85 Bible Verses About Jesus

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Jesus
  1. 5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

    9 Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana,

    na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,

    10 ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,

    la vitu vya mbinguni, na vya duniani,

    na vya chini ya nchi,

    11 na kila ulimi ukiri ya kwamba

    Yesu Kristo ni Bwana,

    kwa utukufu wa Mungu Baba.

  2. 6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. 7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”

    8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”

    9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo.

  3. 7 Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. 8 Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia. 9 Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

    11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. 13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.

    14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

  4. 1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.

    3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.

  5. 14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.

  6. 11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita. 12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe. 13 Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.” 14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri. 15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi. 16 Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili:

    Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.

  7. 1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

    “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. 2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. 3 Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. 4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. 5 Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo.

  8. 9 Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani. 10 Yesu alipokuwa akitoka ndani ya maji, aliona mbingu zikifunguka na Roho akishuka juu yake kama hua. 11 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”

    12 Wakati huo huo, Roho akamwongoza Yesu kwenda nyikani, 13 naye akawa huko nyikani kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikaa na wanyama wa mwituni, nao malaika wakamhudumia.

  9. 1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. 3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.

  10. 16 Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu. 17 Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu. 18 Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.

  11. 24 Lakini kwa sababu Yesu anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu. 25 Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.

    26 Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani, aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu. 27 Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe. 28 Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu; lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.

  12. 14 Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. 15 Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

    16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  13. 23 Kisha akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. 24 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa. 25 Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akapoteza au kuangamiza nafsi yake? 26 Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba, pamoja na malaika watakatifu.

  14. 17 Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.” 18 Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumuua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.

    19 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, Mwana hawezi kufanya jambo lolote peke yake, yeye aweza tu kufanya lile analomwona Baba yake akifanya, kwa maana lolote afanyalo Baba, Mwana pia hufanya vivyo hivyo. 20 Baba ampenda Mwana na kumwonyesha yale ambayo yeye Baba mwenyewe anayafanya, naye atamwonyesha kazi kuu kuliko hizi ili mpate kushangaa. 21 Hakika kama vile Baba awafufuavyo wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo Mwana huwapa uzima wale anaopenda. 22 Wala Baba hamhukumu mtu yeyote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23 ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Yeyote asiyemheshimu Mwana, hamheshimu Baba aliyemtuma.

  15. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  16. 21 Ninyi mliitwa kwa ajili ya haya, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.

    22 “Yeye hakutenda dhambi,

    wala hila haikuonekana kinywani mwake.”

    23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa. 25 Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.

  17. 32 Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. 33 Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. 34 Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani.

  18. 5 Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”

    6 Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao, 7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

    8 Mara moja Yesu akatambua rohoni mwake kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu? 9 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue mkeka wako, uende’? 10 Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza, 11 “Nakuambia, inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama, akachukua mkeka wake, akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”

  19. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata, 28 nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. 29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake. 30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”

    31 Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo, 32 lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?”

    33 Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.”

  20. 2 Alikua mbele yake kama mche mwororo

    na kama mzizi katika nchi kavu.

    Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake,

    hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani.

    3 Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu,

    mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso.

    Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

    alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu.

    4 Hakika alichukua udhaifu wetu

    na akajitwika huzuni zetu,

    hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

    akapigwa sana naye, na kuteswa.

    5 Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu,

    alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu;

    adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake,

    na kwa majeraha yake sisi tumepona.

    6 Sisi sote, kama kondoo, tumepotea,

    kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe,

    naye Bwana aliweka juu yake

    maovu yetu sisi sote.

    7 Alionewa na kuteswa,

    hata hivyo hakufungua kinywa chake;

    aliongozwa kama mwana-kondoo

    apelekwaye machinjoni,

    kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya,

    hivyo hakufungua kinywa chake.

    8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa.

    Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake?

    Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai,

    alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu.

  21. 18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

    20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”

    22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”

  22. 25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

    28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  23. 30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Maria, umepata kibali kwa Mungu. 31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Yesu. 32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. 33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

    34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

    35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu.

  24. 13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize. 14 Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

    15 Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

    16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake. 17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

  25. 40 Jua lilipokuwa linatua, watu wakamletea Yesu watu wote waliokuwa na maradhi mbalimbali, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, naye akawaponya. 41 Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele, wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ndiye Kristo.

  26. 9 Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

    10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha na mkono wake ukaponywa kabisa.

  27. 22 Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. 23 Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”

    24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”

    25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. 26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.

  28. 8 Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utiifu kutokana na mateso aliyoyapata, 9 na akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii. 10 Naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

  29. 25 Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

  30. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”

  31. 25 Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”

    27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”

  32. 15 Yeye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwake yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa: vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, viwe ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala; vitu vyote viliumbwa na yeye na kwa ajili yake. 17 Yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote, na katika yeye vitu vyote vinashikamana pamoja. 18 Yeye ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa, naye ndiye mwanzo na mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu, ili yeye awe mkuu katika vitu vyote.

  33. 13 na katikati ya vile vinara vya taa, alikuwamo mtu kama Mwana wa Adamu, akiwa amevaa joho refu, na mkanda wa dhahabu ukiwa umefungwa kifuani mwake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu, nyeupe kama theluji, nayo macho yake yalikuwa kama mwali wa moto. 15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba inayongʼaa, katika tanuru ya moto, nayo sauti yake ilikuwa kama mugurumo ya maji mengi. 16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua likingʼaa kwa nguvu zake zote.

    17 Nilipomwona, nilianguka miguuni pake kama aliyekufa. Ndipo akauweka mkono wake wa kuume juu yangu na kusema: “Usiogope, Mimi ndiye wa Kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ni Yeye Aliye Hai, niliyekuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele! Nami ninazo funguo za mauti na kuzimu.

  34. 1 Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,

    kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.

    2 Roho wa Bwana atakaa juu yake,

    Roho wa hekima na wa ufahamu,

    Roho wa shauri na wa uweza,

    Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana

    3 naye atafurahia kumcha Bwana.

    Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,

    wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,

    4 bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji,

    kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.

    Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,

    kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

    5 Haki itakuwa mkanda wake

    na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.

  35. 21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

    24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

  36. 6 Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa,

    tumepewa mtoto mwanaume,

    nao utawala utakuwa mabegani mwake.

    Naye ataitwa

    Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu,

    Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.

    7 Kuongezeka kwa utawala wake na amani

    hakutakuwa na mwisho.

    Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi

    na juu ya ufalme wake,

    akiuthibitisha na kuutegemeza

    kwa haki na kwa adili,

    tangu wakati huo na hata milele.

    Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote

    utatimiza haya.

  37. 28 Kisha Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua juu Mwana wa Adamu, ndipo mtakapojua kuwa, ‘Mimi ndiye yule niliyesema na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu bali ninasema yale tu ambayo Baba yangu amenifundisha. 29 Yeye aliyenituma yu pamoja nami, hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.’ ”

  38. 9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka.

  39. 13 Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”

    14 Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yohana Mbatizaji; wengine husema ni Eliya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”

    15 Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

    16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”

    17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni.

  40. 17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:

    18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

    kwa sababu amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwatangazia wafungwa

    kufunguliwa kwao,

    na vipofu kupata kuona tena,

    kuwaweka huru wanaoonewa,

    19 na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika.”

    20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. 21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo Andiko hili limetimia mkiwa mnasikia.”

  41. 21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai. 23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. 24 Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. 25 Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti.

  42. 17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

  43. 5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, 6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”

    7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”

    8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 9 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”

    10 Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”

    13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.

  44. 62 Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 63 Lakini Yesu akakaa kimya.

    Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”

    64 Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

    65 Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru. 66 Uamuzi wenu ni gani?”

    Wakajibu, “Anastahili kufa.”

    67 Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi 68 na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

  45. 21 Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka. 22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua, nayo sauti kutoka mbinguni ikasema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa; nami nimependezwa nawe sana.”

    23 Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu,

    Yosefu alikuwa mwana wa Eli,

  46. 41 Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba 42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” 43 Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. 44 Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.

  47. 4 Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:

    5 “Mwambieni Binti Sayuni,

    ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,

    ni mnyenyekevu, naye amepanda punda,

    juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”

    6 Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza. 7 Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake. 8 Umati mkubwa wa watu ukatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti, wakayatandaza barabarani. 9 Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema,

    “Hosana, Mwana wa Daudi!”

    “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

    “Hosana juu mbinguni!”

  48. 39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

    40 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”

    42 Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

    43 Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44 Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.

    45 Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 46 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”

  49. 13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14 Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.

    15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.

  50. 3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? 4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.

    5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake. 6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi. 7 Kwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

    8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye. 9 Kwa maana tunajua kwamba Kristo, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake. 10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.

  51. 23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. 24 Ghafula, kukainuka dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. 25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

    26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.

    27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

  52. 54 Yesu akawajibu, “Kama nikijitukuza utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi. 55 Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake. 56 Baba yenu Abrahamu alishangilia kwamba angaliiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.”

    57 Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, wewe wasema umemwona Abrahamu?”

    58 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Abrahamu hajakuwako, ‘Mimi niko.’ ” 59 Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Yesu akajificha, naye akatoka Hekaluni.

  53. 24 Lakini Tomaso, aliyeitwa Didimasi, yaani Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Yesu alipokuja. 25 Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.”

    Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”

    26 Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Yesu akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”

    28 Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”

    29 Yesu akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”

  54. 10 Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana

    kumchubua na kumsababisha ateseke.

    Ingawa Bwana amefanya maisha yake

    kuwa sadaka ya hatia,

    ataona uzao wake na kuishi siku nyingi,

    nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake.

    11 Baada ya maumivu ya nafsi yake,

    ataona nuru ya uzima na kuridhika;

    kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki

    atawafanya wengi kuwa wenye haki,

    naye atayachukua maovu yao.

    12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu,

    naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu,

    kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti,

    naye alihesabiwa pamoja na wakosaji.

    Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi,

    na kuwaombea wakosaji.

  55. 48 Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho. 49 Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema. 50 Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”

  56. 33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

    35 Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.”

    36 Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, 37 na wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

  57. 11 Huyu ndiye

    “ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,

    ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’

    12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

  58. 41 Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza, 42 “Mnaonaje kuhusu Kristo? Yeye ni mwana wa nani?”

    Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”

    43 Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,

    44 “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:

    “Keti mkono wangu wa kuume,

    hadi nitakapowaweka adui zako

    chini ya miguu yako.” ’

    45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” 46 Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali.

  59. 8 Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. 9 Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”

    13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,

    14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,

    na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

  60. 38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”

    39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. 41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”

  61. 6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”

    7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

    9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.

    10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”

  62. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi.

  63. 1 Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:

  64. 2 Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

    4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

  65. 10 Yesu alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake. 11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

    12 Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

  66. 14 Huko Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ngʼombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. 15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu, pamoja na kondoo na ngʼombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. 16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”

    17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”

    18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?”

    19 Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”

    20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” 21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema.

  67. 36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”

  68. 1 “Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,

    mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye;

    nitaweka Roho yangu juu yake,

    naye ataleta haki kwa mataifa.

    2 Hatapaza sauti wala kupiga kelele,

    wala hataiinua sauti yake barabarani.

    3 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,

    na utambi unaofuka moshi hatauzima.

    Kwa uaminifu ataleta haki,

    4 hatazimia roho wala kukata tamaa,

    mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia.

    Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”

  69. 5 Bwana asema, “Siku zinakuja,

    nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,

    Mfalme atakayetawala kwa hekima,

    na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.

    6 Katika siku zake, Yuda ataokolewa

    na Israeli ataishi salama.

    Hili ndilo jina atakaloitwa:

    Bwana Haki Yetu.

  70. 23 Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, 24 naye akapiga kelele akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!”

    25 Lakini Yesu akamkemea, akamwambia, “Nyamaza kimya! Nawe umtoke!” 26 Yule pepo mchafu akamtikisatikisa huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa.

    27 Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!”

  71. 23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke. 24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”

    25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula? 26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.”

    27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato. 28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

  72. 37 Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini, 38 lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.”

  73. 3 Yesu akijua ya kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 hivyo aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.

  74. 12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi, akawauliza, “Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana,’ hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri yenu ninyi kama mkiyatenda.

  75. 13 Mungu wa Abrahamu na Isaki na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake. 14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule muuaji. 15 Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya.

  76. 12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

    15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

  77. 11 Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. 12 Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. 13 Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, 14 kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa.

  78. 14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli. 15 Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema. 16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa.

  79. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo.

  80. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

  81. 53 Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. 54 Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?” 55 “Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Maria, nao ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” 57 Wakachukizwa naye.

    Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”

    58 Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

  82. 33 Wakamwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”

    34 Yesu akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati yuko pamoja nao? 35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.”

  83. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  84. 6 Lakini kuna mahali mtu fulani ameshuhudia akisema:

    “Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,

    binadamu ni nani hata unamjali?

    7 Umemfanya chini kidogo kuliko malaika;

    ukamvika taji ya utukufu na heshima,

    8 nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.”

    Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake. 9 Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji ya utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwamba kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.

  85. 1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni, 2 yeye ahudumuye katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si na mwanadamu.

    3 Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa. 4 Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria. 5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Mose alionywa alipokaribia kujenga hema, akiambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano ulioonyeshwa kule mlimani.” 6 Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora zaidi kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani, nalo limewekwa misingi wa ahadi zilizo bora zaidi.