57 Bible Verses About Worry

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Worry
  1. 25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?

    28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

  2. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  3. 5 Vivyo hivyo, ninyi mlio vijana watiini wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu kila mtu kwa mwenzake, kwa kuwa,

    “Mungu huwapinga wenye kiburi,

    lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

    6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

  4. 22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake: “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. 23 Maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. 24 Fikirini ndege! Wao hawapandi wala hawavuni, hawana ghala wala popote pa kuhifadhi nafaka; lakini Mungu huwalisha. Ninyi ni wa thamani zaidi kuliko ndege! 25 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake? 26 Kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini basi kuyasumbukia hayo mengine?

    27 “Angalieni maua jinsi yameavyo: Hayafanyi kazi wala hayafumi. Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 28 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo, na kesho yanatupwa motoni, si atawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba! 29 Wala msisumbuke mioyoni mwenu mtakula nini au mtakunywa nini. Msiwe na wasiwasi juu ya haya. 30 Watu wa mataifa ya duniani husumbuka sana kuhusu vitu hivi vyote, lakini Baba yenu anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 31 Bali utafuteni Ufalme wa Mungu, na haya yote atawapa pia.

    32 “Msiogope enyi kundi dogo, kwa maana Baba yenu ameona vyema kuwapa ninyi Ufalme. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  5. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

    13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    nikushikaye mkono wako wa kuume

    na kukuambia, Usiwe na hofu,

    nitakusaidia.

  6. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

    28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi.

  7. 18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”

    Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.

    19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,

    faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.

  8. 25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,

    bali neno la huruma humfurahisha.

  9. 5 Hili ndilo asemalo Bwana:

    “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu,

    ategemeaye mwenye mwili

    kwa ajili ya nguvu zake,

    ambaye moyo wake

    umemwacha Bwana.

    6 Atakuwa kama kichaka cha jangwani;

    hataona mafanikio yatakapokuja.

    Ataishi katika sehemu zisizo na maji,

    katika nchi ya chumvi ambapo

    hakuna yeyote aishiye humo.

    7 “Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana,

    ambaye matumaini yake ni katika Bwana.

    8 Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji

    uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji.

    Hauogopi wakati wa joto ujapo;

    majani yake ni mabichi daima.

    Hauna hofu katika mwaka wa ukame

    na hautaacha kuzaa matunda.”

  10. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

  11. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

    41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

  12. Zaburi ya Daudi.

    1 Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu,

    wala usiwaonee wivu watendao mabaya,

    2 kwa maana kama majani watanyauka mara,

    kama mimea ya kijani watakufa mara.

    3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema;

    Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama.

    4 Jifurahishe katika Bwana

    naye atakupa haja za moyo wako.

    5 Mkabidhi Bwana njia yako,

    mtumaini yeye, naye atatenda hili:

    6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko,

    na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri.

    7 Tulia mbele za Bwana

    na umngojee kwa uvumilivu;

    usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao,

    wanapotekeleza mipango yao miovu.

    8 Epuka hasira na uache ghadhabu,

    usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu.

    9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali,

    bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi.

  13. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  14. 22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.

  15. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

  16. 5 Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

    “Kamwe sitakuacha,

    wala sitakupungukia.”

    6 Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

    “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.

    Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

    7 Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao.

  17. 3 Wakati ninapoogopa,

    nitakutumaini wewe.

    4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,

    katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.

    Mwanadamu apatikanaye na kufa,

    atanitenda nini?

  18. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  19. 26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.

    28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  20. 31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu? 32 Ikiwa Mungu hakumhurumia Mwanawe, bali alimtoa kwa ajili yetu sote, atakosaje basi kutupatia vitu vyote kwa ukarimu pamoja naye?

  21. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. 14 Nitaonekana kwenu,” asema Bwana, “nami nitawarudisha watu wenu waliotekwa. Nitawakusanya kutoka mataifa yote na mahali pote nilipokuwa nimewafukuzia, nami nitawarudisha mahali ambapo nilikuwa nimewatoa walipochukuliwa uhamishoni,” asema Bwana.

  22. 4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  23. 4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,

    akaniokoa kwenye hofu zangu zote.

    5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,

    nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.

    6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,

    akamwokoa katika taabu zake zote.

    7 Malaika wa Bwana hufanya kituo

    akiwazunguka wale wamchao,

    naye huwaokoa.

    8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,

    heri mtu yule anayemkimbilia.

  24. 1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

    yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

    “Usiogope kwa maana nimekukomboa,

    nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

    2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

    3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

    Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

    Kushi na Seba badala yako.

    4 Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu,

    nami kwa kuwa ninakupenda,

    nitatoa watu badala yako

    na mataifa badala ya maisha yako.

  25. 11 “Watakapowapeleka katika masinagogi, na mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema. 12 Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati huo huo mnachopaswa kusema.”

  26. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  27. 32 Ningetaka msiwe na masumbufu. Mwanaume ambaye hajaoa anajishughulisha na mambo ya Bwana, jinsi ya kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa anajishughulisha na mambo ya dunia, jinsi ya kumfurahisha mkewe, 34 na mawazo yake yamegawanyika. Mwanamke asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana: lengo lake ni awe mtakatifu kimwili na kiroho. Lakini yule aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia, jinsi atakavyoweza kumfurahisha mumewe.

  28. 28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote.

  29. 15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani.

  30. 17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu. 18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.

    19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza.

  31. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

    2 Waovu watakaposogea dhidi yangu

    ili wanile nyama yangu,

    adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

    watajikwaa na kuanguka.

    3 Hata jeshi linizunguke pande zote,

    moyo wangu hautaogopa;

    hata vita vitokee dhidi yangu,

    hata hapo nitakuwa na ujasiri.

  32. 3 Utamlinda katika amani kamilifu

    yeye ambaye moyo wake ni thabiti

    kwa sababu anakutumaini wewe.

  33. 3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu,

    yafanyeni imara magoti yaliyolegea,

    4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu,

    “Kuweni hodari, msiogope;

    tazama, Mungu wenu atakuja,

    pamoja na malipo ya Mungu,

    atakuja na kuwaokoa ninyi.”

  34. 16 Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

  35. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Nayainua macho yangu nitazame vilima,

    msaada wangu utatoka wapi?

    2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana,

    Muumba wa mbingu na dunia.

  36. 30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  37. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  38. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

    14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu.

  39. 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi.

    8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,

  40. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  41. 10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;

    nitatukuzwa katikati ya mataifa,

    nitatukuzwa katika dunia.”

    11 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi;

    Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

  42. 11 Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.

  43. 20 Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akaanguka chini katika kuabudu 21 na kusema:

    “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi,

    nami nitaondoka uchi,

    Bwana alinipa, naye Bwana ameviondoa,

    jina la Bwana litukuzwe.”

  44. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ndiye mchungaji wangu,

    sitapungukiwa na kitu.

  45. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

    3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

    milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

  46. 35 Siku hiyo ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo.” 36 Wakauacha ule umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye. 37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji. 38 Yesu alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

    39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

    40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

    41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

  47. 34 “Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama vile mtego unasavyo.

  48. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  49. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  50. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  51. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  52. 15 Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”

    16 Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.”

    17 Kisha Elisha akaomba, “Ee Bwana, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Elisha pande zote.

  53. 22 Mtu atapata nini kwa taabu yote na kuhangaika kwa bidii katika kazi anayotaabikia chini ya jua? 23 Siku zake zote kazi yake ni maumivu na masikitiko, hata usiku akili yake haipati mapumziko. Hili nalo pia ni ubatili.

  54. 22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

    25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,

    kwa yule ambaye humtafuta;

  55. 14 Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15 Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga.

  56. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

  57. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”