108 Bible Verses About Praising God

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Praising God
  1. 1 Msifuni Bwana.

    Msifuni Mungu katika patakatifu pake,

    msifuni katika mbingu zake kuu.

    2 Msifuni kwa matendo yake makuu,

    msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.

    3 Msifuni kwa mvumo wa tarumbeta,

    msifuni kwa kinubi na zeze,

    4 msifuni kwa matari na kucheza,

    msifuni kwa kinanda cha nyuzi na filimbi,

    5 msifuni kwa matoazi yaliayo,

    msifuni kwa matoazi yavumayo sana.

    6 Kila chenye pumzi na kimsifu Bwana.

    Msifuni Bwana!

  2. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

    Vyote vilivyomo ndani yangu

    vilihimidi jina lake takatifu.

    2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,

    wala usisahau wema wake wote,

    3 akusamehe dhambi zako zote,

    akuponya magonjwa yako yote,

    4 aukomboa uhai wako na kaburi,

    akuvika taji ya upendo na huruma,

    5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema,

    ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.

  3. 15 Basi kwa njia ya Yesu, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

  4. Zaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka.

    1 Nitamtukuza Bwana nyakati zote,

    sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote.

    2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,

    walioonewa watasikia na wafurahi.

    3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami,

    naam, na tulitukuze jina lake pamoja.

    4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,

    akaniokoa kwenye hofu zangu zote.

  5. 6 Pia mbele ya kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama bilauri.

    Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wakiwa wamejawa na macho mbele na nyuma. 7 Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ngʼombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka. 8 Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:

    “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

    ni Bwana Mungu Mwenyezi,

    aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.”

    9 Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aketiye kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele, 10 wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aketiye kwenye kiti cha enzi na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:

    11 “Bwana wetu na Mungu wetu,

    wewe unastahili kupokea utukufu

    na heshima na uweza,

    kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,

    na kwa mapenzi yako viliumbwa

    na vimekuwako.”

  6. 6 Bwana asifiwe,

    kwa maana amesikia kilio changu

    nikimwomba anihurumie.

    7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu,

    moyo wangu umemtumaini yeye,

    nami nimesaidiwa.

    Moyo wangu unarukaruka kwa furaha

    nami nitamshukuru kwa wimbo.

  7. 3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai,

    midomo yangu itakuadhimisha.

    4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu,

    na kwa jina lako nitainua mikono yangu.

    5 Nafsi yangu itatoshelezwa

    kama kwa wingi wa vyakula;

    kwa midomo iimbayo

    kinywa changu kitakusifu wewe.

    6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe,

    ninawaza juu yako makesha yote ya usiku.

  8. Zaburi ya shukrani.

    1 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote.

    2 Mwabuduni Bwana kwa furaha;

    njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe.

    3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu.

    Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake;

    sisi tu watu wake,

    kondoo wa malisho yake.

    4 Ingieni malangoni mwake kwa shukrani

    na katika nyua zake kwa kusifu,

    mshukuruni yeye na kulisifu jina lake.

    5 Kwa maana Bwana ni mwema

    na upendo wake wadumu milele;

    uaminifu wake unadumu kwa vizazi vyote.

  9. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa.

  10. 18 Pia msilewe kwa mvinyo, ambamo ndani yake mna upotovu, bali mjazwe Roho. 19 Msemezane ninyi kwa ninyi kwa zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, 20 siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

    21 Nyenyekeaneni ninyi kwa ninyi kwa heshima kwa ajili ya Kristo.

  11. 1 Msifuni Bwana.

    Msifuni Bwana kutoka mbinguni,

    msifuni juu vileleni.

    2 Msifuni, enyi malaika wake wote,

    msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni.

    3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi,

    msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo.

    4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana,

    na ninyi maji juu ya anga.

    5 Vilisifu jina la Bwana

    kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa.

  12. 22 Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko. 23 Baada ya kuwachapa sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. 24 Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

    25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.

  13. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  14. 1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya;

    mwimbieni Bwana dunia yote.

    2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake;

    tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.

    3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,

    matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.

    4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;

    yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.

    5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,

    lakini Bwana aliziumba mbingu.

    6 Fahari na enzi viko mbele yake;

    nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.

    7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa,

    mpeni Bwana utukufu na nguvu.

    8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;

    leteni sadaka na mje katika nyua zake.

    9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake;

    dunia yote na itetemeke mbele zake.

  15. 1 Msifuni Bwana.

    Lisifuni jina la Bwana,

    msifuni, enyi watumishi wa Bwana,

    2 ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Bwana,

    katika nyua za nyumba ya Mungu wetu.

    3 Msifuni Bwana, kwa kuwa Bwana ni mwema,

    liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza.

    4 Kwa maana Bwana amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe,

    Israeli kuwa mali yake ya thamani.

  16. 3 Wakasema tena kwa nguvu:

    “Haleluya!

    Moshi wake huyo kahaba unapanda juu

    milele na milele.”

    4 Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu:

    “Amen, Haleluya!”

    5 Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema:

    “Msifuni Mungu wetu,

    ninyi watumishi wake wote,

    ninyi nyote mnaomcha,

    wadogo kwa wakubwa!”

    6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema:

    “Haleluya!

    Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.

    7 Tufurahi, tushangilie

    na kumpa utukufu!

    Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia

    na bibi arusi wake amejiweka tayari.

  17. 33 Kisha miti ya msituni itaimba,

    itaimba kwa furaha mbele za Bwana,

    kwa maana anakuja kuihukumu dunia.

    34 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

    35 Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe.

    Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa,

    ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,

    na kushangilia katika sifa zako.”

    36 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,

    tangu milele na hata milele.

    Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni Bwana.”

  18. 5 Nao Walawi Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabnea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakasema: “Simameni mkamsifu Bwana Mungu wenu, yeye ambaye ni Mungu tangu milele hata milele.

    “Libarikiwe jina lake tukufu, litukuzwe juu ya baraka zote na sifa. 6 Wewe peke yako ndiwe Bwana. Uliziumba mbingu, hata mbingu za mbingu na jeshi lote la mbinguni, dunia na vyote vilivyo ndani yake, na pia bahari na vyote vilivyomo ndani yake. Huvipa vitu vyote uhai, nalo jeshi la mbinguni linakuabudu wewe.

    7 “Wewe ni Bwana Mungu uliyemchagua Abramu na kumtoa kutoka Uru ya Wakaldayo, nawe ukamwita Abrahamu. 8 Uliona kuwa moyo wake ni mwaminifu kwako, nawe ukafanya Agano naye kuwapa wazao wake nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi. Umetimiza ahadi yako kwa sababu wewe ni mwenye haki.

  19. 1 Mwimbieni Bwana kwa furaha, enyi wenye haki;

    kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.

    2 Msifuni Bwana kwa kinubi,

    mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.

    3 Mwimbieni wimbo mpya;

    pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.

    4 Maana neno la Bwana ni haki na kweli,

    ni mwaminifu kwa yote atendayo.

    5 Bwana hupenda uadilifu na haki;

    dunia imejaa upendo wake usiokoma.

  20. 1 Msifuni Bwana.

    Enyi watumishi wa Bwana msifuni,

    lisifuni jina la Bwana.

    2 Jina la Bwana na lisifiwe,

    sasa na hata milele.

    3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake,

    jina la Bwana linapaswa kusifiwa.

  21. Wimbo wa Sifa. Wa Daudi.

    1 Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,

    nitalisifu jina lako milele na milele.

    2 Kila siku nitakusifu

    na kulitukuza jina lako milele na milele.

    3 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

    ukuu wake haupimiki.

    4 Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,

    watasimulia matendo yako makuu.

  22. 15 Ee Bwana, fungua midomo yangu,

    na kinywa changu kitatangaza sifa zako.

  23. 1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

    Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana,

    umejivika utukufu na enzi.

  24. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”

    13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,

    14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni,

    na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

  25. 30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,

    nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.

    31 Hili litampendeza Bwana kuliko ngʼombe dume,

    zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.

  26. 33 Nitamwimbia Bwana maisha yangu yote;

    nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.

    34 Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye,

    ninapofurahi katika Bwana.

    35 Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia

    na waovu wasiwepo tena.

    Ee nafsi yangu, msifu Bwana.

    Msifuni Bwana.

  27. 1 Ee Bwana, wewe ni Mungu wangu,

    nitakutukuza na kulisifu jina lako,

    kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu

    umetenda mambo ya ajabu,

    mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.

  28. 1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha;

    tumfanyie kelele za shangwe

    Mwamba wa wokovu wetu.

    2 Tuje mbele zake kwa shukrani,

    tumtukuze kwa vinanda na nyimbo.

    3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu,

    mfalme mkuu juu ya miungu yote.

    4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia,

    na vilele vya milima ni mali yake.

    5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya,

    na mikono yake iliumba nchi kavu.

    6 Njooni, tusujudu, tumwabudu,

    tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu,

    7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu,

    na sisi ni watu wa malisho yake,

    kondoo chini ya utunzaji wake.

    Kama mkiisikia sauti yake leo,

  29. 9 Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

    “Wewe unastahili kukitwaa kitabu

    na kuzivunja lakiri zake,

    kwa sababu ulichinjwa

    na kwa damu yako ukamnunulia Mungu watu

    kutoka kila kabila, kila lugha,

    kila jamaa na kila taifa.

    10 Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani

    wa kumtumikia Mungu wetu,

    nao watatawala duniani.”

    11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. 12 Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:

    “Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,

    kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu

    na heshima na utukufu na sifa!”

    13 Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi na baharini na vyote vilivyomo ndani yake vikiimba:

    “Sifa na heshima na utukufu na uweza

    ni vyake yeye aketiye juu ya hicho kiti cha enzi

    na kwa Mwana-Kondoo,

    milele na milele!”

    14 Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee ishirini na wanne wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

  30. Utenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi.

    1 Nitakutukuza wewe, Ee Bwana,

    kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,

    na hukuacha adui zangu

    washangilie juu yangu.

    2 Ee Bwana, Mungu wangu, nilikuita unisaidie

    na wewe umeniponya.

    3 Ee Bwana, umenitoa Kuzimu,

    umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.

    4 Mwimbieni Bwana, enyi watakatifu wake;

    lisifuni jina lake takatifu.

    5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,

    bali upendo wake hudumu siku zote.

    Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,

    lakini asubuhi kukawa na furaha.

  31. 5 Kwa kuwa umekuwa tumaini langu, Ee Bwana Mwenyezi,

    tegemeo langu tangu ujana wangu.

    6 Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe,

    ulinitoa tumboni mwa mama yangu.

    Nitakusifu wewe daima.

    7 Nimekuwa kama kioja kwa wengi,

    lakini wewe ni kimbilio langu imara.

    8 Kinywa changu kimejazwa sifa zako,

    nikitangaza utukufu wako mchana kutwa.

  32. 8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe,

    hakuna matendo ya kulinganishwa na yako.

    9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya

    yatakuja na kuabudu mbele zako;

    wataliletea utukufu jina lako.

    10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu;

    wewe peke yako ndiwe Mungu.

    11 Ee Bwana, nifundishe njia yako,

    nami nitakwenda katika kweli yako;

    nipe moyo usiositasita,

    ili niweze kulicha jina lako.

    12 Ee Bwana wangu, nitakusifu kwa moyo wote;

    nitaliadhimisha jina lako milele.

    13 Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu;

    umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi.

  33. 1 Msifuni Bwana.

    Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote,

    katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.

    2 Kazi za Bwana ni kuu,

    wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.

    3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu,

    haki yake hudumu daima.

    4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe,

    Bwana ni mwenye neema na huruma.

    5 Huwapa chakula wale wanaomcha,

    hulikumbuka agano lake milele.

  34. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

  35. 1 Msifuni Bwana.

    Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

    2 Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Bwana

    au kutangaza kikamilifu sifa zake?

  36. 8 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma,

    na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu,

    9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu,

    na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema.

  37. 10 Mwimbieni Bwana wimbo mpya,

    sifa zake toka miisho ya dunia,

    ninyi mshukao chini baharini,

    na vyote vilivyomo ndani yake,

    enyi visiwa na wote wakaao ndani yake.

    11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;

    makao anamoishi Kedari na yashangilie.

    Watu wa Sela waimbe kwa furaha,

    na wapige kelele kutoka vilele vya milima.

    12 Wampe Bwana utukufu,

    na kutangaza sifa zake katika visiwa.

  38. 68 “Ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli,

    kwa kuwa amewajilia watu wake na kuwakomboa.

    69 Naye ametusimamishia pembe ya wokovu

    katika nyumba ya Daudi mtumishi wake,

  39. 9 Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema:

    “Wokovu una Mungu wetu,

    yeye aketiye kwenye kiti cha enzi,

    na Mwana-Kondoo!”

    11 Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, 12 wakisema:

    “Amen!

    Sifa na utukufu

    na hekima na shukrani na heshima

    na uweza na nguvu

    viwe kwa Mungu wetu milele na milele.

    Amen!”

  40. Zaburi ya Daudi.

    1 Mpeni Bwana, enyi mashujaa,

    mpeni Bwana utukufu na nguvu.

    2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;

    mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.

  41. Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi.

    1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!

    2 Imbeni utukufu wa jina lake;

    mpeni sifa zake kwa utukufu!

    3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!

    Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba

    adui wananyenyekea mbele zako.

    4 Dunia yote yakusujudia,

    wanakuimbia wewe sifa,

    wanaliimbia sifa jina lako.”

  42. Zaburi ya Daudi.

    1 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote,

    mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako.

    2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu,

    nami nitalisifu jina lako

    kwa ajili ya upendo wako

    na uaminifu,

    kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako

    juu ya vitu vyote.

  43. 1 Msifuni Bwana.

    Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa,

    jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye!

  44. 37 Alipokaribia mahali yanapoanzia materemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:

    38 “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa Jina la Bwana!”

    “Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.”

  45. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

    1 Nilimngoja Bwana kwa saburi,

    naye akaniinamia, akasikia kilio changu.

    2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu,

    kutoka matope na utelezi;

    akaiweka miguu yangu juu ya mwamba

    na kunipa mahali imara pa kusimama.

    3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,

    wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.

    Wengi wataona na kuogopa

    na kuweka tumaini lao kwa Bwana.

  46. 4 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote,

    ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda;

    5 mwimbieni Bwana kwa kinubi,

    kwa kinubi na sauti za kuimba,

    6 kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume:

    shangilieni kwa furaha mbele za Bwana, aliye Mfalme.

  47. 3 Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:

    “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu

    ni Bwana Mwenye Nguvu Zote;

    dunia yote imejaa utukufu wake.”

  48. 19 Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni, 20 na akasema:

    “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele;

    hekima na uweza ni vyake.

    21 Yeye hubadili nyakati na majira;

    huwaweka wafalme na kuwaondoa.

    Huwapa hekima wenye hekima,

    na maarifa wenye ufahamu.

    22 Hufunua siri na mambo yaliyofichika;

    anajua yale yaliyo gizani,

    nayo nuru hukaa kwake.

    23 Ninakushukuru na kukuhimidi,

    Ee Mungu wa baba zangu:

    Umenipa hekima na uwezo,

    umenijulisha kile tulichokuomba,

    umetujulisha ndoto ya mfalme.”

  49. 2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu. 3 Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema:

    “Bwana Mungu Mwenyezi,

    matendo yako ni makuu na ya ajabu.

    Njia zako wewe ni za haki na za kweli,

    Mfalme wa nyakati zote!

    4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana

    na kulitukuza jina lako?

    Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.

    Mataifa yote yatakuja

    na kuabudu mbele zako,

    kwa kuwa matendo yako ya haki

    yamedhihirishwa.”

  50. 9 Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa Bwana. Mfalme Daudi pia akafurahi sana.

    10 Daudi akamhimidi Bwana mbele ya kusanyiko lote, akisema:

    “Uhimidiwe wewe, Ee Bwana,

    Mungu wa Israeli baba yetu,

    tangu milele hata milele.

    11 Ukuu na uweza, ni vyako, Ee Bwana,

    na utukufu na enzi na uzuri,

    kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani

    ni chako wewe.

    Ee Bwana, ufalme ni wako;

    umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote.

    12 Utajiri na heshima vyatoka kwako;

    wewe ndiwe utawalaye vitu vyote.

    Mikononi mwako kuna nguvu na uweza

    ili kuinua na kuwapa wote nguvu,

    13 Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru

    na kulisifu Jina lako tukufu.

  51. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa muth-labeni. Zaburi ya Daudi.

    1 Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote,

    nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.

    2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako.

    Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana.

  52. 13 Ee Bwana, utukuzwe katika nguvu zako,

    tutaimba na kusifu nguvu zako.

  53. 3 Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu;

    wewe ni sifa ya Israeli.

  54. 28 Ulimi wangu utanena haki yako

    na sifa zako mchana kutwa.

  55. 7 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti;

    nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.

    8 Amka, nafsi yangu!

    Amka, kinubi na zeze!

    Nitayaamsha mapambazuko.

    9 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa;

    nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.

    10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni,

    uaminifu wako unazifikia anga.

    11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,

    utukufu wako na uwe duniani pote.

  56. 19 Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni,

    ufalme wake unatawala juu ya vyote.

    20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,

    ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake,

    ninyi mnaotii neno lake.

    21 Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni,

    ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.

    22 Mhimidini Bwana, kazi zake zote

    kila mahali katika milki yake.

    Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

  57. 47 Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe.

    Tukusanye tena kutoka kwa mataifa,

    ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,

    na kushangilia katika sifa zako.

    48 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,

    tangu milele na hata milele.

    Watu wote na waseme, “Amen!”

    Msifuni Bwana.

  58. 23 Mwimbieni Bwana dunia yote;

    tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.

    24 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,

    matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.

    25 Kwa kuwa Bwana ni mkuu,

    mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;

    yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.

    26 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,

    lakini Bwana aliziumba mbingu.

    27 Fahari na enzi viko mbele yake;

    nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.

    28 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa,

    mpeni Bwana utukufu na nguvu,

    29 mpeni Bwana utukufu

    unaostahili jina lake.

    Leteni sadaka na mje katika nyua zake;

    mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.

  59. Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato.

    1 Ni vyema kumshukuru Bwana

    na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,

    2 kuutangaza upendo wako asubuhi,

    na uaminifu wako wakati wa usiku,

    3 kwa zeze yenye nyuzi kumi

    na kwa sauti ya kinubi.

  60. 20 Wanyama wa mwituni wataniheshimu,

    mbweha na bundi,

    kwa sababu ninawapatia maji jangwani,

    na vijito katika nchi kame,

    ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua,

    21 watu wale niliowaumba kwa ajili yangu,

    ili wapate kutangaza sifa zangu.

  61. 10 Ninafurahia sana katika Bwana,

    nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu.

    Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu,

    na kunipamba kwa joho la haki,

    kama vile bwana arusi apambavyo

    kichwa chake kama kuhani,

    na kama bibi arusi ajipambavyo

    kwa vito vyake vya thamani.

    11 Kwa maana kama vile ardhi ifanyavyo chipukizi kuota,

    na bustani isababishavyo mbegu kuota,

    ndivyo Bwana Mwenyezi atafanya haki na sifa

    zichipuke mbele ya mataifa yote.

  62. 11 sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi na bwana arusi, na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba ya Bwana, wakisema,

    “ ‘ “Mshukuruni Bwana Mwenye Nguvu Zote,

    kwa maana Bwana ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.”

    Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama zilivyokuwa hapo awali,’ asema Bwana.

  63. 34 Mwisho wa huo wakati, mimi Nebukadneza, niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele.

    Utawala wake ni utawala wa milele;

    ufalme wake hudumu kutoka kizazi na kizazi.

    35 Mataifa yote ya dunia

    yanahesabiwa kuwa si kitu.

    Hufanya kama atakavyo

    kwa majeshi ya mbinguni,

    na kwa mataifa ya dunia.

    Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake

    au kumwambia, “Umefanya nini wewe?”

    36 Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, nikarudishiwa heshima yangu na fahari yangu kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni. 37 Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, na humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu afanyacho ni haki, na njia zake zote ni adili. Nao waendao kwa kiburi anaweza kuwashusha.

  64. 52 Kisha wakamwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wamejawa na furaha kuu. 53 Nao wakadumu ndani ya Hekalu wakimtukuza Mungu. Amen.

  65. 42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.

  66. 3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kupitia kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka: uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani, hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho.

  67. 24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi: 25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka ni vyake tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

  68. 21 Yeye ni sifa yako; yeye ni Mungu wako, ambaye alikutendea yale maajabu makubwa na ya kutisha uliyoyaona kwa macho yako mwenyewe.

  69. 4 Ninamwita Bwana, anayestahili kusifiwa,

    nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.

  70. 46 Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!

    Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu!

    47 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,

    awatiishaye mataifa chini yangu,

    48 aniokoaye na adui zangu.

    Uliniinua juu ya adui zangu;

    uliniokoa toka kwa watu wajeuri.

  71. 22 Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu,

    katika kusanyiko nitakusifu wewe.

    23 Ninyi ambao mnamcha Bwana, msifuni!

    Ninyi nyote wazao wote wa Yakobo, mheshimuni yeye!

    Mcheni yeye, ninyi wazao wote wa Israeli!

  72. 16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,

    asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;

    kwa maana wewe ndiwe ngome yangu

    na kimbilio langu wakati wa shida.

    17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.

    Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

    Mungu unipendaye.

  73. 5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu,

    na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake;

    yeye ni mtakatifu.

    6 Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake,

    Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake;

    walimwita Bwana,

    naye aliwajibu.

    7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu;

    walizishika sheria zake na amri alizowapa.

    8 Ee Bwana, wetu,

    ndiwe uliyewajibu,

    kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,

    ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.

    9 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu,

    mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu,

    kwa maana Bwana Mungu wetu ni mtakatifu.

  74. 1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema;

    upendo wake wadumu milele.

    2 Israeli na aseme sasa:

    “Upendo wake wadumu milele.”

    3 Nyumba ya Aroni na iseme sasa:

    “Upendo wake wadumu milele.”

    4 Wote wamchao Bwana na waseme sasa:

    “Upendo wake wadumu milele.”

  75. 1 Msifuni Bwana.

    Mwimbieni Bwana wimbo mpya,

    sifa zake katika kusanyiko la watakatifu.

  76. 19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

  77. 13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu.

  78. 20 Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana,

    ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.”

    Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu.

  79. 56 “Ahimidiwe Bwana, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose.

  80. 13 Wapiga tarumbeta na waimbaji wakaungana katika sauti linganifu, ikawa kama vile ni sauti moja, wakimsifu na kumshukuru Bwana, nao alipoinua sauti zao pamoja na tarumbeta na matoazi na vyombo vingine vya uimbaji, wakamsifu Bwana wakisema:

    “Yeye ni mwema;

    upendo wake unadumu milele.”

    Ndipo Hekalu la Bwana likajazwa na wingu, 14 nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Bwana ulijaza Hekalu la Mungu.

  81. 21 Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia Bwana na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema:

    “Mshukuruni Bwana

    kwa kuwa upendo wake wadumu milele.”

  82. 10 Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Bwana, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza Bwana, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. 11 Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Bwana hivi:

    “Yeye ni mwema;

    upendo wake kwa Israeli

    wadumu milele.”

    Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana ulikuwa umewekwa.

  83. 2 Bwana ni mwamba wangu,

    ngome yangu na mwokozi wangu,

    Mungu wangu ni mwamba,

    ambaye kwake ninakimbilia.

    Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu,

    ngome yangu.

    3 Ninamwita Bwana anayestahili kusifiwa,

    nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.

  84. 6 Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa,

    mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa.

    7 Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote,

    mwimbieni zaburi za sifa.

    8 Mungu anatawala juu ya mataifa,

    Mungu ameketi juu ya kiti chake cha enzi kitakatifu.

  85. 14 Lakini mimi, nitatumaini siku zote,

    nitakusifu zaidi na zaidi.

    15 Kinywa changu kitasimulia haki yako,

    wokovu wako mchana kutwa,

    ingawa sifahamu kipimo chake.

  86. Utenzi wa Ethani Mwezrahi.

    1 Nitaimba juu ya upendo mkuu wa Bwana milele;

    kwa kinywa changu nitajulisha uaminifu wako

    ujulikane kwa vizazi vyote.

  87. 14 Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,

    kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana.

    15 Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu,

    liadhimisheni jina la Bwana, Mungu wa Israeli,

    katika visiwa vya bahari.

  88. 33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

    wa hekima na maarifa ya Mungu!

    Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

    na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

    34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

    Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

    35 “Au ni nani aliyempa chochote

    ili arudishiwe?”

    36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

    Utukufu ni wake milele! Amen.

  89. 11 “Ni nani miongoni mwa miungu aliye kama wewe, Ee Bwana?

    Ni nani kama Wewe:

    uliyetukuka katika utakatifu,

    utishaye katika utukufu,

    ukitenda maajabu?

  90. 10 Yethro akasema, “Sifa na ziwe kwa Bwana, aliyekuokoa wewe kutoka mikononi mwa Wamisri na Farao, na aliyewaokoa watu kutoka mikononi mwa Wamisri.

  91. 6 Ezra akamsifu Bwana, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Bwana hali nyuso zao zikigusa ardhi.

  92. 17 Nitamshukuru Bwana kwa ajili ya haki yake,

    na nitaliimbia sifa jina la Bwana Aliye Juu Sana.

  93. 13 Ee Bwana, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa!

    Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti,

    14 ili niweze kutangaza sifa zako

    katika malango ya Binti Sayuni

    na huko niushangilie wokovu wako.

  94. 1 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,

    wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.

    2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,

    waambieni matendo yake yote ya ajabu.

    3 Lishangilieni jina lake takatifu,

    mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.

    4 Mtafuteni Bwana na nguvu zake,

    utafuteni uso wake siku zote.

    5 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,

    miujiza yake na hukumu alizozitamka,

  95. 21 Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana.

    Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu

    milele na milele.

  96. 21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

  97. 1 Baada ya Yesu kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

    “Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. 2 Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. 3 Nao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma. 4 Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye.

  98. 11 Tena,

    “Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote,

    na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”

  99. 1 Ndipo Mose na Waisraeli wakamwimbia Bwana wimbo huu:

    “Nitamwimbia Bwana,

    kwa kuwa ametukuzwa sana.

    Farasi na mpanda farasi

    amewatosa baharini.

    2 Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu;

    amekuwa wokovu wangu.

    Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu,

    Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

  100. 50 Kwa hiyo nitakusifu, Ee Bwana,

    katikati ya mataifa;

    nitaliimbia sifa jina lako.

  101. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.

    1 Pigeni makofi, enyi mataifa yote,

    mpigieni Mungu kelele za shangwe!

  102. 8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,

    sauti ya sifa yake isikike,

  103. 1 Msifuni Bwana, enyi mataifa yote;

    mtukuzeni yeye, enyi watu wote.

  104. 164 Ninakusifu mara saba kwa siku,

    kwa ajili ya sheria zako za haki.

  105. 19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni Bwana;

    ee nyumba ya Aroni, msifuni Bwana;

    20 ee nyumba ya Lawi, msifuni Bwana;

    ninyi mnaomcha, msifuni Bwana.

    21 Msifuni Bwana kutoka Sayuni,

    msifuni yeye aishiye Yerusalemu.

    Msifuni Bwana.

  106. 1 Msifuni Bwana!

    Ee nafsi yangu, umsifu Bwana,

    2 Nitamsifu Bwana maisha yangu yote;

    nitamwimbia Mungu wangu sifa

    wakati wote niishipo.

  107. 31 Baada ya Yuda kutoka nje, Yesu akasema, “Sasa Mwana wa Adamu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake. 32 Ikiwa Mungu ametukuzwa ndani ya Mwana, Mungu atamtukuza Mwana ndani yake mwenyewe naye atamtukuza mara.

  108. 11 Kwa sababu hii, tunawaombea ninyi bila kukoma, ili Mungu apate kuwahesabu kuwa mnastahili wito wake na kwamba kwa uwezo wake apate kutimiza kila kusudi lenu jema na kila tendo linaloongozwa na imani yenu. 12 Tunaomba hivi ili Jina la Bwana wetu Yesu lipate kutukuzwa ndani yenu, nanyi ndani yake, kulingana na neema ya Mungu wetu na Bwana Yesu Kristo.