54 Bible Verses About Mother's Day

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Mother's Day
  1. 10 Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata?

    Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani.

    11 Mume wake anamwamini kikamilifu

    wala hakosi kitu chochote cha thamani.

    12 Humtendea mumewe mema, wala si mabaya,

    siku zote za maisha yake.

    13 Huchagua sufu na kitani

    naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii.

    14 Yeye ni kama meli za biashara

    akileta chakula chake kutoka mbali.

    15 Yeye huamka kungali bado giza

    huwapa jamaa yake chakula

    na mafungu kwa watumishi wake wa kike.

    16 Huangalia shamba na kulinunua,

    kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu.

    17 Hufanya kazi zake kwa nguvu,

    mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake.

    18 Huona kwamba biashara yake ina faida,

    wala taa yake haizimiki usiku.

    19 Huweka mikono yake kwenye pia,

    navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi.

    20 Huwanyooshea maskini mikono yake

    na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake.

    21 Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake,

    kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto.

    22 Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake,

    yeye huvaa kitani safi na urujuani.

    23 Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji,

    aketipo miongoni mwa wazee wa nchi.

    24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza,

    naye huwauzia wafanyabiashara mishipi.

    25 Amevikwa nguvu na heshima,

    anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo.

    26 Huzungumza kwa hekima

    na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake.

    27 Huangalia mambo ya nyumbani mwake

    wala hali chakula cha uvivu.

    28 Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa,

    mumewe pia humsifu, akisema:

    29 “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri,

    lakini wewe umewapita wote.”

    30 Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi,

    bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa.

    31 Mpe thawabu anayostahili,

    nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.

  2. 25 Wakati huo huo karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Maria mke wa Klopa, na Maria Magdalene. 26 Yesu alipomwona mama yake mahali pale pamoja na yule mwanafunzi aliyempenda wamesimama karibu, akamwambia mama yake, “Mwanamke, huyo hapo ndiye mwanao,” 27 kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyo hapo ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani kwake.

  3. 1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2 “Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3 “upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

  4. 22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,

    wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.

    23 Nunua kweli wala usiiuze,

    pata hekima, adabu na ufahamu.

    24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,

    naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.

    25 Baba yako na mama yako na wafurahi,

    mama aliyekuzaa na ashangilie!

  5. 12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.

  6. 8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

    9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

    na mkufu wa kuipamba shingo yako.

  7. 6 Mfundishe mtoto njia impasayo kuiendea,

    naye hataiacha hata akiwa mzee.

  8. 3 Vivyo hivyo, wafundishe wanawake wazee kuwa na mwenendo wa utakatifu, wala wasiwe wasingiziaji au walevi, bali wafundishe yale yaliyo mema, 4 ili waweze kuwafundisha wanawake vijana kuwa na kiasi, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao, 5 wawe waaminifu, watakatifu, wakitunza vyema nyumba zao, wema, watiifu kwa waume zao, ili mtu yeyote asije akalikufuru neno la Mungu.

  9. 1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama kunao wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4 Badala yake, kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa moyoni, yaani uzuri usioharibika wa roho ya upole na utulivu, ambayo ni ya thamani sana machoni pa Mungu.

  10. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

  11. 3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana,

    watoto ni zawadi kutoka kwake.

    4 Kama mishale mikononi mwa shujaa

    ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.

    5 Heri mtu ambaye podo lake

    limejazwa nao.

    Hawataaibishwa wanaposhindana

    na adui zao langoni.

  12. 41 Naye Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto aliyekuwa tumboni mwake akaruka. Elizabeti akajazwa na Roho Mtakatifu, 42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, “Umebarikiwa wewe miongoni mwa wanawake, naye mtoto utakayemzaa amebarikiwa. 43 Lakini ni kwa nini mimi nimepata upendeleo kiasi hiki, hata mama wa Bwana wangu afike kwangu? 44 Mara tu niliposikia sauti ya salamu yako, mtoto aliyeko tumboni mwangu aliruka kwa furaha. 45 Amebarikiwa yeye aliyeamini kwamba lile Bwana alilomwambia litatimizwa.”

    46 Naye Maria akasema:

    “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

    47 nayo roho yangu inamfurahia

    Mungu Mwokozi wangu,

    48 kwa kuwa ameangalia kwa fadhili

    unyonge wa mtumishi wake.

    Hakika tangu sasa vizazi vyote vitaniita aliyebarikiwa,

    49 kwa maana yeye Mwenye Nguvu

    amenitendea mambo ya ajabu:

    jina lake ni takatifu.

  13. 5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo mimi ninasadiki sasa wewe pia unayo.

  14. 20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

    21 Yafunge katika moyo wako daima,

    yakaze kuizunguka shingo yako.

    22 Wakati utembeapo, yatakuongoza;

    wakati ulalapo, yatakulinda;

    wakati uamkapo, yatazungumza nawe.

    23 Kwa maana amri hizi ni taa,

    mafundisho haya ni mwanga

    na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,

  15. 4 Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. 5 Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. 6 Upendo haufurahii mabaya bali hufurahi pamoja na kweli. 7 Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.

  16. 1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako; 2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.

  17. 26 naye Hana akamwambia Eli, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu, mimi ndiye yule mama ambaye alisimama hapa karibu nawe akiomba kwa Bwana. 27 Niliomba mtoto huyu, naye Bwana amenijalia kile nilichomwomba. 28 Hivyo sasa ninamtoa kwa Bwana. Kwa maana maisha yake yote atakuwa ametolewa kwa Bwana.” Naye akamwabudu Bwana huko.

  18. 15 Fimbo ya maonyo hutia hekima,

    bali mtoto aliyeachiwa bila maonyo

    humwaibisha mama yake.

    16 Wakati waovu wanapostawi,

    pia dhambi vivyo hivyo,

    lakini wenye haki wataliona anguko lao.

    17 Mrudi mwanao, naye atakupa amani,

    atakufurahisha nafsi yako.

  19. 46 Wakati alikuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye. 47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”

    48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?” 49 Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu! 50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

  20. 35 Kwa maana nimekuja kumfitini

    “ ‘mtu na babaye,

    binti na mamaye,

    mkwe na mama mkwe wake;

    36 nao adui za mtu watakuwa

    ni wale watu wa nyumbani kwake.’

    37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu.

  21. 48 Yosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”

    49 Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”

    50 Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.

    51 Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote.

  22. 57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe. 59 Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, 60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake. 61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwepo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

  23. 16 Lakini Ruthu akajibu, “Usinisihi nikuache au niache kukufuata. Utakakokwenda nami nitakwenda, na wewe utakapoishi nitaishi. Watu wako watakuwa watu wangu, na Mungu wako atakuwa Mungu wangu. 17 Pale utakapofia nami nitafia hapo, na papo hapo nitazikwa. Bwana na aniadhibu vikali, kama kitu kingine chochote kitanitenga nawe isipokuwa kifo.”

  24. 38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana akisikiliza yale aliyokuwa akisema. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

    41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

  25. 20 Unazijua amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

  26. 14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.

  27. 13 Basi sasa, yanadumu mambo haya matatu: Imani, tumaini na upendo. Lakini lililo kuu miongoni mwa haya matatu ni upendo.

  28. 8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.

  29. 4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

  30. 5 Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako. 7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo. 8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako. 9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.

  31. 18 Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomrudi, 19 baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake. 20 Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.” 21 Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe mpaka afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.

  32. 1 Mithali za Solomoni:

    Mwana mwenye hekima

    huleta furaha kwa baba yake,

    lakini mwana mpumbavu

    huleta huzuni kwa mama yake.

  33. 6 Wana wa wana ni taji la wazee,

    nao wazazi ni fahari ya watoto wao.

  34. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  35. 22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria.

  36. 22 Kisha Bwana Mungu akamfanya mwanamke kutoka kwenye ule ubavu aliouchukua kutoka kwa huyo mwanaume, akamleta huyo mwanamke kwa huyo mwanaume.

    23 Huyo mwanaume akasema,

    “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu

    na nyama ya nyama yangu,

    ataitwa ‘mwanamke,’

    kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.”

    24 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

  37. 15 Nami nitaweka uadui

    kati yako na huyo mwanamke,

    na kati ya uzao wako na wake,

    yeye atakuponda kichwa,

    nawe utamuuma kisigino.”

    16 Kwa mwanamke akasema,

    “Nitakuzidishia sana utungu wakati wa kuzaa kwako;

    kwa utungu utazaa watoto.

    Tamaa yako itakuwa kwa mumeo

    naye atakutawala.”

  38. 20 Adamu akamwita mkewe Eva, kwa kuwa atakuwa mama wa wote walio hai.

  39. 16 Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima,

    bali wanaume wakorofi hupata mali tu.

  40. 22 Apataye mke apata kitu chema

    naye ajipatia kibali kwa Bwana.

  41. 20 Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake,

    taa yake itazimwa katika giza nene.

  42. 1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.

  43. 29 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au mama au baba, au watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, 30 ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu: nyumba, ndugu wa kiume na wa kike, mama na baba na watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

  44. 34 Maria akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

    35 Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”

    38 Maria akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Bwana. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.

  45. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  46. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo.

  47. 11 kama tai avurugaye kiota chake,

    na kurukaruka juu ya makinda yake,

    ambaye hutanda mabawa yake kuwadaka,

    na huwachukua kwenye mabawa yake.

  48. Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.

    1 Moyo wangu hauna kiburi, Ee Bwana,

    macho yangu hayajivuni;

    sijishughulishi na mambo makuu kunizidi

    wala mambo ya ajabu mno kwangu.

    2 Lakini nimetuliza na kunyamazisha nafsi yangu;

    kama mtoto aliyeachishwa kunyonya na mama yake,

    kama mtoto aliyeachishwa kunyonya

    ndivyo ilivyo nafsi iliyoko ndani yangu.

  49. 14 Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi,

    bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.

  50. 20 Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.

    21 Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”

    22 Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”

    Wakajibu, “Tunaweza.”

    23 Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”

  51. 29 Mara walipotoka katika sinagogi, walikwenda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea. 30 Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. 31 Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia.

  52. 27 Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”

    28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

  53. 34 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka!

  54. 2 Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu. 3 Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.