51 Bible Verses About Overcoming Hard Times

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Bible Verses About Overcoming Hard Times
  1. 4 Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema furahini! 5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu. 6 Msijisumbue kwa jambo lolote, bali katika kila jambo kwa kuomba na kusihi pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. 7 Nayo amani ya Mungu, inayopita fahamu zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.

    8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo na sifa njema, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote ya kupendeza, yoyote yenye staha, ukiwepo uzuri wowote, pakiwepo chochote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. 9 Mambo yote mliyojifunza au kuyapokea au kuyasikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatendeni hayo. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.

  2. 6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana na mambo yenu.

    8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi huzungukazunguka kama simba angurumaye akitafuta mtu ili apate kummeza. 9 Mpingeni, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso kama hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

    10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawarejesha na kuwatia nguvu, akiwaimarisha na kuwathibitisha.

  3. 10 Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe;

    usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako.

    Nitakutia nguvu na kukusaidia;

    nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

    11 “Wote walioona hasira dhidi yako

    hakika wataaibika na kutahayarika,

    wale wakupingao

    watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia.

    12 Ingawa utawatafuta adui zako,

    hutawaona.

    Wale wanaopigana vita dhidi yako

    watakuwa kama vile si kitu kabisa.

    13 Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    nikushikaye mkono wako wa kuume

    na kukuambia, Usiwe na hofu,

    nitakusaidia.

  4. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”

    7 Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”

  5. 28 Je wewe, hufahamu?

    Je wewe, hujasikia?

    Bwana ni Mungu wa milele,

    Muumba wa miisho ya dunia.

    Hatachoka wala kulegea,

    wala hakuna hata mmoja

    awezaye kuupima ufahamu wake.

    29 Huwapa nguvu waliolegea

    na huongeza nguvu za wadhaifu.

    30 Hata vijana huchoka na kulegea,

    nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,

    31 bali wale wamtumainio Bwana

    atafanya upya nguvu zao.

    Watapaa juu kwa mbawa kama tai;

    watapiga mbio wala hawatachoka,

    watatembea kwa miguu wala hawatazimia.

  6. 6 “Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

  7. 2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali, 3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. 4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.

  8. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.

    28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru.

    “Haya inukeni; twendeni zetu.

  9. 7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

  10. Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.

    1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,

    msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.

    2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa

    nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.

    3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,

    milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.

  11. 33 Nimewaambia mambo haya, ili mpate kuwa na amani mkiwa ndani yangu. Ulimwenguni mtapata dhiki. Lakini jipeni moyo, kwa maana mimi nimeushinda ulimwengu.”

  12. 11 Sisemi hivyo kwa vile nina mahitaji, la! Kwa maana nimejifunza kuridhika katika hali yoyote. 12 Ninajua kupungukiwa, pia ninajua kuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuridhika katika kila hali, wakati wa kushiba na wakati wa kuona njaa, wakati wa kuwa na vingi na wakati wa kupungukiwa. 13 Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

  13. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

  14. 3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo.

  15. 11 Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,” asema Bwana, “ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo. 12 Kisha mtaniita, na mtakuja na kuniomba, nami nitawasikiliza. 13 Mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.

  16. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, ni shida au taabu au mateso au njaa au uchi au hatari au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa:

    “Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

    tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.”

    37 Lakini katika mambo haya yote tunashinda, naam na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kujua kwa hakika ya kuwa sio mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuja, wala wenye uwezo, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine chochote zitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

  17. 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote

    wala usizitegemee akili zako mwenyewe;

    6 katika njia zako zote mkiri yeye,

    naye atayanyoosha mapito yako.

  18. 28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

  19. 1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana,

    yeye aliyekuumba, ee Yakobo,

    yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:

    “Usiogope kwa maana nimekukomboa,

    nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.

    2 Unapopita kwenye maji makuu,

    nitakuwa pamoja nawe,

    unapopita katika mito ya maji,

    hayatakugharikisha.

    Utakapopita katika moto,

    hutaungua,

    miali ya moto haitakuunguza.

    3 Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,

    yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.

    Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,

    Kushi na Seba badala yako.

  20. 12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.

  21. 22 Yesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu.

  22. 3 Utamlinda katika amani kamilifu

    yeye ambaye moyo wake ni thabiti

    kwa sababu anakutumaini wewe.

    4 Mtumaini Bwana milele,

    kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

  23. 28 Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

  24. 17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,

    huwaokoa katika taabu zao zote.

    18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,

    na huwaokoa waliopondeka roho.

    19 Mwenye haki ana mateso mengi,

    lakini Bwana humwokoa nayo yote,

  25. 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kwamba sisi tu watoto wa Mungu. 17 Hivyo, ikiwa sisi ni watoto, basi tu warithi, warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja naye tupate pia kutukuzwa pamoja naye.

    18 Nayahesabu mateso yetu ya wakati huu kuwa si kitu kulinganisha na utukufu utakaodhihirishwa kwetu.

  26. 4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.

  27. 5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema:

    “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana,

    wala usikate tamaa akikukemea,

    6 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao,

    na humwadhibu kila mmoja

    anayemkubali kuwa mwana.”

  28. Zaburi ya Daudi.

    1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,

    nimwogope nani?

    Bwana ni ngome ya uzima wangu,

    nimhofu nani?

    2 Waovu watakaposogea dhidi yangu

    ili wanile nyama yangu,

    adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia,

    watajikwaa na kuanguka.

    3 Hata jeshi linizunguke pande zote,

    moyo wangu hautaogopa;

    hata vita vitokee dhidi yangu,

    hata hapo nitakuwa na ujasiri.

  29. 15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

    16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

  30. 6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe

    wakati unapopatikana,

    hakika maji makuu yatakapofurika

    hayatamfikia yeye.

    7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,

    utaniepusha na taabu

    na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.

    8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;

    nitakushauri na kukuangalia.

  31. 6 Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana juu ya kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe na binti zake. Lakini Daudi akajitia nguvu katika Bwana, Mungu wake.

  32. 9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa,

    ni ngome imara wakati wa shida.

    10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe,

    kwa maana wewe Bwana,

    hujawaacha kamwe wakutafutao.

  33. 1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,

    atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

    2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

    Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”

    3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,

    na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

    4 Atakufunika kwa manyoya yake,

    chini ya mbawa zake utapata kimbilio,

    uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

  34. 21 Hivyo watu hawa, walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba na nguo zao nyingine. 22 Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru ilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. 23 Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana.

    24 Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?”

    Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.”

    25 Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto, hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.”

    26 Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!”

    Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto.

  35. 31 Tuseme nini basi kuhusu haya? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, ni nani awezaye kuwa kinyume chetu?

  36. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi.

  37. 1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwenu. 2 Ombeni pia ili tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si wote wanaoamini. 3 Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu. 4 Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza. 5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.

  38. 12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. 13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

    14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. 15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. 16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

  39. 1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu. 2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. 3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.

  40. 4 Inuka, suala hili lipo mikononi mwako. Sisi tutaungana nawe, uwe na ujasiri ukatende hili.”

  41. 4 Hata kama nikipita katikati

    ya bonde la uvuli wa mauti,

    sitaogopa mabaya,

    kwa maana wewe upo pamoja nami;

    fimbo yako na mkongojo wako

    vyanifariji.

  42. 4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,

    akaniokoa kwenye hofu zangu zote.

    5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,

    nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.

    6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,

    akamwokoa katika taabu zake zote.

    7 Malaika wa Bwana hufanya kituo

    akiwazunguka wale wamchao,

    naye huwaokoa.

    8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,

    heri mtu yule anayemkimbilia.

    9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,

    kwa maana wale wamchao

    hawapungukiwi na chochote.

    10 Wana simba wenye nguvu

    hutindikiwa na kuona njaa,

    bali wale wamtafutao Bwana

    hawatakosa kitu chochote kilicho chema.

  43. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako,

    naye atakutegemeza,

    hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

  44. 13 Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu;

    furahi, ee dunia;

    pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima!

    Kwa maana Bwana anawafariji watu wake,

    naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.

  45. 7 Bwana ni Mwema,

    kimbilio wakati wa taabu.

    Huwatunza wale wanaomtegemea,

  46. 11 Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”

  47. 13 Hakuna jaribu lolote lililowapata ambalo si la kawaida kwa wanadamu. Naye Mungu ni mwaminifu; hataruhusu mjaribiwe kupita mnavyoweza. Lakini mnapojaribiwa atawapa njia ya kutokea ili mweze kustahimili.

  48. 8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. 9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa. 11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.

  49. 17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba.

  50. 23 Tushike kwa uthabiti lile tumaini la ukiri wetu bila kuyumbayumba, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.

  51. 4 Watoto wapendwa, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.