26 Bible Verses About Forgiving Others

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Forgiving Others
  1. 12 Utusamehe deni zetu,

    kama sisi nasi tulivyokwisha

    kuwasamehe wadeni wetu.

    13 Usitutie majaribuni,

    bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

    [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

    na utukufu, hata milele. Amen].’

    14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

  2. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

  3. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  4. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”

  5. 37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa.

  6. 3 Kwa hiyo, jilindeni.

    “Kama ndugu yako akikukosea mwonye, naye akitubu, msamehe. 4 Kama akikukosea mara saba kwa siku moja na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”

  7. 21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

    23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

  8. 15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.

    18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.

    19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

  9. 21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”

    22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

    23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. 25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.

    26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.

    28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’

    29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’

    30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.

    32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.

    35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”

  10. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:

    “Kama adui yako ana njaa, mlishe;

    kama ana kiu, mpe kinywaji.

    Kwa kufanya hivyo,

    unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

  11. 43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

  12. 33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.

  13. 20 Basi Bwana akasema, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao inasikitisha sana, 21 kwamba nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”

    22 Basi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Abrahamu akabaki amesimama mbele za Bwana. 23 Ndipo Abrahamu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24 Je, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake? 25 Hilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?”

    26 Bwana akasema, “Kama nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitausamehe huo mji wote kwa ajili yao.”

    27 Kisha Abrahamu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu; 28 je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?”

    Bwana akamwambia, “Kama nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”

    29 Abrahamu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?”

    Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”

    30 Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?”

    Akajibu, “Sitapaangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”

    31 Abrahamu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, kama wakipatikana huko watu ishirini tu?”

    Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”

    32 Abrahamu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?”

    Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”

    33 Bwana alipomaliza kuzungumza na Abrahamu, akaondoka, naye Abrahamu akarudi nyumbani kwake.

  14. 4 Utusamehe dhambi zetu,

    kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.

    Wala usitutie majaribuni

    (bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’ ”

  15. 59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

  16. 8 Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema. 9 Lakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi, na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji. 10 Kwa maana mtu yeyote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote. 11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.

    12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru. 13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu yeyote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.

  17. 30 Siku iliyofuata Mose akawaambia watu, “Mmefanya dhambi kubwa. Lakini sasa nitapanda juu kwa Bwana, labda nitaweza kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu.”

    31 Hivyo Mose akarudi kwa Bwana na kumwambia, “Lo! Hawa watu wamefanya dhambi kubwa namna gani! Wamejitengenezea miungu ya dhahabu. 32 Lakini sasa nakusihi, wasamehe dhambi yao; lakini kama sivyo, basi nifute kutoka kwenye kitabu ulichoandika.”

  18. Zaburi ya Daudi. Funzo.

    1 Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake,

    ambaye dhambi zake zimefunikwa.

    2 Heri mtu yule ambaye Bwana

    hamhesabii dhambi,

    na ambaye rohoni mwake

    hamna udanganyifu.

    3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa

    kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.

    4 Usiku na mchana

    mkono wako ulinilemea,

    nguvu zangu zilinyonywa

    kama vile katika joto la kiangazi.

    5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu

    wala sikuficha uovu wangu.

    Nilisema, “Nitaungama

    makosa yangu kwa Bwana.”

    Ndipo uliponisamehe

    hatia ya dhambi yangu.

  19. 8 Heri walio na moyo safi,

    maana hao watamwona Mungu.

  20. 8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu. 9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.

  21. 7 Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote:

    Je, marafiki zake watamkwepa kiasi gani!

    Ingawa huwafuata kwa kuwasihi,

    hawapatikani popote.

  22. 17 Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo;

    wakati ajikwaapo,

    usiruhusu moyo wako ushangilie.

    18 Bwana asije akaona na kuchukia

    akaiondoa ghadhabu yake mbali naye.

  23. 21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale;

    kama ana kiu, mpe maji anywe.

    22 Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake,

    naye Bwana atakupa thawabu.

  24. 36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

  25. 3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa.

  26. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Baada ya kukemewa na nabii Nathani kwa kuzini na Bathsheba.

    1 Ee Mungu, unihurumie,

    kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,

    kwa kadiri ya huruma yako kuu,

    uyafute makosa yangu.

    2 Unioshe na uovu wangu wote

    na unitakase dhambi yangu.

    3 Kwa maana ninajua makosa yangu,

    na dhambi yangu iko mbele yangu daima.

    4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi

    na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,

    ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo,

    na kuwa na haki utoapo hukumu.