo pamoja nami;
fimbo yako na mkongojo wako
vyanifariji.
-
24 Kuweni hodari na mjipe moyo,
ninyi nyote mnaomtumaini Bwana.
-
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.
1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa
nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.
3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,
milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.
-
5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyoosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe;
mche Bwana ukajiepushe na uovu.
8 Hii itakuletea afya mwilini mwako,
na mafuta kwenye mifupa yako.
-
25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,
bali neno la huruma humfurahisha.
-
13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
-
7 Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote.
-
7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.
-
1 Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu. 2 Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Kristo, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu, 3 ili mtu yeyote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso.
-
15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.
16 Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema, 17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.
-
7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,
utaniepusha na taabu
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
-
24 Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali,
ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.
-
17 jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
-
1 Wafarijini, wafarijini watu wangu,
asema Mungu wenu.
2 Sema na Yerusalemu kwa upole,
umtangazie
kwamba kazi yake ngumu imekamilika,
kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia,
kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Bwana
maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.
-
11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
-
16 Ndipo wale waliomcha Bwana wakasemezana wao kwa wao, naye Bwana akasikiliza na akasikia. Kitabu cha kumbukumbu kikaandikwa mbele yake kuhusu wale ambao walimcha Bwana na kuliheshimu jina lake.
17 “Nao watakuwa watu wangu,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, “katika siku ile nitakapowafanya watu kuwa hazina yangu. Nitawahurumia, kama vile kwa huruma mtu amhurumiavyo mwanawe anayemtumikia. 18 Kwa mara nyingine tena utaona tofauti kati ya wenye haki na waovu, kati ya wale wanaomtumikia Mungu na wale wasiomtumikia.
-
6 Mnajua kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti mbili? Lakini Mungu hamsahau hata mmoja wao. 7 Naam, hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.
-
22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. 23 Wakatumwa na barua ifuatayo:
Sisi mitume na wazee, ndugu zenu,
Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia:
Salamu.
24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu. 25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, 26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia. 28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.
Kwaherini.
30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua. 31 Nao hao watu wakiisha kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo. 32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii, wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga katika imani wale ndugu walioamini. 33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma. [ 34 Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.] 35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana.
-
31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye? 33 Ni nani atakayewashtaki wale ambao Mungu amewateua? Ni Mungu mwenyewe ndiye mwenye kuwahesabia haki.
-
1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana.
-
13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari.
-
16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.
-
12 Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. 13 Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo. 14 Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.
-
9 Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. 10 Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.
11 Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, 12 ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.
-
10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.
12 Kwa msaada wa Silvano, ambaye ninamhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo, na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.
-
11 Mtafuteni Bwana na nguvu zake;
utafuteni uso wake siku zote.
-
22 Mtwike Bwana fadhaa zako,
naye atakutegemeza,
hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.
-
17 Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu;
uzithibitishe kazi za mikono yetu:
naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.
-
28 Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni,
uniimarishe sawasawa na neno lako.
-
2 Unapopita kwenye maji makuu,
nitakuwa pamoja nawe,
unapopita katika mito ya maji,
hayatakugharikisha.
Utakapopita katika moto,
hutaungua,
miali ya moto haitakuunguza.
-
40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.
-
27 Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini. 28 Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.
-
28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
-
13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.
-
14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.
20 Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, 21 yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.
-
3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. 4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, 5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. 6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.
-
15 Basi wewe fundisha mambo haya. Onya na kukaripia kwa mamlaka yote. Mtu yeyote asikudharau.
-
13 Kwa maana yeyote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki. 14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.
-
12 Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea. 13 Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe.
Shows Read in context, Share and Copy.