82 Bible Verses About Light

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Light
  1. 1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.

    3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.

    6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7 Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. 8 Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. 9 Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.

    10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

    14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.

  2. 13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

    14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

  3. 8 Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, lakini sasa ninyi ni nuru katika Bwana. Enendeni kama watoto wa nuru 9 (kwa kuwa tunda la nuru hupatikana katika wema wote, haki na kweli), 10 nanyi tafuteni yale yanayompendeza Bwana. 11 Msishiriki matendo ya giza yasiyofaa, bali yafichueni. 12 Kwa maana ni aibu hata kutaja mambo yale ambayo wasiotii wanayafanya sirini. 13 Lakini kila kitu kilichowekwa nuruni, huonekana, 14 kwa kuwa nuru ndiyo hufanya kila kitu kionekane. Hii ndiyo sababu imesemekana:

    “Amka, wewe uliyelala,

    ufufuke kutoka kwa wafu,

    naye Kristo atakuangazia.”

  4. 5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

    8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  5. 12 Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

  6. 1 Hapo mwanzo Mungu aliumba mbingu na dunia. 2 Wakati huu dunia ilikuwa haina umbo, tena ilikuwa tupu. Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji, naye Roho wa Mungu alikuwa ametulia juu ya maji.

    3 Mungu akasema, “Iwepo nuru,” nayo nuru ikawepo. 4 Mungu akaona ya kuwa nuru ni njema, ndipo Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru “mchana,” na giza akaliita “usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya kwanza.

  7. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”

  8. 105 Neno lako ni taa ya miguu yangu

    na mwanga katika njia yangu.

  9. 3 Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. 4 Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu. 5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ingʼae gizani,” ameifanya nuru yake ingʼae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.

    7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu.

  10. 14 Fanyeni mambo yote bila kunungʼunika wala kushindana, 15 ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnangʼaa kama mianga ulimwenguni. 16 Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure.

  11. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

  12. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

    2 Waovu watakaposogea dhidi yangu

    ili wanile nyama yangu,

    adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

    watajikwaa na kuanguka.

  13. 35 Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda. 36 Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.

    37 Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini.

  14. 19 Jua halitakuwa tena nuru yako mchana,

    wala mwangaza wa mwezi hautakuangazia,

    kwa maana Bwana atakuwa nuru yako ya milele,

    naye Mungu wako atakuwa utukufu wako.

    20 Jua lako halitazama tena,

    nao mwezi wako hautafifia tena;

    Bwana atakuwa nuru yako milele,

    nazo siku zako za huzuni zitakoma.

  15. 1 “Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja

    na utukufu wa Bwana umezuka juu yako.

    2 Tazama, giza litaifunika dunia

    na giza kuu litayafunika mataifa,

    lakini Bwana atazuka juu yako

    na utukufu wake utaonekana juu yako.

    3 Mataifa watakuja kwenye nuru yako

    na wafalme kwa mwanga wa mapambazuko yako.

    4 “Inua macho yako na utazame pande zote:

    Wote wanakusanyika na kukujia,

    wana wako wanakuja toka mbali,

    nao binti zako wanabebwa mikononi.

    5 Ndipo utatazama na kutiwa nuru,

    moyo wako utasisimka na kujaa furaha,

    mali zilizo baharini zitaletwa kwako,

    utajiri wa mataifa utakujilia.

  16. 11 Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia zaidi kuliko hapo kwanza tulipoamini. 12 Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru. 13 Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. 14 Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.

  17. 17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.

  18. 1 Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia, 2 kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku. 3 Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

    4 Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi. 5 Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. 6 Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi.

  19. 44 Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma. 45 Yeyote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma. 46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani.

  20. 126 Ee Bwana, wakati wako wa kutenda umewadia,

    kwa kuwa sheria yako inavunjwa.

    127 Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu,

    naam, zaidi ya dhahabu safi,

    128 na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili,

    nachukia kila njia potovu.

    129 Sheria zako ni za ajabu,

    hivyo ninazitii.

    130 Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru,

    kunampa mjinga ufahamu.

  21. 15 “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,

    kwenye njia ya kuelekea baharini,

    ngʼambo ya Yordani,

    Galilaya ya watu wa Mataifa:

    16 watu wale waliokaa gizani

    wameona nuru kuu;

    nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti,

    nuru imewazukia.”

  22. 2 Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukangʼaa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho.

  23. 23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake. 24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake. 25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo.

  24. 28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:

    29 “Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,

    sasa wamruhusu mtumishi wako

    aende zake kwa amani.

    30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,

    31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,

    32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa

    na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”

  25. 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.

  26. 7 Upendo wako usiokoma

    ni wa thamani mno!

    Watu wakuu na wadogo

    hujificha uvulini wa mbawa zako.

    8 Wanajifurahisha katika wingi nyumbani mwako,

    nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.

    9 Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,

    katika nuru yako twaona nuru.

  27. 8 Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

    na uponyaji wako utatokea upesi;

    ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

    na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako.

    9 Ndipo utaita, naye Bwana atajibu,

    utalia kuomba msaada,

    naye atasema: Mimi hapa.

    “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu,

    na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

    10 nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

    na kutosheleza mahitaji ya walioonewa,

    ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani,

    nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

  28. 35 Yohana alikuwa taa iliyowaka na kutoa nuru, nanyi kwa muda mlichagua kuifurahia nuru yake.

  29. 47 Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru:

    “ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa,

    ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”

  30. 9 Yeyote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani. 10 Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu chochote ndani yake cha kumkwaza.

  31. 14 Mungu akasema, “Iwepo mianga kwenye nafasi ya anga ili itenganishe usiku na mchana, nayo iwe alama ya kutambulisha majira mbalimbali, siku na miaka, 15 nayo iwe mianga kwenye nafasi ya anga ya kutia nuru juu ya dunia.” Ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa: mwanga mkubwa utawale mchana, na mwanga mdogo utawale usiku. Pia Mungu akafanya nyota. 17 Mungu akaiweka katika nafasi ya anga iangaze dunia, 18 itawale usiku na mchana, na ikatenganishe nuru na giza. Mungu akaona kuwa hili ni jema. 19 Ikawa jioni, ikawa asubuhi, siku ya nne.

  32. 11 Nuru huangaza wenye haki

    na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.

  33. 13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, 15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe: yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, 16 yeye peke yake ambaye hapatikani na mauti, na anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

  34. 18 Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko,

    ambayo hungʼaa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu.

    19 Lakini njia ya waovu ni kama giza nene;

    hawajui kinachowafanya wajikwae.

  35. 3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

    5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

    Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.

  36. 3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia, 4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao. 5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

  37. 5 Wakati niko ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu.”

  38. 6 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki;

    nitakushika mkono wako.

    Nitakulinda na kukufanya

    kuwa Agano kwa ajili ya watu

    na nuru kwa Mataifa,

    7 kuwafungua macho wale wasioona,

    kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela,

    na kuwafungua kutoka gerezani

    wale wanaokaa gizani.

  39. 33 “Hakuna mtu yeyote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru. 34 Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote pia umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote pia umejaa giza. 35 Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyoko ndani yako isiwe giza. 36 Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yoyote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”

  40. 8 “Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru.

  41. 23 Kwa maana amri hizi ni taa,

    mafundisho haya ni mwanga

    na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,

  42. 22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!

    24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

  43. 4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu,

    yule mwenye rehema, huruma na haki.

  44. 19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inavyongʼaa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi izuke mioyoni mwenu.

  45. 13 “Wako wale wanaoiasi nuru,

    wasiofahamu njia zake

    wala hawakai katika mapito yake.

    14 Wakati mwanga wa mchana unapotoweka, muuaji huinuka

    naye huwaua maskini na mhitaji;

    wakati wa usiku hunyemelea kama mwizi.

    15 Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza,

    naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’

    naye huuficha uso wake.

    16 Katika giza, huvunja majumba,

    lakini wakati wa mchana hujifungia ndani;

    hawataki kufanya lolote nuruni.

    17 Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao;

    hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.

  46. 16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha. 17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwenye nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

  47. 3 Mungu wa Israeli alinena,

    mwamba wa Israeli akaniambia:

    ‘Mtu anatawala watu kwa haki,

    wakati anapotawala

    akiwa na hofu ya Mungu,

    4 yeye ni kama mwanga wa asubuhi jua lichomozapo

    asubuhi isiyo na mawingu,

    kama mwanga baada ya mvua

    uchipuzao majani kutoka ardhini.’

  48. 2 Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi,

    amezitandaza mbingu kama hema

  49. 14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? 15 Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini?

  50. 6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye

    kutuonyesha jema lolote?”

    Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako.

  51. 6 yeye asema:

    “Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu

    ili kurejeza makabila ya Yakobo,

    na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi?

    Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa,

    ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

  52. 23 Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.

  53. 14 Aliwaongoza kwa wingu mchana

    na kwa nuru kutoka kwenye moto usiku kucha.

  54. 30 Tazama jinsi anavyotandaza umeme wa radi kumzunguka,

    naye huvifunika vilindi vya bahari.

    31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa,

    na kuwapa chakula kwa wingi.

    32 Huujaza mkono wake kwa umeme wa radi,

    na kuuagiza kulenga shabaha yake.

  55. 28 Wewe, Ee Bwana, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka;

    Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga.

  56. 7 Nuru ni tamu,

    tena inafurahisha macho kuona jua.

  57. 1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza,

    kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia,

    mpaka haki yake itakapoangaza kama mapambazuko,

    wokovu wake kama mwanga wa moto.

  58. 4 Mngʼao wake ulikuwa kama jua lichomozalo;

    mionzi ilimulika kutoka mkononi mwake,

    ambako nguvu zake zilifichwa.

  59. 2 Bali kwenu ninyi mnaoliheshimu Jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mabawa yake. Nanyi mtatoka nje na kurukaruka kama ndama aliyeachiwa kutoka zizini.

  60. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

  61. 20 ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha.

  62. 7 Sheria ya Bwana ni kamilifu,

    ikihuisha nafsi.

    Shuhuda za Bwana ni za kuaminika,

    zikimpa mjinga hekima.

    8 Maagizo ya Bwana ni kamili,

    nayo hufurahisha moyo.

    Amri za Bwana huangaza,

    zatia nuru machoni.

    9 Kumcha Bwana ni utakatifu,

    nako kwadumu milele.

    Amri za Bwana ni za hakika,

    nazo zina haki.

    10 Ni za thamani kuliko dhahabu,

    kuliko dhahabu iliyo safi sana,

    ni tamu kuliko asali,

    kuliko asali kutoka kwenye sega.

  63. 11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao,

    Bwana hutoa wema na heshima;

    hakuna kitu chema anachowanyima

    wale ambao hawana hatia.

  64. 9 Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana,

    bali taa ya mwovu itazimwa.

  65. 13 Nikaona kuwa hekima ni bora kuliko upumbavu,

    kama vile nuru ilivyo bora kuliko giza.

  66. 20 Ole wao wanaoita ubaya ni wema,

    na wema ni ubaya,

    wawekao giza badala ya nuru,

    na nuru badala ya giza,

    wawekao uchungu badala ya utamu,

    na utamu badala ya uchungu.

  67. 3 Wale wenye hekima watangʼaa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watangʼaa kama nyota milele na milele.

  68. 15 Watu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unangʼaa kama uso wa malaika.

  69. 21 Wakati wa mchana Bwana aliwatangulia kwa nguzo ya wingu kuwaongoza katika njia yao, na wakati wa usiku aliwatangulia kwa nguzo ya moto kuwaangazia, ili waweze kusafiri mchana au usiku. 22 Ile nguzo ya wingu wakati wa mchana au ile nguzo ya moto wakati wa usiku haikuondoka mahali pake mbele ya watu.

  70. 18 Akipiga chafya mwanga humetameta;

    macho yake ni kama mionzi ya mapambazuko.

    19 Mienge iwakayo humiminika kutoka kinywani mwake;

    cheche za moto huruka nje.

    20 Moshi hufuka kutoka puani mwake,

    kama kutoka kwenye chungu kinachotokota kwa moto wa matete.

    21 Pumzi yake huwasha makaa ya mawe,

    nayo miali ya moto huruka kutoka kinywani mwake.

  71. 10 Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi na bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na mwanga wa taa.

  72. 3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.

  73. 4 Yanipasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma wakati bado ni mchana, kwa kuwa usiku waja ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi.

  74. 9 Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”

  75. 7 Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

  76. 3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni. 4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.

  77. 16 Katika mkono wake wa kuume alishika nyota saba, na kinywani mwake ulitoka upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa kama jua likingʼaa kwa nguvu zake zote.

  78. 29 Mose alipoteremka kutoka Mlima Sinai akiwa na vile vibao viwili vya Ushuhuda mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa ukingʼaa, kwa sababu alikuwa amezungumza na Bwana. 30 Aroni na Waisraeli wote walipomwona Mose, kuwa uso wake unangʼaa, waliogopa kumkaribia.

  79. 26 Lakini nilipotazamia mema, mabaya yalinijia;

    nilipotafuta nuru, ndipo giza lilipokuja.

  80. 5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,

    nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.

  81. 17 Nuru ya Israeli itakuwa moto,

    Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto;

    katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba

    na michongoma yake.

  82. 5 Kwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.