85 Bible Verses About Sympathy

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Sympathy
  1. 2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

    3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo. 6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.

  2. 14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  3. 18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

    19 Mwenye haki ana mateso mengi,

    lakini Bwana humwokoa nayo yote,

    20 huhifadhi mifupa yake yote,

    hata mmoja hautavunjika.

    21 Ubaya utamuua mtu mwovu,

    nao adui za mwenye haki watahukumiwa.

    22 Bwana huwakomboa watumishi wake,

    yeyote anayemkimbilia yeye

    hatahukumiwa kamwe.

  4. Mahubiri Ya Yesu Kwenye Mlima

    1 Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. 2 Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:

    3 “Heri walio maskini wa roho,

    maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

    4 Heri wale wanaohuzunika,

    maana hao watafarijiwa.

  5. 13 Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini. 14 Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake. 15 Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti. 16 Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza. 17 Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

  6. 1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena. 2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe. 3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. 4 Atafuta kila chozi kutoka macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

    5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”

  7. 2 Hunilaza katika malisho

    ya majani mabichi,

    kando ya maji matulivu huniongoza,

    3 hunihuisha nafsi yangu.

    Huniongoza katika njia za haki

    kwa ajili ya jina lake.

    4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

    5 Waandaa meza mbele yangu

    machoni pa adui zangu.

    Umenipaka mafuta kichwani pangu,

    kikombe changu kinafurika.

    6 Hakika wema na upendo vitanifuata

    siku zote za maisha yangu,

    nami nitakaa nyumbani mwa Bwana

    milele.

  8. 35 Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 Alipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”

  9. 1 Kama kukiwa na jambo lolote la kutia moyo katika kuunganishwa na Kristo, kukiwa faraja yoyote katika upendo wake, kukiwa na ushirika wowote na Roho, kukiwa na wema wowote na huruma, 2 basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia moja, mkiwa na upendo huo moja, mkiwa wa roho na kusudi moja. 3 Msitende jambo lolote kwa nia ya kujitukuza wala kujivuna, bali kwa unyenyekevu kila mtu amhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4 Kila mmoja wenu asiangalie faida yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

    5 Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu:

    6 Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,

    hakuona kule kuwa sawa na Mungu

    kuwa kitu cha kushikilia,

    7 bali alijifanya si kitu,

    akachukua hali hasa na mtumwa,

    naye akazaliwa katika umbo la mwanadamu.

    8 Naye akiwa na umbo la mwanadamu,

    alijinyenyekeza, akatii hata mauti:

    naam, mauti ya msalaba!

  10. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

  11. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

  12. 33 Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”

    Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”

    35 Yesu akalia machozi.

  13. 8 Hatimaye, ninyi nyote kuweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, na mwe wasikitivu na wanyenyekevu.

  14. 25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

    28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  15. 15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao.

  16. 11 Basi marafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia juu ya taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga toka manyumbani mwao, nao wakakutana pamoja kwa makubaliano kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. 12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. 13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.

  17. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  18. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

    3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

    milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

  19. 22 Hivyo ninyi mna maumivu sasa, lakini nitawaona tena, nayo mioyo yenu itafurahi na furaha yenu hakuna awaondoleaye.

  20. 16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu. 17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo? 18 Watoto wapendwa, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na kweli. 19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu 20 kila mara mioyo yetu inapotuhukumu. Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, naye anajua kila kitu.

    21 Wapendwa, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu, 22 lolote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza. 23 Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru. 24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kwa njia ya Roho yule aliyetupa.

  21. 14 Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, 15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti. 16 Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu. 17 Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu. 18 Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.

  22. 1 Yesu akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi pia. 2 Nyumbani kwa Baba yangu kuna makao mengi. Kama sivyo, ningeliwaambia. Naenda kuwaandalia makao. 3 Nami nikienda na kuwaandalia makao, nitarudi tena na kuwachukua mkae pamoja nami, ili mahali nilipo, nanyi mpate kuwepo. 4 Ninyi mnajua njia ya kufika ninakokwenda.”

  23. 26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,

    bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu

    na fungu langu milele.

  24. 12 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

    “Nitamwongezea amani kama mto,

    nao utajiri wa mataifa kama kijito kifurikacho;

    utanyonya na kuchukuliwa mikononi mwake

    na kubembelezwa magotini pake.

    13 Kama mama anavyomfariji mtoto wake,

    ndivyo nitakavyokufariji wewe,

    nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.”

    14 Wakati mtakapoona jambo hili, mioyo yenu itashangilia,

    nanyi mtastawi kama majani;

    mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake,

    bali ghadhabu yake kali

    itaonyeshwa kwa adui zake.

  25. 25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

    28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini.

  26. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

  27. 13 Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. 14 Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

  28. 9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,

    ni ngome imara wakati wa shida.

    10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

    kwa maana wewe Bwana,

    hujawaacha kamwe wakutafutao.

  29. 3 Anawaponya waliovunjika mioyo

    na kuvifunga vidonda vyao.

  30. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  31. 13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;

    furahi, ee dunia;

    pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!

    Kwa maana Bwana anawafariji watu wake,

    naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.

  32. 11 Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye. 12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. 13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”

    14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” 15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.

    16 Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”

  33. 40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akamwomba akipiga magoti, akamwambia, “Ukitaka, waweza kunitakasa.”

    41 Yesu, akiwa amejawa na huruma, akanyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” 42 Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. 43 Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake 44 akimwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Mose kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” 45 Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi lakini alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

  34. 12 Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13 Vumilianeni na kusameheana mtu akiwa na lalamiko lolote dhidi ya mwenzake. Sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14 Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

    15 Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena kuweni watu wa shukrani. 16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17 Lolote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

  35. 25 Je, sikulia kwa ajili ya wale waliokuwa katika taabu?

    Je, nafsi yangu haikusononeka kwa ajili ya maskini?

  36. 50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii:

    Ahadi yako inahifadhi maisha yangu.

  37. 17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

    naye atamtuza kwa aliyotenda.

  38. 31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali

    na Bwana milele.

    32 Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma,

    kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.

    33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso

    au huzuni watoto wa wanadamu.

  39. 1 Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo.

  40. 3 Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.

  41. 4 Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,

    kama mngekuwa katika hali yangu;

    ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,

    na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

    5 Lakini kinywa changu kingewatia moyo;

    faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu.

  42. 14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele;

    atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.

  43. 1 Mwenye haki hupotea,

    wala hakuna hata mmoja awazaye hilo moyoni mwake;

    watu wanaomcha Mungu huondolewa,

    wala hakuna hata mmoja anayeelewa

    kuwa wenye haki wameondolewa

    ili wasipatikane na maovu.

    2 Wale waendao kwa unyofu

    huwa na amani;

    hupata pumziko walalapo mautini.

  44. 5 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga, usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeziondoa baraka zangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema Bwana. 6 “Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao.

  45. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  46. 11 Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba awatendeavyo watoto wake. 12 Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yampendezayo Mungu, anayewaita katika Ufalme na utukufu wake.

  47. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

    23 Lakini wewe, Ee Mungu,

    utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.

    Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,

    hawataishi nusu ya siku zao.

    Lakini mimi ninakutumaini wewe.

  48. 7 Kwa kuwa hakuna hata mmoja wetu anayeishi kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna hata mmoja wetu afaye kwa ajili yake mwenyewe. 8 Kama tunaishi, tunaishi kwa Bwana, nasi pia tukifa tunakufa kwa Bwana. Kwa hiyo basi, kama tukiishi au kama tukifa, sisi ni mali ya Bwana.

    9 Kwani kwa sababu hii hasa, Kristo alikufa na akawa hai tena kusudi apate kuwa Bwana wa wote, yaani, waliokufa na walio hai.

  49. 2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea wema.”

    Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji, 3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?”

  50. 14 “Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,

    hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.

    15 Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa,

    ni kama vijito vya msimu,

    ni kama vijito ambavyo hufurika

    16 wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo,

    ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,

    17 lakini hukauka majira ya ukame,

    na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.

    18 Misafara hugeuka kutoka njia zake;

    hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.

  51. 2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita,

    ninaita huku moyo wangu unadhoofika;

    uniongoze kwenye mwamba

    ule ulio juu kuliko mimi.

  52. 20 Dharau zimenivunja moyo

    na nimekata tamaa,

    nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata,

    wa kunituliza, lakini sikumpata.

  53. 15 Kifo cha watakatifu kina thamani

    machoni pa Bwana.

  54. 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake.

    “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu.

  55. 41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia, 42 akisema, “Laiti ungalijua hata wewe leo yale ambayo yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako.

  56. 10 Nina furaha kubwa katika Bwana kwamba hatimaye mmeanza upya kushughulika tena na maisha yangu. Kweli mmekuwa mkinifikiria lakini mlikuwa hamjapata nafasi ya kufanya hivyo. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

    14 Lakini, mlifanya vyema kushiriki nami katika taabu zangu. 15 Zaidi ya hayo, ninyi Wafilipi mnajua kwamba siku za kwanza nilipoanza kuhubiri Injili, nilipoondoka Makedonia, hakuna kanisa jingine lililoshiriki nami katika masuala ya kutoa na kupokea isipokuwa ninyi. 16 Kwa maana hata nilipokuwa huko Thesalonike, mliniletea msaada kwa ajili ya mahitaji yangu zaidi ya mara moja. 17 Si kwamba natafuta sana yale matoleo, bali natafuta sana ile faida itakayozidi sana kwa upande wenu. 18 Nimelipwa kikamilifu hata na zaidi; nimetoshelezwa kabisa sasa, kwa kuwa nimepokea kutoka kwa Epafrodito vile vitu mlivyonitumia, sadaka yenye harufu nzuri, dhabihu inayokubalika na ya kumpendeza Mungu. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

    20 Mungu wetu aliye Baba yetu apewe utukufu milele na milele. Amen.

  57. 34 Mliwahurumia wale waliokuwa kifungoni, mkikubali kwa furaha kunyangʼanywa mali zenu kwa maana mlijua kwamba mnayo mali iliyo bora zaidi idumuyo.

  58. 6 Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Kiebrania.”

  59. 33 “ ‘Wakati mgeni anaishi pamoja nawe katika nchi yako, usimnyanyase. 34 Mgeni anayeishi pamoja nawe ni lazima umtendee kama mmoja wa wazawa wa nchi yako. Mpende kama unavyojipenda mwenyewe, kwa maana ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Bwana Mungu wako.

  60. 6 “Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

    kufungua minyororo ya udhalimu,

    na kufungua kamba za nira,

    kuwaweka huru walioonewa,

    na kuvunja kila nira?

    7 Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

    na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,

    unapomwona aliye uchi, umvike,

    wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe?

  61. 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’

  62. 25 ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. 26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

  63. 5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi. 6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha. 7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi. 8 Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake. 9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo. 10 Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.

  64. 6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito. 7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.

  65. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  66. 3 Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;

    vifunge shingoni mwako,

    viandike katika ubao wa moyo wako.

    4 Ndipo utapata kibali na jina zuri

    mbele za Mungu na mwanadamu.

    5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  67. 20 Ninayakumbuka vyema,

    nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.

    21 Hata hivyo najikumbusha neno hili

    na kwa hiyo ninalo tumaini.

    22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii,

    kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.

    23 Ni mpya kila asubuhi,

    uaminifu wako ni mkuu.

    24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,

    kwa hiyo nitamngojea.”

    25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,

    kwa yule ambaye humtafuta;

    26 ni vyema kungojea kwa utulivu

    kwa ajili ya wokovu wa Bwana.

  68. 7 Heri wenye huruma,

    maana hao watapata rehema.

  69. 12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.

  70. 21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”

    22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

    23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. 25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.

    26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.

    28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’

    29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’

    30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.

    32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.

    35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”

  71. 9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, 10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.

  72. 2 Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka.

  73. 67 Ndipo Isaki akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake, Isaki akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaki akampenda, akafarijika baada ya kifo cha mama yake.

  74. 5 Bwana ni mwenye neema na haki,

    Mungu wetu ni mwingi wa huruma.

    6 Bwana huwalinda wanyenyekevu,

    nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.

  75. 1 Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu,

    kwa sababu Bwana amenitia mafuta

    kuwahubiria maskini habari njema.

    Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo,

    kuwatangazia mateka uhuru wao,

    na hao waliofungwa

    habari za kufunguliwa kwao;

    2 kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,

    na siku ya kisasi ya Mungu wetu,

    kuwafariji wote waombolezao,

    3 na kuwapa mahitaji

    wale wanaohuzunika katika Sayuni,

    ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu,

    mafuta ya furaha badala ya maombolezo,

    vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa.

    Nao wataitwa mialoni ya haki,

    pando la Bwana,

    ili kuonyesha utukufu wake.

  76. 36 “Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”

    37 Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”

  77. 19 Ingawa mimi ni huru, wala si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya kuwa mtumwa wa kila mtu, ili niweze kuwavuta wengi kadri iwezekanavyo. 20 Kwa Wayahudi, nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa watu wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama aliye chini ya sheria (ingawa mimi siko chini ya sheria), ili niweze kuwapata wale walio chini ya sheria. 21 Kwa watu wasio na sheria nilikuwa kama asiye na sheria (ingawa siko huru mbali na sheria ya Mungu, bali niko chini ya sheria ya Kristo), ili niweze kuwapata wale wasio na sheria. 22 Kwa walio dhaifu nilikuwa dhaifu, ili niweze kuwapata walio dhaifu. Nimekuwa mtu wa hali zote kwa watu wote ili kwa njia yoyote niweze kuwaokoa baadhi yao. 23 Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, ili nipate kushiriki baraka zake.

    24 Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wote wanaoshindana hukimbia, lakini ni mmoja wao tu apewaye tuzo? Kwa hiyo kimbieni katika mashindano kwa jinsi ambavyo mtapata tuzo.

    25 Kila mmoja anayeshiriki katika mashindano hufanya mazoezi makali. Wao hufanya hivyo ili wapokee taji isiyodumu, lakini sisi tunafanya hivyo ili kupata taji idumuyo milele. 26 Kwa hiyo mimi sikimbii kama mtu akimbiaye bila lengo, sipigani kama mtu anayepiga hewa, 27 la, bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha ili nikiisha kuwahubiria wengine, mimi nisiwe mtu wa kukataliwa.

  78. 14 Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni,

    umekubali kuyapokea mkononi mwako.

    Mhanga anajisalimisha kwako,

    wewe ni msaada wa yatima.

  79. 8 Andika maombolezo yangu,

    orodhesha machozi yangu katika gombo lako:

    je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?

  80. 16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako,

    asubuhi nitaimba juu ya upendo wako;

    kwa maana wewe ndiwe ngome yangu

    na kimbilio langu wakati wa shida.

    17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa.

    Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu,

    Mungu unipendaye.

  81. 4 Hakika alichukua udhaifu wetu

    na akajitwika huzuni zetu,

    hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu,

    akapigwa sana naye, na kuteswa.

  82. 15 Tazama chini kutoka mbinguni ukaone

    kutoka kiti chako cha enzi

    kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu.

    Uko wapi wivu wako na uweza wako?

    Umetuzuilia wema wako na huruma zako.

  83. 1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji

    na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!

    Ningelia usiku na mchana

    kwa kuuawa kwa watu wangu.

  84. 30 Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”

    32 Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

    33 Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”

    34 Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.

  85. 15 Ataniita, nami nitamjibu;

    nitakuwa pamoja naye katika taabu,

    nitamwokoa na kumheshimu.