101 Bible Verses About Lying and Deceit

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Lying and Deceit
  1. 5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lolote. 6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.

    8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha kutoka kwenye udhalimu wote. 10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

  2. 17 Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika,

    bali shahidi wa uongo husema uongo.

    18 Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga,

    bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.

    19 Midomo isemayo kweli hudumu milele,

    bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.

    20 Upo udanganyifu katika mioyo

    ya wale ambao hupanga mabaya,

    bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.

    21 Hakuna dhara linalompata mwenye haki,

    bali waovu wana taabu nyingi.

    22 Bwana anachukia sana midomo idanganyayo,

    bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.

  3. 9 Msiambiane uongo, kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10 nanyi mmevaa utu mpya, unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11 Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote, na ndani ya wote.

  4. 17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

    20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

    25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27 wala msimpe ibilisi nafasi. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

    29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  5. 42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. 43 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho. 44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo. 45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini! 46 Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini? 47 Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”

  6. 1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikia haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu yeyote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo, Mwenye Haki. 2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

    3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua, tukizishika amri zake. 4 Mtu yeyote asemaye kuwa, “Ninamjua,” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli. 5 Lakini mtu yeyote anayelitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake. 6 Yeyote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

  7. 23 Kama rangi ingʼaayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo

    ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.

    24 Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake,

    lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.

    25 Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini,

    kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.

    26 Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu,

    lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.

    27 Kama mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake,

    kama mtu akivingirisha jiwe, litamrudia.

    28 Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza,

    nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.

  8. 3 Sitaweka mbele ya macho yangu

    kitu kiovu.

    Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani;

    hawatashikamana nami.

    4 Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami;

    nitajitenga na kila ubaya.

    5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri,

    huyo nitamnyamazisha;

    mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi

    huyo sitamvumilia.

    6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi,

    ili waweze kuishi pamoja nami;

    yeye ambaye moyo wake hauna lawama

    atanitumikia.

    7 Mdanganyifu hatakaa

    nyumbani mwangu,

    yeye asemaye kwa uongo

    hatasimama mbele yangu.

    8 Kila asubuhi nitawanyamazisha

    waovu wote katika nchi;

    nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya

    kutoka mji wa Bwana.

  9. 12 Mtu mbaya sana na mlaghai,

    ambaye huzungukazunguka

    na maneno ya upotovu,

    13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake,

    anayetoa ishara kwa miguu yake

    na kuashiria kwa vidole vyake,

    14 ambaye hupanga ubaya

    kwa udanganyifu moyoni mwake:

    daima huchochea fitina.

    15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula;

    ataangamizwa mara, pasipo msaada.

    16 Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana,

    naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:

    17 macho ya kiburi,

    ulimi udanganyao,

    mikono imwagayo damu isiyo na hatia,

    18 moyo uwazao mipango miovu,

    miguu iliyo myepesi kukimbilia uovu,

    19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo,

    na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

    20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,

    wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

  10. 1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini ambao Bwana Mungu aliwafanya. Nyoka akamwambia mwanamke, “Ati kweli Mungu alisema, ‘Kamwe msile matunda ya mti wowote wa bustanini’?”

    2 Mwanamke akamjibu nyoka, “Tunaweza kula matunda ya miti iliyoko bustanini, 3 lakini Mungu alisema, ‘Kamwe msile tunda la mti ulio katikati ya bustani, wala kuugusa, la sivyo mtakufa.’ ”

    4 Lakini nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa. 5 Kwa maana Mungu anajua ya kuwa wakati mtakapoyala, macho yenu yatafumbuliwa, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

  11. 10 Kwa maana wako wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, hasa wale wa kikundi cha tohara. 11 Hao ni lazima wanyamazishwe, kwa sababu wanaharibu watu wa nyumba nzima wakifundisha mambo yasiyowapasa kufundisha. Wanafanya hivyo kwa ajili ya kujipatia mapato ya udanganyifu. 12 Hata mmojawapo wa manabii wao mwenyewe amesema, “Wakrete ni waongo siku zote, wanyama wabaya, walafi, wavivu.” 13 Ushuhuda huu ni kweli. Kwa hiyo, uwakemee kwa ukali wapate kuwa wazima katika imani, 14 ili wasiendelee kuangalia hadithi za Kiyahudi au maagizo ya wale watu wanaoikataa kweli. 15 Kwa wale walio safi, kila kitu ni safi kwao. Lakini kwa wale waliopotoka na wasioamini, hakuna chochote kilicho safi. Kwa kweli nia zao na dhamiri zao zimepotoka. 16 Wanadai kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Hao watu ni chukizo, wasiotii, wasiofaa kwa jambo lolote jema.

  12. 16 Usimshuhudie jirani yako uongo.

  13. 8 Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. 9 Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo, 10 na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa. 11 Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo, 12 na wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.

  14. 9 Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote,

    ni mwovu kupita kiasi.

    Ni nani awezaye kuujua?

    10 “Mimi Bwana huchunguza moyo

    na kuzijaribu nia,

    ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake,

    kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”

  15. 7 Yeye ashindaye atayarithi haya yote, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. 8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

  16. 4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu,

    kwako mtu mwovu hataishi.

    5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,

    unawachukia wote watendao mabaya.

    6 Unawaangamiza wasemao uongo.

    Bwana huwachukia

    wamwagao damu na wadanganyifu.

  17. 1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli.

  18. 11 “ ‘Usiibe.

    “ ‘Usiseme uongo.

    “ ‘Msidanganyane.

    12 “ ‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Bwana.

  19. 1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji

    na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!

    Ningelia usiku na mchana

    kwa kuuawa kwa watu wangu.

    2 Laiti ningekuwa na nyumba

    ya kukaa wasafiri jangwani,

    ningewaacha watu wangu

    na kwenda mbali nao,

    kwa kuwa wote ni wazinzi,

    kundi la watu wadanganyifu.

    3 “Huweka tayari ndimi zao kama upinde,

    ili kurusha uongo;

    wamekuwa na nguvu katika nchi

    lakini si katika ukweli.

    Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,

    hawanitambui mimi,”

    asema Bwana.

    4 “Jihadhari na rafiki zako;

    usiwaamini ndugu zako.

    Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,

    na kila rafiki ni msingiziaji.

    5 Rafiki humdanganya rafiki,

    hakuna yeyote asemaye kweli.

    Wamefundisha ndimi zao kudanganya,

    wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.

    6 Unakaa katikati ya udanganyifu;

    katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,”

    asema Bwana.

    7 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote:

    “Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,

    kwani ni nini kingine niwezacho kufanya

    kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?

    8 Ndimi zao ni mshale wenye sumu,

    hunena kwa udanganyifu.

    Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,

    lakini moyoni mwake humtegea mtego.

    9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”

    asema Bwana.

    “Je, nisijilipizie kisasi

    kwa taifa kama hili?”

  20. 19 Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika. 20 Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.

    22 Basi kuweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo 24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo. 25 Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.

    26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu. 27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

  21. 12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa. 13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema.

  22. 3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Bwana?

    Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake?

    4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe,

    yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake

    au kuapa kwa kitu cha uongo.

    5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Bwana,

    na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake.

  23. 1 Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2 Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.

    3 Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

    5 Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6 Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.

    7 Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8 Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”

    9 Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”

    10 Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. 11 Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.

  24. 10 Kwa maana,

    “Yeyote apendaye uzima

    na kuona siku njema,

    basi auzuie ulimi wake usinene mabaya,

    na midomo yake isiseme hila.

    11 Mtu huyo lazima aache uovu, akatende mema;

    lazima aitafute amani na kuifuatilia sana.

    12 Kwa maana macho ya Bwana

    huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini

    kusikiliza maombi yao.

    Bali uso wa Bwana uko kinyume

    na watendao maovu.”

  25. Wimbo wa kwenda juu.

    1 Katika dhiki yangu namwita Bwana,

    naye hunijibu.

    2 Ee Bwana, uniokoe kutoka midomo ya uongo

    na ndimi za udanganyifu.

    3 Atakufanyia nini,

    au akufanyie nini zaidi, ewe ulimi mdanganyifu?

    4 Atakuadhibu kwa mishale mikali ya shujaa,

    kwa makaa yanayowaka ya mti wa mretemu.

  26. 20 Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 Kwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23 Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

  27. 12 Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. 13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

  28. 14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake. 15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.

  29. Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.”

    1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?

    Kwa nini unajivuna mchana kutwa,

    wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?

    2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi.

    Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.

    3 Unapenda mabaya kuliko mema,

    uongo kuliko kusema kweli.

    4 Unapenda kila neno lenye kudhuru,

    ewe ulimi wenye hila!

    5 Hakika Mungu atakushusha chini

    kwa maangamizi ya milele:

    atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu

    kutoka hema yako,

    atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai.

  30. 17 Ndugu zangu, nawasihi mjihadhari na kujiepusha na wale watu waletao matengano na kuweka vikwazo mbele yenu dhidi ya mafundisho mliyojifunza. 18 Kwa maana watu kama hao hawamtumikii Bwana Kristo, bali wanatumikia tamaa zao wenyewe. Kwa kutumia maneno laini na ya kubembeleza, hupotosha mioyo ya watu wajinga. 19 Kila mtu amesikia juu ya utii wenu, nami nimejawa na furaha tele kwa ajili yenu. Lakini nataka mwe na hekima katika mambo mema na bila hatia katika mambo maovu.

    20 Mungu wa amani atamponda Shetani chini ya miguu yenu upesi.

    Neema ya Bwana wetu Yesu iwe nanyi. Amen.

  31. 2 “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu,

    Mwenyezi ambaye amenifanya

    nionje uchungu wa nafsi,

    3 kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu,

    nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,

    4 midomo yangu haitanena uovu,

    wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.

    5 Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi;

    hadi nife, sitakana uadilifu wangu.

  32. 1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna.

  33. 7 Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho;

    shida na ubaya viko chini ya ulimi wake.

  34. 5 Shahidi mwaminifu hadanganyi,

    bali shahidi wa uongo humimina uongo.

  35. 25 Shahidi wa kweli huokoa maisha,

    bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu.

  36. 17 Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu,

    bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.

  37. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

    23 Lakini wewe, Ee Mungu,

    utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.

    Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,

    hawataishi nusu ya siku zao.

    Lakini mimi ninakutumaini wewe.

  38. 5 Mipango ya mtu mwadilifu ni ya haki,

    bali ushauri wa mwovu ni udanganyifu.

  39. 27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu yeyote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

  40. 20 Naye Bwana akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’

    “Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile. 21 Mwishoni, pepo mchafu akajitokeza, akasimama mbele za Bwana na kusema, ‘Nitamshawishi.’

    22 “Bwana akauliza, ‘Kwa njia gani?’

    “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’

    “Bwana akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’

    23 “Kwa hiyo sasa Bwana ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Bwana ameamuru maafa kwa ajili yako.”

  41. 9 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

    naye amwagaye uongo ataangamia.

  42. 13 Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa;

    hawatasema uongo,

    wala udanganyifu hautakuwa

    katika vinywa vyao.

    Watakula na kulala

    wala hakuna yeyote

    atakayewaogopesha.”

  43. 6 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa maneno matupu, kwa kuwa hasira ya Mungu huwaka kwa sababu ya mambo kama haya juu ya wale wasiomtii. 7 Kwa hiyo, msishirikiane nao.

  44. 1 Ee Mungu unihukumu,

    nitetee dhidi ya taifa lisilomcha Mungu,

    niokoe na watu wadanganyifu na waovu.

  45. 23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. 24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.

    26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

  46. 10 Kama ilivyoandikwa:

    “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.

    11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,

    hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.

    12 Wote wamepotoka,

    wote wameoza pamoja;

    hakuna atendaye mema,

    naam, hakuna hata mmoja.”

    13 “Makoo yao ni makaburi wazi;

    kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.”

    “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”

  47. 22 “Yeye hakutenda dhambi,

    wala hila haikuonekana kinywani mwake.”

  48. 10 Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu,

    hazina yako uliyopata kwa udanganyifu

    na vipimo vilivyopunguka,

    ambavyo vimelaaniwa?

    11 Je, naweza kuhukumu kuwa

    mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia,

    aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?

    12 Matajiri wake ni wajeuri;

    watu wake ni waongo

    na ndimi zao zinazungumza

    kwa udanganyifu.

    13 Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu,

    kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.

  49. 11 Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

    14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

  50. 22 Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedha na mivao miwili ya mavazi.’ ”

    23 Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mivao miwili ya mavazi. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi. 24 Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka. 25 Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Elisha bwana wake.

    Elisha akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?”

    Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakwenda popote.”

    26 Lakini Elisha akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka kwenye gari lake ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ngʼombe, au watumishi wa kiume na wa kike? 27 Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Elisha, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.

  51. 28 Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu,

    au kutumia midomo yako kudanganya.

  52. 28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

  53. 3 Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,

    ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema.

  54. 6 Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo

    ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha.

  55. 1 Nataka mjue jinsi ninavyojitaabisha kwa ajili yenu na kwa ajili ya wale walioko Laodikia, na pia kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona mimi binafsi. 2 Kusudi langu ni watiwe moyo na kuunganishwa katika upendo, ili wapate ule utajiri wa ufahamu mkamilifu, ili waijue siri ya Mungu, yaani, Kristo mwenyewe, 3 ambaye ndani yake kumefichwa hazina zote za hekima na maarifa. 4 Nawaambia mambo haya ili mtu yeyote asiwadanganye kwa maneno ya kuwashawishi. 5 Kwa kuwa ingawa mimi siko pamoja nanyi kimwili, lakini niko pamoja nanyi kiroho, nami nafurahi kuuona utaratibu wenu na jinsi uthabiti wa imani yenu katika Kristo ulivyo.

    6 Hivyo basi, kama vile mlivyompokea Kristo Yesu kuwa Bwana, endeleeni kukaa ndani yake, 7 mkiwa na mizizi, na mmejengwa ndani yake, mkiimarishwa katika imani kama mlivyofundishwa, na kufurika kwa wingi wa shukrani.

    8 Angalieni mtu yeyote asiwafanye ninyi mateka kwa elimu batili na madanganyo matupu yanayotegemea mapokeo ya wanadamu na mafundisho ya ulimwengu badala ya Kristo.

    9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka. 11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, 12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.

    13 Mlipokuwa wafu katika dhambi zenu na kutokutahiriwa katika asili yenu ya dhambi, Mungu aliwafanya mwe hai pamoja na Kristo. Alitusamehe dhambi zetu zote, 14 akiisha kuifuta ile hati yenye mashtaka yaliyokuwa yanatukabili, pamoja na maagizo yake. Aliiondoa isiwepo tena, akiigongomea kwenye msalaba wake. 15 Mungu akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuziburura kwa ujasiri, akizishinda katika msalaba wa Kristo.

  56. 11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,

    nitawafundisha kumcha Bwana.

    12 Yeyote kati yenu anayependa uzima

    na kutamani kuziona siku nyingi njema,

    13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,

    na midomo yake kutokana na kusema uongo.

    14 Aache uovu, atende mema,

    aitafute amani na kuifuatilia.

    15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,

    na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.

  57. 3 Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao,

    toka tumboni mwa mama zao

    ni wakaidi na husema uongo.

  58. 1 Hakika mkono wa Bwana si mfupi hata usiweze kuokoa,

    wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia.

    2 Lakini maovu yenu yamewatenga

    ninyi na Mungu wenu,

    dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake,

    ili asisikie.

    3 Kwa maana mikono yenu imetiwa mawaa kwa damu

    na vidole vyenu kwa hatia.

    Midomo yenu imenena uongo,

    nazo ndimi zenu zimenongʼona mambo maovu.

    4 Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki;

    hakuna hata mmoja anayetetea shauri lake kwa haki.

    Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo,

    huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu.

  59. 14 Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwaweka, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu, na madanganyo ya mawazo yao wenyewe.

  60. 1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. 2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. 4 Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi. 5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.”

  61. 18 Akamwendea baba yake akasema, “Baba yangu.”

    Akajibu, “Naam, mwanangu, wewe ni nani?”

    19 Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili uweze kunibariki.”

  62. 35 Hutunga mimba ya madhara na kuzaa uovu;

    matumbo yao huumba udanganyifu.”

  63. 27 Kama vitundu vilivyojaa ndege,

    nyumba zao zimejaa udanganyifu;

    wamekuwa matajiri na wenye nguvu,

    28 wamenenepa na kunawiri.

    Matendo yao maovu hayana kikomo;

    hawatetei mashauri ya yatima wapate kushinda,

    hawatetei haki za maskini.

  64. 20 Hawazungumzi kwa amani,

    bali wanatunga mashtaka ya uongo

    dhidi ya wale wanaoishi

    kwa utulivu katika nchi.

  65. 8 Hekima ya mwenye busara ni kufikiria njia zake,

    bali upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.

  66. 4 Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya;

    mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.

  67. 7 Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametokea ulimwenguni. Mtu wa namna hiyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo.

  68. 2 Heri mtu yule ambaye Bwana

    hamhesabii dhambi,

    na ambaye rohoni mwake

    hamna udanganyifu.

  69. 3 Mtamshambulia mtu hata lini?

    Je, ninyi nyote mtamtupa chini,

    ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika?

    4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha

    toka mahali pake pa fahari;

    wanafurahia uongo.

    Kwa vinywa vyao hubariki,

    lakini ndani ya mioyo yao hulaani.

  70. 18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,

    na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.

    19 Wakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani,

    lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.

  71. 18 Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu,

    bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika.

  72. 5 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

    naye amwagaye uongo hataachwa huru.

  73. 9 Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu,

    pamoja na matajiri katika kifo chake,

    ingawa hakutenda jeuri,

    wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

  74. 6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu.

  75. 7 Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyangʼanywa? 8 Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.

    9 Je, hamjui kwamba wasio haki hawataurithi Ufalme wa Mungu? Msidanganyike: Waasherati, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wahanithi, wala walawiti, 10 wala wezi, wala wenye tamaa mbaya, wala walevi, wala wanaodhihaki, wala wanyangʼanyi hawataurithi Ufalme wa Mungu. 11 Baadhi yenu mlikuwa kama hao. Lakini mlioshwa, mlitakaswa, mlihesabiwa haki kwa jina la Bwana Yesu Kristo na katika Roho wa Mungu wetu.

  76. 1 Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi, 2 msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho wala neno au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, isemayo kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwako. 3 Mtu yeyote na asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. 4 Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.

  77. 9 Kisha Bwana akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?”

    Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”

  78. 10 Basi kulikuwako na njaa katika nchi, naye Abramu akashuka kwenda Misri kukaa huko kwa muda, kwa maana njaa ilikuwa kali. 11 Alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, “Ninajua ya kwamba wewe ni mwanamke mzuri wa sura. 12 Wakati Wamisri watakapokuona, watasema, ‘Huyu ni mke wake.’ Ndipo wataniua, lakini wewe watakuacha hai. 13 Sema wewe ni dada yangu, ili nitendewe mema kwa ajili yako, na maisha yangu yatahifadhiwa kwa sababu yako.”

  79. 19 Mungu si mtu, hata aseme uongo,

    wala yeye si mwanadamu, hata ajute.

    Je, anasema, kisha asitende?

    Je, anaahidi, asitimize?

  80. 29 Niepushe na njia za udanganyifu,

    kwa neema unifundishe sheria zako.

    30 Nimechagua njia ya kweli,

    nimekaza moyo wangu katika sheria zako.

  81. 118 Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako,

    kwa maana udanganyifu wao ni bure.

  82. 5 Mwenye haki huchukia uongo,

    bali waovu huleta aibu na fedheha.

  83. 7 Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu:

    je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala!

  84. 8 Uutenge mbali nami udanganyifu na uongo;

    usinipe umaskini wala utajiri,

    bali unipe chakula cha kunitosha kila siku.

    9 Nisije nikawa na vingi vya kuzidi nikakukana

    na kusema, ‘Bwana ni nani?’

    Au nisije nikawa maskini nikaiba,

    nami nikaliaibisha jina la Mungu wangu.

  85. 4 Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ nao watawadanganya wengi.

  86. 13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

  87. 7 Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

  88. 9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

  89. 11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka dunia. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka. 12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akawafanya wote wakaao duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. 13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi. 14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya wakaao duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi. 15 Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa.

  90. 6 Hivyo Isaki akaishi huko Gerari.

    7 Watu wa mahali pale walipomuuliza habari za mke wake, akasema, “Huyu ni dada yangu,” kwa sababu aliogopa kusema, “Huyu ni mke wangu.” Alifikiri, “Watu wa mahali pale wataweza kumuua kwa sababu ya Rebeka, kwa kuwa alikuwa mzuri wa sura.”

    8 Wakati Isaki alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki mfalme wa Wafilisti akachungulia dirishani, akaona jinsi Isaki alivyomkumbatia Rebeka mke wake. 9 Abimeleki akamwita Isaki akamwambia, “Hakika huyu ni mke wako! Mbona uliniambia, ‘Huyu ni dada yangu?’ ”

    Isaki akamjibu, “Kwa sababu nilifikiri ningeweza kuuawa kwa sababu yake.”

    10 Ndipo Abimeleki akamjibu, “Ni nini hiki ulichotufanyia? Ingewezekana mtu yeyote akawa amekutana kimwili na mke wako, nawe ungeleta hatia juu yetu.”

  91. 163 Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo,

    lakini napenda sheria yako.

  92. 6 Maono yao ni ya uongo na ubashiri wao ni wa udanganyifu. Wao husema, “Bwana amesema,” wakati Bwana hakuwatuma, bado wakitarajia maneno yao kutimizwa. 7 Je, hamjaona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu hapo msemapo, “Bwana asema,” lakini Mimi sijasema?

    8 “ ‘Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ya uongo wa maneno yenu na kwa madanganyo ya maono yenu, Mimi ni kinyume na ninyi, asema Bwana Mwenyezi. 9 Mkono wangu utakuwa dhidi ya manabii ambao huona maono ya uongo na kusema ubashiri wa udanganyifu. Hawatakuwa katika baraza la watu wangu au kuandikwa katika kumbukumbu ya nyumba ya Israeli wala hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mwenyezi.

  93. 1 Sikieni neno la Bwana, enyi Waisraeli,

    kwa sababu Bwana analo shtaka

    dhidi yenu ninyi mnaoishi katika nchi:

    “Hakuna uaminifu, hakuna upendo,

    hakuna kumjua Mungu katika nchi.

    2 Kuna kulaani tu, uongo na uuaji,

    wizi na uzinzi,

    bila kuwa na mipaka,

    nao umwagaji damu mmoja

    baada ya mwingine.

  94. 1 Ole wa mji umwagao damu,

    uliojaa uongo,

    umejaa nyara,

    usiokosa kuwa na vitu vya kuteka nyara.

  95. 31 Kisha wakalichukua lile joho la Yosefu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. 32 Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”

    33 Baba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yosefu ameraruliwa vipande vipande.”

    34 Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. 35 Wanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.

  96. 20 Usimshuhudie jirani yako uongo.

  97. 16 Haya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu, 17 usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia yote haya,” asema Bwana.

  98. 15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali. 16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma? 17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.

    21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

    24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

  99. 18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

  100. 13 Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. 14 Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. 15 Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako. 16 Kwa maana Bwana Mungu wako humchukia yeyote ambaye hufanya mambo kama haya, yeyote anayetenda kwa udanganyifu.

  101. 33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.”