40 Bible Verses About Identity in Christ

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Identity in Christ
  1. 1 Kwa habari zenu, mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuatisha namna ya ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulikuwa wana wa ghadhabu, kama mtu mwingine yeyote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Kristo Yesu, 7 ili katika ule ulimwengu ujao apate kuonyesha wingi wa neema yake isiyopimika, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Kristo Yesu. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala si kwa matendo yenu mema. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Kristo Yesu, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.

  2. 14 Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa. 15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.

    16 Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Kristo kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

  3. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki sisi kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani ya Kristo. 4 Kwa maana alituchagua katika yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake. Kwa upendo 5 alitangulia kutuchagua tuwe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo kwa furaha yake na mapenzi yake mwenyewe. 6 Kwa hiyo tunamsifu Mungu kwa huruma zake kuu alizotumiminia sisi katika Mwanawe Mpendwa. 7 Ndani yake tunao ukombozi kwa njia ya damu yake, yaani, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake 8 aliyotumiminia kwa wingi, kwa hekima yote na maarifa yote. 9 Naye alitujulisha siri ya mapenzi yake sawasawa na uradhi wa mapenzi yake, ambayo alikusudia katika Kristo, 10 ili yapate kutimizwa wakati mkamilifu utakapowadia, yaani, kuvitia vitu vyote vya mbinguni na vya duniani pamoja, chini ya kiongozi mmoja, ndiye Kristo.

    11 Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na kusudi la mapenzi yake, 12 ili kwamba, sisi tuliokuwa wa kwanza kuweka tumaini katika Kristo, tupate kuishi kwa sifa ya utukufu wake. 13 Ninyi pia mliingia ndani ya Kristo mliposikia Neno la kweli, Injili ya wokovu wenu. Mkiisha kuamini, ndani yake mlitiwa muhuri, yaani, Roho Mtakatifu mliyeahidiwa, 14 yeye ambaye ni amana yetu akituhakikishia urithi wetu hadi ukombozi wa wale walio milki ya Mungu kwa sifa ya utukufu wake.

  4. 9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

  5. 26 Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

  6. 1 Tazameni ni pendo kuu namna gani alilotupa Baba, kwamba sisi tuitwe wana wa Mungu! Na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. 2 Wapendwa, sasa tu wana wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo. 3 Kila mmoja mwenye matumaini haya ndani yake hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.

  7. 19 Je, hamjui ya kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, 20 kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.

  8. 1 Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo alikoketi mkono wa kuume wa Mungu. 2 Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3 Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4 Wakati Kristo, aliye uzima wenu, atakapotokea, ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.

  9. 11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.

  10. 14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 15 Siwaiti ninyi watumishi tena, kwa sababu watumishi hawajui bwana wao analofanya, bali nimewaita ninyi rafiki, kwa maana nimewajulisha mambo yote niliyoyasikia kutoka kwa Baba yangu. 16 Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kudumu. Ili nalo lolote mtakalomwomba Baba katika Jina langu, awape ninyi.

  11. 17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

    20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

    25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27 wala msimpe ibilisi nafasi. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

    29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

  12. 20 Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

  13. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  14. 9 Maana ukamilifu wote wa Uungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu, 10 nanyi mmepewa ukamilifu ndani ya Kristo, ambaye ndiye mkuu juu ya kila enzi na kila mamlaka. 11 Katika Kristo pia mlitahiriwa kwa kutengwa mbali na asili ya dhambi, si kwa tohara inayofanywa kwa mikono ya wanadamu, bali kwa ile tohara iliyofanywa na Kristo, 12 mkiwa mmezikwa pamoja naye katika ubatizo, na kufufuliwa pamoja naye kwa njia ya imani yenu katika uweza wa Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu.

  15. 1 Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu ya adhabu kwa wale walio ndani ya Kristo Yesu, wale ambao hawaenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho. 2 Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti. 3 Kwa maana kile ambacho sheria haikuwa na uwezo wa kufanya, kwa vile ilivyokuwa dhaifu katika mwili, Mungu kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe kwa mfano wa mwanadamu mwenye mwili ulio wa dhambi na kwa ajili ya dhambi, yeye aliihukumu dhambi katika mwili, 4 ili kwamba haki ipatikanayo kwa sheria itimizwe ndani yetu sisi, ambao hatuenendi kwa kuufuata mwili bali kwa kufuata Roho.

    5 Kwa maana wale wanaoishi kwa kuufuata mwili huziweka nia zao katika vitu vya mwili, lakini wale wanaoishi kwa kufuata Roho, huziweka nia zao katika mambo ya Roho. 6 Kwa maana kuwa na nia ya mwili ni mauti, bali kuwa na nia inayoongozwa na Roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui na Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale wanaotawaliwa na mwili, hawawezi kumpendeza Mungu.

    9 Lakini ninyi, hamtawaliwi na mwili, bali na Roho, ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu. Mtu yeyote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo. 10 Lakini kama Kristo anakaa ndani yenu, miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, lakini roho zenu zi hai kwa sababu ya haki. 11 Nanyi ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu kutoka kwa wafu ataihuisha pia miili yenu ambayo hufa, kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu.

    12 Kwa hiyo ndugu zangu, sisi tu wadeni, si wa mwili, ili tuishi kwa kuufuata mwili, 13 kwa maana mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa, lakini kama mkiyaua matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. 14 Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio watoto wa Mungu. 15 Kwa maana hamkupokea roho ya utumwa iwaleteayo tena hofu, bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambaye kwa yeye twalia, “Abba, yaani, Baba,” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

  16. 12 Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo. 13 Kwa maana katika Roho mmoja wote tulibatizwa katika mwili mmoja, kama ni Wayahudi au Wayunani, kama ni watumwa au watu huru, nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

    14 Basi mwili si kiungo kimoja, bali ni viungo vingi. 15 Kama mguu ungesema, “Kwa kuwa mimi si mkono basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya huo mguu usiwe sehemu ya mwili. 16 Na kama sikio lingesema, “Kwa kuwa mimi si jicho, basi mimi si wa mwili,” hiyo isingefanya hilo sikio lisiwe sehemu ya mwili. 17 Kama mwili wote ungelikuwa jicho, kusikia kungekuwa wapi? Au kama mwili wote ungelikuwa sikio, kunusa kungekuwa wapi? 18 Lakini kama ilivyo, Mungu ameweka viungo katika mwili, kila kimoja kama alivyopenda. 19 Kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20 Kama ulivyo, una viungo vingi, lakini mwili ni mmoja.

    21 Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sina haja nawe!” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, “Sina haja na ninyi!” 22 Lakini badala yake, vile viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu, ndivyo ambavyo ni vya muhimu sana. 23 Navyo vile viungo tunavyoviona havina heshima, ndivyo tunavipa heshima maalum. Vile viungo vya mwili ambavyo havina uzuri, tunavipa heshima ya pekee; 24 wakati vile viungo vyenye uzuri havihitaji utunzaji wa pekee. Lakini Mungu ameviweka pamoja viungo vya mwili na akavipa heshima zaidi vile vilivyopungukiwa, 25 ili pasiwe na mafarakano katika mwili, bali viungo vyote vihudumiane kwa usawa kila kimoja na mwenzake. 26 Kama kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia pamoja nacho, kama kiungo kimoja kikipewa heshima, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

    27 Sasa ninyi ni mwili wa Kristo na kila mmoja wenu ni sehemu ya huo mwili. 28 Mungu ameweka katika kanisa, kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu, kisha watenda miujiza, pia karama za kuponya, karama za kusaidiana, karama za uongozi, aina mbalimbali za lugha. 29 Je, wote ni mitume? Je, wote ni manabii? Je, wote ni walimu? Je, wote wanatenda miujiza? 30 Je, wote wana karama ya kuponya? Je, wote hunena kwa lugha mpya? Je, wote wanatafsiri? 31 Basi tamanini sana karama zilizo kuu.

    Nami nitawaonyesha njia iliyo bora zaidi.

  17. 27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe,

    kwa mfano wa Mungu alimuumba;

    mwanaume na mwanamke aliwaumba.

  18. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani;

    uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu.

    14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa

    kwa namna ya ajabu na ya kutisha;

    kazi zako ni za ajabu,

    ninajua hayo kikamilifu.

    15 Umbile langu halikufichika kwako,

    nilipoumbwa mahali pa siri.

    Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi,

    16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika.

    Siku zangu zote ulizonipangia

    ziliandikwa katika kitabu chako

    kabla haijakuwepo hata moja.

  19. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

    9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

  20. 16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa.

  21. 1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Kila tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata, nalo kila tawi lizaalo, hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililonena nanyi. 4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani yangu hamwezi kuzaa matunda.

    5 “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote.

  22. 20 Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, 21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

  23. 13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

    14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

  24. 1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  25. 24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tufe kwa mambo ya dhambi, bali tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa.

  26. 1 Tuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka? 2 La hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi? 3 Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? 4 Kwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.

    5 Kwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake. 6 Kwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi. 7 Kwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

    8 Basi ikiwa tulikufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye. 9 Kwa maana tunajua kwamba Kristo, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake. 10 Kifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.

    11 Vivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu. 12 Kwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 Wala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 Kwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.

    15 Ni nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha! 16 Je, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 Lakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 Nanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

    19 Ninasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa. 20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki. 21 Lakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti. 22 Lakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele. 23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

  27. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  28. 17 Lakini mtu aliyeungwa na Bwana anakuwa roho moja naye.

  29. 2 kwa maana ninyi ni taifa takatifu kwa Bwana Mungu wenu. Bwana amewachagua ninyi kuwa taifa la kipekee kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia, mwe tunu yake.

  30. 7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.

  31. 1 Paulo, niliyeitwa kwa mapenzi ya Mungu kuwa mtume wa Kristo Yesu, na Sosthene ndugu yetu.

    2 Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, kwa wale waliotakaswa katika Kristo Yesu na walioitwa kuwa watakatifu, pamoja na wale wote ambao kila mahali wanaliitia Jina la Kristo Yesu Bwana wetu, aliye Bwana wao na wetu pia:

    3 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.

  32. 26 Ndugu zangu, kumbukeni mlivyokuwa mlipoitwa. Kwa kipimo cha kibinadamu, si wengi wenu mliokuwa na hekima. Si wengi mliokuwa na ushawishi, si wengi mliozaliwa katika jamaa zenye vyeo. 27 Lakini Mungu alivichagua vitu vipumbavu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye hekima, Mungu alivichagua vitu dhaifu vya ulimwengu ili awaaibishe wenye nguvu. 28 Alivichagua vitu vya chini na vinavyodharauliwa vya dunia hii, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko, 29 ili mtu yeyote asijisifu mbele zake. 30 Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanyika kwetu hekima itokayo kwa Mungu, yaani haki, na utakatifu na ukombozi. 31 Hivyo, kama ilivyoandikwa: “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

  33. 14 Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.

  34. 7 Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

  35. 11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba ninyi ambao hapo awali mlikuwa watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu), 12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Kristo, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi mkiwa hamna tumaini wala Mungu duniani. 13 Lakini sasa katika Kristo Yesu, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kwa njia ya damu ya Kristo.

    14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa wawili, yaani, Wayahudi na watu wa Mataifa, tuwe wamoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, 15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, 16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao. 17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu. 18 Kwa maana kwa kupitia kwake, sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

    19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena wala wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni. 21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kusimamishwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Bwana. 22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kwa njia ya Roho wake.

  36. 12 Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri.

  37. 14 Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15 ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16 Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17 ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18 mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19 na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.

  38. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  39. 19 Naye Mungu wangu atawajaza ninyi na kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu.

  40. 21 Hapo kwanza mlikuwa mmetengana na Mungu, na mlikuwa adui zake katika nia zenu kwa sababu ya mienendo yenu mibaya. 22 Lakini sasa Mungu amewapatanisha ninyi kwa njia ya mwili wa Kristo kupitia mauti, ili awalete mbele zake mkiwa watakatifu, bila dosari wala lawama, 23 ikiwa mnaendelea katika imani yenu mkiwa imara na thabiti, pasipo kuliacha tumaini lililoahidiwa katika Injili. Hii ndiyo ile Injili mliyoisikia, ambayo imehubiriwa kwa kila kiumbe chini ya mbingu, na ambayo mimi Paulo nimekuwa mtumwa wake.