28 Bible Verses About Dreams
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
-
11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. 12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.
13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”
14 Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri
-
1 Kama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, 2 ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” 3 kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. Bwana Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. 4 Ni Bwana Mungu wenu ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. 5 Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya Bwana Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo Bwana Mungu wenu aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.
-
1 Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala. 2 Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme, 3 akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.”
4 Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.”
-
3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto wakati wa usiku na kumwambia, “Wewe ni kama mfu kwa sababu ya huyu mwanamke uliyemchukua; yeye ni mke wa mtu.”
4 Wakati huo Abimeleki alikuwa bado hajamsogelea, kwa hiyo akasema, “Je, Bwana utaliharibu taifa lisilo na hatia? 5 Hakusema kwangu, ‘Huyu ni dada yangu,’ naye Sara pia hakusema, ‘Huyu ni kaka yangu’? Nimefanya haya kwa dhamiri njema na mikono safi.”
6 Kisha Mungu akamwambia katika ndoto, “Ndiyo, najua ya kwamba umefanya haya kwa dhamiri safi, kwa hiyo nimekuzuia usinitende dhambi. Ndiyo sababu sikukuacha umguse. 7 Sasa umrudishe huyo mke wa mtu, kwa maana ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini kama hutamrudisha, ujue kwa hakika kuwa wewe na watu wako wote mtakufa.”
-
12 Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine yote ya mashariki walikaa bondeni, nao walikuwa mfano wa nzige kwa wingi wao. Ngamia zao hazikuhesabika, wingi wao ulikuwa kama mchanga wa ufuoni mwa bahari.
13 Gideoni alifika wakati huo huo kukiwa na mtu mmoja aliyekuwa anamweleza mwenzake ndoto yake, akisema, “Niliota ndoto: Tazama mkate wa shayiri ulioviringana ulianguka katika kambi moja ya Wamidiani, ukaipiga na ikaanguka nao ukaipindua juu chini na hema ikaporomoka chini.”
14 Rafiki yake akamjibu, “Habari hii si kitu kingine zaidi ya upanga wa Gideoni mwana wa Yoashi, Mwisraeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote mkononi mwake.”
15 Gideoni alipoisikia hiyo ndoto na tafsiri yake, akamwabudu Mungu. Akarudi kwenye kambi ya Israeli na kusema, “Inukeni! Bwana amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”
-
19 Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri 20 na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”
21 Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli. 22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya,
-
1 Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.
2 Zifuatazo ni habari za Yakobo.
Yosefu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.
3 Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana. 4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.
5 Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. 6 Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”
8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.
9 Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”
10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?” 11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.
-
6 Bwana akasema, “Sikilizeni maneno yangu:
“Akiwapo nabii wa Bwana miongoni mwenu,
nitajifunua kwake kwa maono,
nitanena naye katika ndoto.
-
19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.
20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”
24 Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake.
-
12 Akaota ndoto ambayo aliona ngazi imesimamishwa juu ya ardhi, ncha yake ikiwa imefika mbinguni na malaika wa Mungu wakawa wakipanda na kushuka juu yake. 13 Juu yake alisimama Bwana, akasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wa baba yako Abrahamu na Mungu wa Isaki. Nchi ambayo umelala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako. 14 Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi na mashariki, kaskazini na kusini. Kupitia wewe na uzao wako mataifa yote ya duniani yatabarikiwa. 15 Niko pamoja nawe nami nitakulinda kila uendako na nitakurudisha katika nchi hii. Sitakuacha mpaka nitakapofanya hayo niliyokuahidi.”
16 Yakobo alipoamka kutoka usingizini, akawaza, “Hakika Bwana yuko mahali hapa, wala mimi sikujua.” 17 Kwa hiyo akaogopa, akasema, “Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka hapa ndipo nyumba ya Mungu ilipo, hili ni lango la mbinguni.”
-
14 Kwa kuwa Mungu husema, wakati huu kwa njia moja,
au wakati mwingine kwa njia nyingine,
ingawa mwanadamu anaweza asielewe.
15 Mungu husema na mwanadamu katika ndoto,
katika maono ya usiku,
wakati usingizi mzito uwaangukiapo
wanadamu wasinziapo vitandani mwao,
16 anaweza akasemea masikioni mwao,
na kuwatia hofu kwa maonyo,
17 ili kumgeuza mtu kutoka kwenye kutenda mabaya
na kumwepusha na kiburi,
18 kuiokoa nafsi yake na shimo,
uhai wake usiangamizwe kwa upanga.
-
26 Mfalme akamuuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?”
27 Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza, 28 lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita mawazoni mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya:
-
28 “Hata itakuwa, baada ya hayo,
nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.
29 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu.
30 Nami nitaonyesha maajabu katika mbingu
na duniani:
damu, moto na mawimbi ya moshi.
31 Jua litageuzwa kuwa giza
na mwezi kuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ya Bwana
ile kuu na ya kutisha.
-
8 Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu yeyote wa kuzifasiri.”
Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”
-
24 Ndipo Mungu akamjia Labani Mwaramu katika ndoto usiku na kumwambia, “Jihadhari usiseme neno lolote kwa Yakobo, liwe zuri au baya.”
-
25 “Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’ 26 Mambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe? 27 Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau jina langu kwa kumwabudu Baali. 28 Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Bwana.
-
19 Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni, 20 na akasema:
“Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele;
hekima na uweza ni vyake.
21 Yeye hubadili nyakati na majira;
huwaweka wafalme na kuwaondoa.
Huwapa hekima wenye hekima,
na maarifa wenye ufahamu.
22 Hufunua siri na mambo yaliyofichika;
anajua yale yaliyo gizani,
nayo nuru hukaa kwake.
23 Ninakushukuru na kukuhimidi,
Ee Mungu wa baba zangu:
Umenipa hekima na uwezo,
umenijulisha kile tulichokuomba,
umetujulisha ndoto ya mfalme.”
-
10 “Wakati fulani majira ya kuzaliana niliota ndoto ambayo niliinua macho na kuona kwamba wale mabeberu waliokuwa wakipanda kundi walikuwa wa mistari, madoadoa na mabakabaka. 11 Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, ‘Yakobo.’ Nikamjibu, ‘Mimi hapa.’ 12 Akasema, ‘Inua macho yako uone wale mabeberu wote wanaopanda kundi wana mistari, madoadoa au mabakabaka, kwa maana nimeona yale yote ambayo Labani amekuwa akikutendea. 13 Mimi ndiye Mungu wa Betheli, ulikomiminia ile nguzo mafuta na pale mahali uliponiwekea nadhiri. Sasa ondoka katika nchi hii mara moja urudi katika nchi uliyozaliwa.’ ”
-
5 macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi,
nayo furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kwa kitambo tu.
6 Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni
na kichwa chake hugusa mawingu,
7 ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe.
Wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’
8 Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena,
amefukuziwa mbali kama maono ya usiku.
-
5 Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”
-
9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10 Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.
-
17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.
-
16 Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yosefu amefasiri ikiwa na maana nzuri, akamwambia Yosefu, “Mimi pia niliota ndoto: Kichwani mwangu kulikuwepo vikapu vitatu vya mikate. 17 Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kwenye kikapu nilichokuwa nimebeba kichwani.”
18 Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. 19 Katika siku hizi tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”
-
25 Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 26 Ngʼombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja. 27 Ngʼombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa.
28 “Ni kama vile nilivyomwambia Farao: Mungu amemwonyesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni. 29 Miaka saba ya neema inakuja katika nchi yote ya Misri, 30 lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo neema yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.
31 “Neema iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno.
-
9 Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, 10 nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. 11 Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”
12 Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. 13 Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake.
-
8 Asubuhi yake, alifadhaika akilini, hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.
9 Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu. 10 Wakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi. 11 Kila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti. 12 Basi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake.
-
15 Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.”
16 Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”
-
10 Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”
Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”
11 Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”
Shows Read in context, Share and Copy.