47 Bible Verses About Heaven

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Heaven
  1. 1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

    5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”

    6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yoyote. 7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

  2. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

    5 Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui unakokwenda, tutaijuaje njia?”

    6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.

  3. 9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema:

    “Wokovu una Mungu wetu,

    yeye aketiye kwenye kiti cha enzi,

    na Mwana-Kondoo!”

    11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, 12 wakisema:

    “Amen!

    Sifa na utukufu

    na hekima na shukrani na heshima

    na uweza na nguvu

    viwe kwa Mungu wetu milele na milele.

    Amen!”

    13 Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

  4. 1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo, 2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa. 3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

  5. 1 Kwa maana twajua kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 2 Katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, 3 kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena kuwa uchi.

  6. 20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, 21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

  7. 1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.

  8. 19 Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi, 20 wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto. 21 Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji huo ilikuwa ya dhahabu safi ingʼaayo kama kioo.

    22 Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio hekalu lake. 23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. 24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake. 25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo. 26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo. 27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

  9. 22 Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia, 23 kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa, 24 kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Abeli.

  10. 27 “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga!

  11. 2 Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. 3 Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, 4 alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia.

  12. 10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

    11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

    14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari.

  13. 19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

  14. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

  15. 9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

    “Wewe unastahili kukitwaa kitabu

    na kuzivunja lakiri zake,

    kwa sababu ulichinjwa

    na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu

    kutoka kila kabila, kila lugha,

    kila jamaa na kila taifa.

    10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani

    wa kumtumikia Mungu wetu,

    nao watatawala duniani.”

    11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:

    “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,

    kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu

    na heshima na utukufu na sifa!”

    13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:

    “Sifa na heshima na utukufu na uweza

    ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi

    na kwa Mwana-Kondoo,

    milele na milele!”

    14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

  16. 2 Ghafula nilikuwa katika Roho, na hapo mbele yangu kilikuwepo kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu. 3 Aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua ulioonekana kama zumaridi.

    4 Kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti vingine vya enzi ishirini na vinne, na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne. Walivaa mavazi meupe, na walikuwa na taji za dhahabu vichwani mwao. 5 Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya umeme wa radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya kiti cha enzi, taa saba zilikuwa zinawaka. Hizi ndizo roho saba za Mungu. 6 Pia mbele ya kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama bilauri.

    Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma. 7 Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ngʼombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. 8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:

    “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

    ni Bwana Mungu Mwenyezi,

    aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

  17. 44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

    45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

  18. 33 Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwizi hakaribii wala nondo haharibu. 34 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo moyo wako utakapokuwa pia.

  19. 5 Kwa habari ya mambo haya mjue hakika kwamba: Msherati, wala mtu mwovu, wala mwenye tamaa mbaya, mtu kama huyo ni mwabudu sanamu, kamwe hataurithi Ufalme wa Kristo na wa Mungu.

  20. 4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu;

    Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni.

    Huwaangalia wana wa watu,

    macho yake yanawajaribu.

    5 Bwana huwajaribu wenye haki,

    lakini waovu na wanaopenda jeuri,

    nafsi yake huwachukia.

    6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali

    na kiberiti kinachowaka,

    upepo wenye joto kali ndio fungu lao.

    7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki,

    yeye hupenda haki.

    Wanyofu watauona uso wake.

  21. 24 Je, mtu yeyote aweza kujificha

    mahali pa siri ili nisiweze kumwona?”

    Bwana asema.

    “Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?”

    Bwana asema.

  22. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

  23. 34 Yesu akawajibu, “Katika maisha haya watu huoa na kuolewa. 35 Lakini wale ambao wamehesabiwa kwamba wanastahili kupata nafasi katika ulimwengu ule na katika ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaolewi. 36 Hawa hawawezi kufa tena, kwa maana wao ni kama malaika. Wao ni watoto wa Mungu, kwa sababu ni watoto wa ufufuo.

  24. 21 “Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.

  25. 1 Hili ndilo asemalo Bwana,

    “Mbingu ni kiti changu cha enzi,

    nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.

    Iko wapi nyumba mtakayoijenga kwa ajili yangu?

    Mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

  26. 29 Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. 30 Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni.

  27. 6 na kwenda nyumbani. Kisha huwaita rafiki zake na majirani, na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami; nimempata kondoo wangu aliyepotea.’ 7 Nawaambieni, vivyo hivyo kutakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa wenye haki tisini na tisa ambao hawana haja ya kutubu.”

  28. 1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu.

  29. 15 Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake. 16 Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama kilomita 2,200; urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa. 17 Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144 kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia. 18 Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, ikingʼaa kama kioo.

  30. 17 “Tazama, nitaumba

    mbingu mpya na dunia mpya.

    Mambo ya zamani hayatakumbukwa,

    wala hayatakuja akilini.

    18 Lakini furahini na kushangilia daima

    katika hivi nitakavyoumba,

    kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,

    nao watu wake wawe furaha.

  31. 13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Bwana tangu sasa.”

    “Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

  32. 15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.

    16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ingʼaayo.”

    17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

  33. 22 “Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23 Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake.

  34. 12 Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni? 13 Hakuna mtu yeyote aliyekwenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu.

  35. 12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni kitabu cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu. 13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyoyatenda. 14 Kisha mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. 15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.

  36. 11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana,

    ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;

  37. 11 Wale waliolipiwa fidia na Bwana watarudi.

    Wataingia Sayuni wakiimba;

    furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.

    Furaha na shangwe zitawapata,

    huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.

  38. 46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

  39. 9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu;

  40. 23 Kwa hiyo, ilikuwa muhimu kwa nakala za vitu vile vya mbinguni vitakaswe kwa dhabihu hizi, lakini vitu halisi vya mbinguni vilihitaji dhabihu bora kuliko hizi.

  41. 12 Nikatazama akiivunja ile lakiri ya sita. Pakatokea tetemeko kuu la nchi, na jua likawa jeusi kama nguo ya gunia iliyotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. 13 Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. 14 Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.

  42. 6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

  43. 12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,

    ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko!

    Umetupwa chini duniani,

    wewe uliyepata kuangusha mataifa!

    13 Ulisema moyoni mwako,

    “Nitapanda juu hadi mbinguni,

    nitakiinua kiti changu cha enzi

    juu ya nyota za Mungu,

    nitaketi nimetawazwa

    juu ya mlima wa kusanyiko,

    kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

    14 Nitapaa juu kupita mawingu,

    nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”

    15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu,

    hadi kwenye vina vya shimo.

  44. 13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. 14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

    15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali.

  45. 11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana.

  46. 6 Juu ya mlima huu Bwana Mwenye Nguvu Zote ataandaa

    karamu ya vinono kwa mataifa yote,

    karamu ya mvinyo wa zamani,

    nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

    7 Juu ya mlima huu ataharibu

    sitara ihifadhiyo mataifa yote,

    kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

    8 yeye atameza mauti milele.

    Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

    ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

    Bwana amesema hili.

  47. 1 Kisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. 3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani.