42 Bible Verses About Teens

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Teens
  1. 12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. 13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.

    15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. 16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.

  2. 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

    4 Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

  3. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.

  4. 1 Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,

    bali zitunze amri zangu moyoni mwako,

    2 kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako

    na kukuletea mafanikio.

    3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;

    vifunge shingoni mwako,

    viandike katika ubao wa moyo wako.

    4 Ndipo utapata kibali na jina zuri

    mbele za Mungu na mwanadamu.

    5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  5. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

    10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  6. 9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani?

    Ni kwa kutii, akilifuata neno lako.

    10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote,

    usiniache niende mbali na amri zako.

    11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu

    ili nisikutende dhambi.

  7. 12 Hivyo, yeye ajidhaniaye amesimama, aangalie asianguke. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  8. 4 Neno la Bwana lilinijia, kusema,

    5 “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua;

    kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum;

    nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”

    6 Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”

    7 Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza. 8 Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.

    9 Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako.

  9. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  10. 29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  11. 1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

    3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  12. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

  13. 9 Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana,

    moyo wako na ukupe furaha

    katika siku za ujana wako.

    Fuata njia za moyo wako

    na chochote macho yako yaonayo,

    lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote

    Mungu atakuleta hukumuni.

    10 Kwa hiyo basi, ondoa wasiwasi moyoni mwako

    na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako,

    kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.

  14. 10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,

    maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

    11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

    13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

    14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

  15. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  16. 8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  17. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  18. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  19. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

    11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. 12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi. 13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, 15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe: yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, 16 yeye peke yake ambaye hapatikani na mauti, na anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

  20. 105 Neno lako ni taa ya miguu yangu

    na mwanga katika njia yangu.

  21. 13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote. 14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya. 15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.

  22. 9 Yeyote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani. 10 Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu chochote ndani yake cha kumkwaza. 11 Lakini yeyote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakokwenda, kwa sababu giza limempofusha macho.

    12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,

    kwa sababu dhambi zenu

    zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.

    13 Nawaandikia ninyi, akina baba,

    kwa sababu mmemjua

    yeye aliye tangu mwanzo.

    Nawaandikia ninyi vijana

    kwa sababu mmemshinda yule mwovu.

    Nawaandikia ninyi watoto wadogo,

    kwa sababu mmemjua Baba.

    14 Nawaandikia ninyi akina baba,

    kwa sababu mmemjua

    yeye aliye tangu mwanzo.

    Nawaandikia ninyi vijana,

    kwa sababu mna nguvu,

    na neno la Mungu linakaa ndani yenu,

    nanyi mmemshinda yule mwovu.

    15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyo ulimwenguni. Kama mtu yeyote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake. 16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu. 17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.

  23. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

  24. 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

  25. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  26. 29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao.

  27. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

    10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha. 11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.

  28. 8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

    9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

    na mkufu wa kuipamba shingo yako.

  29. 1 Mkumbuke Muumba wako

    siku za ujana wako,

    kabla hazijaja siku za taabu,

    wala haijakaribia miaka utakaposema,

    “Mimi sifurahii hiyo”:

    2 kabla jua na nuru,

    nao mwezi na nyota havijatiwa giza,

    kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;

    3 siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka,

    nao watu wenye nguvu watakapojiinamisha,

    wakati wasagao watakapokoma kwa sababu ya uchache,

    nao wachunguliao madirishani kutiwa giza;

  30. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  31. 11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.

    12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

  32. 4 Sikia, ee Israeli: Bwana Mungu wako, Bwana ni mmoja. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  33. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

  34. 23 Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo,

    maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.

    24 Epusha kinywa chako na ukaidi;

    weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.

    25 Macho yako na yatazame mbele,

    kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.

    26 Sawazisha mapito ya miguu yako

    na njia zako zote ziwe zimethibitika.

    27 Usigeuke kulia wala kushoto;

    epusha mguu wako na ubaya.

  35. 6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

    naye hataiacha hata akiwa mzee.

  36. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

    6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi.

  37. 16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  38. 22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

  39. 7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

  40. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

  41. 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

  42. 6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.

    7 Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini vinafugika na vimefugwa na binadamu, 8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.

    9 Kwa ulimi tunamhimidi Bwana, yaani Baba yetu, na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu. 10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo.