54 Bible Verses About Praying for Others
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.
17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.
-
5 “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.
9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:
“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10 Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.
11 Utupatie riziki yetu
ya kila siku.
12 Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13 Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu
[kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,
na utukufu, hata milele. Amen].’
14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
-
1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. 3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, 4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. 5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao.
-
43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.
-
26 Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. 27 Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu.
-
17 Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18 Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.
19 Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20 ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.
-
14 Huu ndio ujasiri tulio nao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. 15 Nasi kama tunajua atusikia, lolote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.
16 Kama mtu akimwona ndugu yake akitenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo. Ninamaanisha wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. 17 Jambo lolote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.
-
9 Kwa sababu hii, tangu siku ile tuliposikia habari zenu, hatujakoma kuomba kwa ajili yenu na kumsihi Mungu awajaze ninyi maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote ya kiroho na ufahamu. 10 Nasi tunaomba haya ili mpate kuishi maisha yanayostahili mbele za Bwana, na mpate kumpendeza kwa kila namna: mkizaa matunda kwa kila kazi njema, mkikua katika kumjua Mungu, 11 mkiwa mmetiwa nguvu kwa uwezo wote kwa kadiri ya nguvu yake yenye utukufu, ili mpate kuwa na wingi wa saburi na uvumilivu. Nanyi kwa furaha 12 mkimshukuru Baba, ambaye amewastahilisha kushiriki katika urithi wa watakatifu katika ufalme wa nuru. 13 Kwa maana ametuokoa kutoka ufalme wa giza na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wake mpendwa, 14 ambaye katika yeye tunao ukombozi, yaani msamaha wa dhambi.
-
3 Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi. 4 Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha, 5 kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo. 6 Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.
7 Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami. 8 Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu.
9 Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote, 10 ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo, 11 mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.
-
2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru. 3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa. 4 Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena.
-
16 Furahini siku zote; 17 ombeni bila kukoma; 18 shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.
-
13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14 Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.
15 “Kama mnanipenda, mtazishika amri zangu. 16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine akae nanyi milele. 17 Huyo ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu haumwoni wala haumjui. Ninyi mnamjua kwa kuwa yuko pamoja nanyi naye anakaa ndani yenu.
-
6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu. 7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia usiku na mchana? Je, atakawia kuwasaidia? 8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”
9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiamini kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine: 10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. 11 Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’
13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’
14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.”
-
6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
-
2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu. 3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.
-
24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [
-
27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia. 28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya.
-
7 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Shuka, kwa sababu watu wako, uliowatoa Misri, wamepotoka. 8 Wamekuwa wepesi kugeuka na kuacha niliyowaamuru, na wamejitengenezea sanamu ya kuyeyusha yenye umbo la ndama. Wameisujudia na kuitolea dhabihu, nao wamesema, ‘Hii ndiyo miungu yenu, ee Israeli iliyokupandisha kutoka Misri.’ ”
9 Bwana akamwambia Mose, “Nimeona watu hawa, nao ni watu wenye shingo ngumu. 10 Sasa niache ili hasira yangu ipate kuwaka dhidi yao, nami nipate kuwaangamiza. Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.”
11 Lakini Mose akamsihi Bwana Mungu wake, akasema, “Ee Bwana, kwa nini hasira yako iwake dhidi ya watu wako, wale uliowatoa Misri kwa uweza mkuu na mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri waseme, ‘Ni kwa nia mbaya aliwatoa Misri, ili awaue milimani na kuwafuta usoni mwa dunia’? Achilia mbali hasira yako kali, waonee huruma na usilete maafa juu ya watu wako. 13 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Israeli, ambao uliwaapia kwa nafsi yako mwenyewe: ‘Nitawafanya uzao wako kuwa wengi kama nyota za angani, nami nitawapa wazao wako nchi hii yote ambayo niliwaahidia, nayo itakuwa urithi wao milele.’ ” 14 Kisha Bwana akawaonea huruma, wala hakuleta juu ya watu wake maafa aliyokuwa amekusudia.
-
10 Baada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Bwana akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni.
-
7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?
-
34 Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura.
-
23 Basi pamekuwepo na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani. 24 Lakini kwa sababu Yesu anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu. 25 Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.
-
15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”
-
25 Ndugu, tuombeeni.
-
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
-
18 Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. 19 Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.
20 Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Yesu, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21 awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.
-
2 Akawaambia, “Mnapoomba, semeni:
“ ‘Baba yetu (uliye mbinguni),
jina lako litukuzwe,
ufalme wako uje.
(Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.)
3 Utupatie kila siku riziki yetu.
4 Utusamehe dhambi zetu,
kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.
Wala usitutie majaribuni
(bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’ ”
5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu. 6 Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’
7 “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’ 8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.
9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
-
7 Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa.
-
15 Kwa sababu hii, tangu niliposikia juu ya imani yenu katika Bwana Yesu na upendo wenu kwa watakatifu wote, 16 sijaacha kumshukuru Mungu kwa ajili yenu, nikiwakumbuka katika maombi yangu. 17 Nazidi kumwomba Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awajalieni ninyi roho ya hekima na ya ufunuo, ili mpate kumjua zaidi. 18 Ninaomba pia kwamba macho ya mioyo yenu yatiwe nuru ili mpate kujua tumaini mliloitiwa, utajiri wa urithi wa utukufu wake kwa watakatifu 19 na uweza wake mkuu usiolinganishwa kwa ajili yetu sisi tuaminio. Uweza huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na ile nguvu kuu mno 20 aliyoitumia katika Kristo alipomfufua kutoka kwa wafu, na akamketisha mkono wake wa kuume huko mbinguni, 21 juu sana kuliko falme zote na mamlaka, enzi na milki, na juu ya kila jina litajwalo, si katika ulimwengu huu tu, bali katika ule ujao pia. 22 Naye Mungu ameweka vitu vyote viwe chini ya miguu yake na amemfanya yeye awe kichwa cha vitu vyote kwa ajili ya Kanisa, 23 ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake yeye aliye yote katika yote.
-
5 Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana.” 6 Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za Bwana. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana.” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa.
7 Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. 8 Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” 9 Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Akamlilia Bwana kwa niaba ya Israeli, naye Bwana akamjibu.
-
21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeshe mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali zetu zote. 22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.” 23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.
-
38 Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”
39 Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”
-
15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. 17 Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli. 18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. 19 Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.
20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23 Mimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
-
34 Ni nani basi atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu aliyekufa, naam, zaidi ya hayo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yuko mkono wa kuume wa Mungu, naye pia anatuombea.
-
14 Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe, naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana. 15 Naye Hezekia akamwomba Bwana akisema: “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. 16 Tega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.
17 “Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya na nchi zao. 18 Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 19 Sasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”
-
60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.
-
3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.
-
18 Ndipo tena nikasujudu mbele za Bwana kwa siku arobaini usiku na mchana. Sikula mkate wala sikunywa maji, kwa sababu ya dhambi yote mliyoifanya, mkifanya lile lililo ovu mbele za Bwana na kumkasirisha. 19 Niliogopa hasira na ghadhabu ya Bwana, kwa kuwa aliwakasirikia vya kutosha na kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiliza tena.
-
16 Lakini ninamwita Mungu,
naye Bwana huniokoa.
17 Jioni, asubuhi na adhuhuri
ninalia kwa huzuni,
naye husikia sauti yangu.
-
14 “Wewe usiwaombee watu hawa wala kufanya maombezi yoyote au kunisihi kwa ajili yao, kwa sababu sitawasikiliza watakaponiita wakati wa taabu yao.
-
2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.
-
25 Nilianguka kifudifudi mbele za Bwana kwa zile siku arobaini usiku na mchana kwa sababu Bwana alikuwa amesema angewaangamiza ninyi. 26 Nilimwomba Bwana na kusema, “Ee Bwana Mwenyezi, usiangamize watu wako, urithi wako mwenyewe ule ulioukomboa kwa uweza wako mkuu na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu. 27 Wakumbuke watumishi wako Abrahamu, Isaki na Yakobo. Usiangalie ukaidi wa watu hawa, uovu wao wala dhambi yao. 28 Watu wa nchi ile uliyotutoa sisi wasije wakasema, ‘Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwachukua mpaka nchi aliyokuwa amewaahidia, kwa sababu aliwachukia, akawaleta ili aje kuwaua jangwani.’ 29 Bali wao ni watu wako, urithi wako ule ulioutoa Misri kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyooka.”
-
5 Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwa Bwana Mungu wangu. 6 Nami nikaomba:
“Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni.
-
16 “Kwa hiyo usiombe kwa ajili ya watu hawa, wala usinililie, na usifanye maombi kwa ajili yao; usinisihi, kwa sababu sitakusikiliza.
-
11 Kisha Bwana akaniambia, “Usiombe kwa ajili ya mafanikio ya watu hawa.
-
21 Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”
-
14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.
-
9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa. 11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.
-
8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.
-
9 Mose akasema, “Ee Bwana, kama nimepata kibali mbele zako, basi Bwana uende pamoja nasi. Ingawa watu hawa ni wenye shingo ngumu, samehe uovu wetu na dhambi yetu, tuchukue kuwa urithi wako.”
-
19 Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”
20 Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa moyo wenu wote. 21 Msigeukie sanamu zisizofaa. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana. 22 Kwa ajili ya jina lake kuu Bwana hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza Bwana kuwafanya kuwa wake mwenyewe. 23 Kwa habari yangu, iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya Bwana kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na ya kunyooka.
-
54 Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwa Bwana, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya Bwana, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni.
-
9 Ninawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako.
-
7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.
Shows Read in context, Share and Copy.