50 Bible Verses About God's Creation

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About God's Creation
  1. 1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.

    3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.

    6 Mungu akasema, “Iwepo nafasi kati ya maji igawe maji na maji.” 7 Kwa hiyo Mungu akafanya nafasi, akatenganisha maji yaliyo chini ya hiyo nafasi na maji yaliyo juu yake. Ikawa hivyo. 8 Mungu akaiita hiyo nafasi “anga.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya pili.

    9 Mungu akasema, “Maji yaliyopo chini ya anga na yakusanyike mahali pamoja, pawepo na nchi kavu.” Ikawa hivyo. 10 Mungu akaiita nchi kavu “ardhi,” nalo lile kusanyiko la maji akaliita “bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.

    11 Kisha Mungu akasema, “Ardhi na itoe mimea: miche itoayo mbegu, miti juu ya nchi itoayo matunda yenye mbegu ndani yake, kila mmea kulingana na aina zake mbalimbali.” Ikawa hivyo. 12 Ardhi ikachipua mimea: Mimea itoayo mbegu kulingana na aina zake, na miti itoayo matunda yenye mbegu kulingana na aina zake. Mungu akaona ya kuwa hili ni jema. 13 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tatu.

    14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.

    20 Mungu akasema, “Kuwepo na viumbe hai tele kwenye maji, nao ndege waruke juu ya dunia katika nafasi ya anga.” 21 Kwa hiyo Mungu akaumba viumbe wakubwa wa baharini na kila kiumbe hai kiendacho majini kulingana na aina zake, na kila ndege mwenye mabawa kulingana na aina yake. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 22 Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni mwongezeke, mkayajaze maji ya bahari, nao ndege waongezeke katika dunia.” 23 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya tano.

    24 Mungu akasema, “Ardhi na itoe viumbe hai kulingana na aina zake: wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo ardhini na wanyama pori, kila mnyama kulingana na aina yake.” Ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya wanyama pori kulingana na aina zake, wanyama wa kufugwa kulingana na aina zake, na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi kulingana na aina zake. Mungu akaona kuwa hili ni jema.

    26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.”

    27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

    28 Mungu akawabariki na akawaambia, “Zaeni na mkaongezeke, mkaijaze tena dunia na kuitiisha. Mkatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kiendacho juu ya ardhi.”

    29 Kisha Mungu akasema, “Nimewapa kila mche utoao mbegu juu ya uso wa dunia yote, na kila mti wenye matunda yenye mbegu ndani yake. Vitakuwa chakula chenu. 30 Nao wanyama wote wa dunia, ndege wote wa angani, na viumbe vyote viendavyo juu ya ardhi: yaani kila kiumbe chenye pumzi ya uhai, ninawapa kila mche wa kijani kuwa chakula.” Ikawa hivyo.

    31 Mungu akaona vyote alivyoumba, na tazama, ilikuwa vizuri sana. Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya sita.

  2. 8 Basi Bwana Mungu alikuwa ameotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, huko akamweka huyo mtu aliyemuumba. 9 Bwana Mungu akafanya aina zote za miti ziote kutoka ardhini, miti yenye kupendeza macho na mizuri kwa chakula. Katikati ya bustani ulikuwepo mti wa uzima na mti wa kujua mema na mabaya.

    10 Mto wa kunyeshea bustani ulitiririka toka Edeni, kuanzia hapa ukagawanyika kuwa mito minne. 11 Mto wa kwanza uliitwa Pishoni, nao huzunguka nchi yote ya Havila ambako kuna dhahabu. 12 (Dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri, bedola na vito shohamu pia hupatikana huko.) 13 Jina la mto wa pili ni Gihoni, ambao huzunguka nchi yote ya Kushi. 14 Jina la mto wa tatu ni Tigrisi, unaopita mashariki ya Ashuru. Mto wa nne ni Frati.

    15 Bwana Mungu akamchukua huyo mtu, akamweka kwenye Bustani ya Edeni ailime na kuitunza. 16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akamwambia, “Uko huru kula matunda ya mti wowote katika bustani, 17 lakini kamwe usile matunda ya mti wa kujua mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda yake, hakika utakufa.”

    18 Bwana Mungu akasema, “Si vyema huyu mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kumfaa.”

    19 Basi Bwana Mungu alikuwa amefanyiza kutoka ardhi wanyama wote wa porini na ndege wote wa angani. Akawaleta kwa huyu mtu aone atawaitaje, nalo jina lolote alilokiita kila kiumbe hai, likawa ndilo jina lake. 20 Hivyo Adamu akawapa majina wanyama wote wa kufugwa, ndege wa angani, na wanyama wote wa porini.

    Lakini kwa Adamu hakupatikana msaidizi wa kumfaa. 21 Hivyo Bwana Mungu akamfanya Adamu kulala usingizi mzito, naye alipokuwa amelala akachukua moja ya mbavu zake, akapafunika mahali pale kwa nyama. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.

    23 Huyo mwanaume akasema,

    “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu

    na nyama ya nyama yangu,

    ataitwa ‘mwanamke,’

    kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

    24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

    25 Adamu na mkewe wote wawili walikuwa uchi, wala hawakuona aibu.

  3. 15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote. 19 Kwa kuwa ilimpendeza Mungu kwamba utimilifu wake wote ukae ndani yake, 20 na kwa njia yake aweze kuvipatanisha vitu vyote na yeye mwenyewe, viwe ni vitu vilivyo duniani au vilivyo mbinguni, kwa kufanya amani kwa damu yake, iliyomwagika msalabani.

  4. 1 Kwa hiyo mbingu na dunia zikakamilika, pamoja na vyote vilivyomo.

    2 Katika siku ya saba Mungu alikuwa amekamilisha kazi aliyokuwa akiifanya, hivyo siku ya saba akapumzika kutoka kazi zake zote. 3 Mungu akaibariki siku ya saba akaifanya takatifu, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kazi zote za kuumba alizokuwa amefanya.

  5. 1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. 3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni. 4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.

  6. 18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao, 19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

    21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

    24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

  7. 1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.

    3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.

  8. 5 Bwana hupenda uadilifu na haki;

    dunia imejaa upendo wake usiokoma.

    6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,

    jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.

    7 Ameyakusanya maji ya bahari

    kama kwenye chungu;

    vilindi vya bahari

    ameviweka katika ghala.

    8 Dunia yote na imwogope Bwana,

    watu wote wa dunia wamche.

    9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,

    aliamuru na ikasimama imara.

  9. 3 Nikiziangalia mbingu zako,

    kazi ya vidole vyako,

    mwezi na nyota,

    ulizoziratibisha,

    4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,

    binadamu ni nani hata unamjali?

    5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni,

    ukamvika taji ya utukufu na heshima.

    6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako;

    umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.

    7 Mifugo na makundi yote pia,

    naam, na wanyama wa kondeni,

    8 ndege wa angani na samaki wa baharini,

    naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari.

    9 Ee Bwana, Bwana wetu,

    tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

  10. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu,

    anga zahubiri kazi ya mikono yake.

    2 Siku baada ya siku zinatoa habari,

    usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.

    3 Hakuna msemo wala lugha,

    ambapo sauti zao hazisikiki.

    4 Sauti yao imeenea duniani pote,

    nayo maneno yao yameenea

    hadi miisho ya ulimwengu.

    Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,

    5 linafanana na bwana arusi

    akitoka chumbani mwake,

    kama shujaa afurahiavyo

    kukamilisha kushindana kwake.

    6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu,

    na kufanya mzunguko wake

    hadi upande mwingine.

    Hakuna kilichojificha joto lake.

  11. 3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.

  12. 18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote vinangoja kwa shauku kudhihirishwa kwa watoto wa Mungu. 20 Kwa kuwa viumbe vyote viliwekwa chini ya ubatili, si kwa chaguo lao, bali kwa mapenzi yake yeye aliyevitiisha katika tumaini, 21 ili kwamba viumbe vyote vipate kuwekwa huru kutoka kwa utumwa wa kuharibika na kupewa uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.

    22 Kwa maana twajua ya kuwa hata sasa viumbe vyote vimekuwa vikilia kwa maumivu kama utungu wa mwanamke wakati wa kuzaa. 23 Wala si hivyo viumbe peke yao, bali hata sisi ambao ndio matunda ya kwanza ya Roho, kwa ndani tunalia kwa uchungu tukisubiri kwa shauku kufanywa wana wa Mungu, yaani, ukombozi wa miili yetu.

  13. 22 Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana. 23 Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.

    24 “Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 ‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

    29 “Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

    32 Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.” 33 Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao. 34 Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.

  14. 11 “Bwana wetu na Mungu wetu,

    wewe unastahili kupokea utukufu

    na heshima na uweza,

    kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,

    na kwa mapenzi yako viliumbwa

    na vimekuwako.”

  15. 6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

  16. 7 Bwana Mungu alimuumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, naye mtu akawa kiumbe hai.

  17. 8 Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase. 9 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote, 10 lakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11 Kwa kuwa kwa siku sita, Bwana aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.

  18. 3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,

    mfalme mkuu juu ya miungu yote.

    4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,

    na vilele vya milima ni mali yake.

    5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya,

    na mikono yake iliumba nchi kavu.

    6 Njooni, tusujudu, tumwabudu,

    tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu,

    7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu,

    na sisi ni watu wa malisho yake,

    kondoo chini ya utunzaji wake.

    Kama mkiisikia sauti yake leo,

  19. 1 Msifuni Bwana.

    Msifuni Bwana kutoka mbinguni,

    msifuni juu vileleni.

    2 Msifuni, enyi malaika wake wote,

    msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.

    3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,

    msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.

    4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,

    na ninyi maji juu ya anga.

    5 Vilisifu jina la Bwana

    kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.

    6 Aliviweka mahali pake milele na milele,

    alitoa amri ambayo haibadiliki milele.

    7 Mtukuzeni Bwana kutoka duniani,

    ninyi viumbe vikubwa vya baharini na vilindi vyote vya bahari,

    8 umeme wa radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu,

    pepo za dhoruba zinazofanya amri zake,

    9 ninyi milima na vilima vyote,

    miti ya matunda na mierezi yote,

    10 wanyama wa mwituni na mifugo yote,

    viumbe vidogo na ndege warukao,

    11 wafalme wa dunia na mataifa yote,

    ninyi wakuu na watawala wote wa dunia,

    12 wanaume vijana na wanawali,

    wazee na watoto.

    13 Wote na walisifu jina la Bwana,

    kwa maana jina lake pekee limetukuka,

    utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu.

    14 Amewainulia watu wake pembe,

    sifa ya watakatifu wake wote,

    ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake.

    Msifuni Bwana.

  20. 3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.

    4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake.

    6 “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu,

    damu yake itamwagwa na mwanadamu,

    kwa kuwa katika mfano wa Mungu,

    Mungu alimuumba mwanadamu.

  21. Zaburi ya Daudi.

    1 Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake,

    ulimwengu, na wote waishio ndani yake,

    2 maana aliiwekea misingi yake baharini

    na kuifanya imara juu ya maji.

  22. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

  23. 5 Hili ndilo asemalo Mungu, Bwana,

    yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,

    aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo,

    awapaye watu wake pumzi,

    na uzima kwa wale waendao humo:

    6 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki;

    nitakushika mkono wako.

    Nitakulinda na kukufanya

    kuwa Agano kwa ajili ya watu

    na nuru kwa Mataifa,

    7 kuwafungua macho wale wasioona,

    kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,

    na kuwafungua kutoka gerezani

    wale wanaokaa gizani.

    8 “Mimi ndimi Bwana; hilo ndilo Jina langu!

    Sitampa mwingine utukufu wangu

    wala sanamu sifa zangu.

    9 Tazama, mambo ya kwanza yametokea,

    nami natangaza mambo mapya;

    kabla hayajatokea

    nawatangazia habari zake.”

    10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya,

    sifa zake toka miisho ya dunia,

    ninyi mshukao chini baharini,

    na vyote vilivyomo ndani yake,

    enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.

  24. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  25. 7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu;

    naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu.

    8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake,

    hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.

    9 Huufunika uso wa mwezi mpevu,

    akitandaza mawingu juu yake.

    10 Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji,

    ameweka mpaka wa nuru na giza.

    11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka,

    zinatishika anapozikemea.

    12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari;

    kwa hekima yake alimkata Rahabu vipande vipande.

    13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake;

    kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.

    14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;

    tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!

    Ni nani basi awezaye kuelewa

    ngurumo za nguvu zake?”

  26. 5 Kwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa miungu, kama wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi), 6 kwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi; na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.

  27. 4 Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 Lakini kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

    8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili: kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.

    10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

    11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

  28. 16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

    17 Kwa Adamu akasema, “Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru, ‘Msile tunda lake,’

    “Ardhi imelaaniwa kwa sababu yako,

    kwa kazi ngumu utakula chakula kitokacho humo

    siku zote za maisha yako.

    18 Itazaa miiba na mibaruti kwa ajili yako,

    nawe utakula mimea ya shambani.

    19 Kwa jasho la uso wako

    utakula chakula chako

    hadi utakaporudi ardhini,

    kwa kuwa ulitwaliwa kutoka humo,

    kwa kuwa wewe u mavumbi

    na mavumbini wewe utarudi.”

  29. 7 “Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,

    au ndege wa angani, nao watawaambia;

    8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,

    au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.

    9 Ni nani miongoni mwa hawa wote asiyejua

    kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?

    10 Mkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,

    na pumzi ya wanadamu wote.

    11 Je, sikio haliyajaribu maneno

    kama vile ulimi uonjavyo chakula?

    12 Je, hekima haipatikani katikati ya wazee?

    Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?

  30. 2 Mwabuduni Bwana kwa furaha;

    njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.

    3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu.

    Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake;

    sisi tu watu wake,

    kondoo wa malisho yake.

  31. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  32. 10 Pia asema,

    “Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia,

    nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

    11 Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu;

    zote zitachakaa kama vazi.

    12 Utazikungʼutakungʼuta kama joho,

    nazo zitachakaa kama vazi.

    Lakini wewe hubadiliki,

    nayo miaka yako haikomi kamwe.”

  33. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

  34. 6 Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’

    nayo kusini, ‘Usiwazuie.’

    Walete wana wangu kutoka mbali,

    na binti zangu kutoka miisho ya dunia:

    7 kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu,

    niliyemuumba kwa utukufu wangu,

    niliyemhuluku na kumfanya.”

  35. 11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ”

    12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,

    akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,

    na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

    13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;

    huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.

    Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,

    naye huuleta upepo kutoka ghala zake.

  36. 8 Katika mji wa Listra, alikuwako kiwete, ambaye alikuwa amelemaa tangu kuzaliwa na hakuwa ametembea kamwe. 9 Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa. 10 Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!

    11 Ule umati wa watu ulipoona yaliyokuwa yamefanywa na Paulo, wakapiga kelele kwa lugha yao ya Kilikaonia wakasema, “Miungu imetushukia katika umbo la binadamu!” 12 Wakamwita Barnaba Zeu na Paulo wakamwita Herme kwa kuwa ndiye alikuwa msemaji mkuu. 13 Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye na ule umati wa watu walitaka kuwatolea dhabihu.

    14 Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia haya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema, 15 “Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo. 16 Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka. 17 Lakini hakuacha kuwaonyesha watu uwepo wake: Ameonyesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.” 18 Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuuzuia ule umati wa watu kuwatolea dhabihu.

  37. Sehemu Ya Nne: Mungu Anazungumza

    1 Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:

    2 “Nani huyu atiaye mashauri yangu giza

    kwa maneno yasiyo na maarifa?

    3 Jikaze kama mwanaume;

    nitakuuliza swali,

    nawe unijibu.

    4 “Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?

    Niambie, kama unafahamu.

    5 Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?

    Hakika wewe unajua!

    Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?

    6 Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,

    au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,

    7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,

    na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?

    8 “Ni nani aliyeifungia bahari milango

    ilipopasuka kutoka tumbo,

    9 nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake,

    na kuyafungia katika giza nene,

    10 nilipoamuru mipaka yake,

    na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,

    11 niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi;

    hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?

    12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke,

    au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,

    13 yapate kushika miisho ya dunia,

    na kuwakungʼuta waovu waliomo?

    14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri;

    sura yake hukaa kama ile ya vazi.

    15 Waovu huzuiliwa nuru yao,

    nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.

    16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?

    Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?

    17 Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti?

    Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?

    18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia?

    Niambie kama unajua haya yote.

    19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi?

    Nako maskani mwa giza ni wapi?

    20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake?

    Unajua njia za kufika maskani mwake?

    21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa!

    Kwani umeishi miaka mingi!

    22 “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji,

    au kuona ghala za mvua ya mawe,

    23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu,

    na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?

    24 Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa,

    au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?

    25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi

    na njia ya umeme wa radi,

    26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,

    jangwa lisilo na yeyote ndani yake,

    27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,

    na majani yaanze kumea ndani yake?

    28 Je, mvua ina baba?

    Ni nani baba azaaye matone ya umande?

    29 Barafu inatoka tumbo la nani?

    Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,

    30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,

    wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?

    31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?

    Waweza kulegeza kamba za Orioni?

    32 Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake,

    au kuongoza Dubu na watoto wake?

    33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?

    Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?

    34 “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni,

    na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?

    35 Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?

    Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?

    36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima

    au kuzipa akili ufahamu?

    37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?

    Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni

    38 wakati mavumbi yawapo magumu,

    na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?

    39 “Je, utamwindia simba jike mawindo,

    na kuwashibisha simba wenye njaa

    40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao,

    au wakivizia kichakani?

    41 Ni nani ampaye kunguru chakula

    wakati makinda yake yanamlilia Mungu,

    yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?

  38. 25 Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia,

    nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

    26 Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu,

    zote zitachakaa kama vazi.

    Utazibadilisha kama nguo

    nazo zitaondoshwa.

    27 Lakini wewe, U yeye yule,

    nayo miaka yako haikomi kamwe.

  39. 1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

    Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana,

    umejivika utukufu na enzi.

    2 Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi,

    amezitandaza mbingu kama hema

    3 na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji.

    Huyafanya mawingu kuwa gari lake,

    na hupanda kwenye mbawa za upepo.

    4 Huzifanya pepo kuwa wajumbe wake,

    miali ya moto watumishi wake.

    5 Ameiweka dunia kwenye misingi yake,

    haiwezi kamwe kuondoshwa.

    6 Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi,

    maji yalisimama juu ya milima.

    7 Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia,

    kwa sauti ya radi yako yakatoroka,

    8 yakapanda milima, yakateremka mabondeni,

    hadi mahali pale ulipoyakusudia.

    9 Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka,

    kamwe hayataifunika dunia tena.

    10 Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni,

    hutiririka kati ya milima.

    11 Huwapa maji wanyama wote wa kondeni,

    punda-mwitu huzima kiu yao.

    12 Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji,

    huimba katikati ya matawi.

    13 Huinyeshea milima kutoka orofa zake,

    dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake.

    14 Huyafanya majani ya mifugo yaote,

    na mimea kwa watu kulima,

    wajipatie chakula kutoka ardhini:

    15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu,

    mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake,

    na mkate wa kutia mwili nguvu.

    16 Miti ya Bwana inanyeshewa vizuri,

    mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.

    17 Humo ndege hufanya viota vyao,

    korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.

    18 Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu,

    majabali ni kimbilio la pelele.

    19 Mwezi hugawanya majira,

    na jua hutambua wakati wake wa kutua.

    20 Unaleta giza, kunakuwa usiku,

    wanyama wote wa mwituni huzurura.

    21 Simba hunguruma kwa mawindo yao,

    na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.

    22 Jua huchomoza, nao huondoka,

    hurudi na kulala katika mapango yao.

    23 Kisha mwanadamu huenda kazini mwake,

    katika kazi yake mpaka jioni.

    24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi!

    Kwa hekima ulizifanya zote,

    dunia imejaa viumbe vyako.

    25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele,

    imejaa viumbe visivyo na idadi,

    vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.

    26 Huko meli huenda na kurudi,

    pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake.

    27 Hawa wote wanakutazamia wewe,

    uwape chakula chao kwa wakati wake.

    28 Wakati unapowapa,

    wanakikusanya,

    unapofumbua mkono wako,

    wao wanashibishwa mema.

    29 Unapoficha uso wako,

    wanapata hofu,

    unapoondoa pumzi yao,

    wanakufa na kurudi mavumbini.

    30 Unapopeleka Roho wako,

    wanaumbwa,

    nawe huufanya upya uso wa dunia.

    31 Utukufu wa Bwana na udumu milele,

    Bwana na azifurahie kazi zake:

    32 yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka,

    aigusaye milima, nayo ikatoa moshi.

    33 Nitamwimbia Bwana maisha yangu yote;

    nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.

    34 Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye,

    ninapofurahi katika Bwana.

    35 Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia

    na waovu wasiwepo tena.

    Ee nafsi yangu, msifu Bwana.

    Msifuni Bwana.

  40. 17 “Tazama, nitaumba

    mbingu mpya na dunia mpya.

    Mambo ya zamani hayatakumbukwa,

    wala hayatakuja akilini.

    18 Lakini furahini na kushangilia daima

    katika hivi nitakavyoumba,

    kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,

    nao watu wake wawe furaha.

    19 Nami nitaifurahia Yerusalemu

    na kuwafurahia watu wangu;

    sauti ya maombolezo na ya kilio

    haitasikika humo tena.

  41. 4 Roho wa Mungu ameniumba;

    pumzi ya Mwenyezi hunipa uhai.

  42. 18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyeumba mbingu,

    ndiye Mungu;

    yeye aliyeifanya dunia na kuiumba,

    yeye ndiye aliiwekea misingi imara,

    hakuiumba ili iwe tupu,

    bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.

    Anasema:

    “Mimi ndimi Bwana,

    wala hakuna mwingine.

  43. 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?

    28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba?

  44. 1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

    5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”

  45. 1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

    2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

    4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

    6 Mwanamke alipoona ya kuwa tunda la mti huo lilikuwa zuri kwa chakula na la kupendeza macho, tena linatamanika kwa kujipatia hekima, basi akachuma katika matunda yake, akala, pia akampa mumewe, aliyekuwa pamoja naye, naye akala.

  46. 1 Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu.

    Wakati Mungu alipomuumba Adamu, alimfanya kwa sura ya Mungu.

  47. 25 “Utanilinganisha mimi na nani?

    Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.

    26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni:

    Ni nani aliyeumba hivi vyote?

    Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine

    na kuziita kila moja kwa jina lake.

    Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,

    hakuna hata mojawapo inayokosekana.

  48. 17 “Ee Bwana Mwenyezi, umeumba mbingu na nchi kwa uwezo wako mkuu na kwa mkono ulionyooshwa. Hakuna jambo lililo gumu usiloliweza.

  49. 10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua.

  50. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.