Daudi katika Jangwa la Zifu na Maoni
1059 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
13 Basi Daudi na watu wake, wapatao 600, wakaondoka Keila wakawa wanakwenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakwenda huko.
14 Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwake.
15 Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. 16 Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. 17 Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” 18 Wote wawili wakaweka agano mbele za Bwana. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.
19 Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni? 20 Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.”
21 Sauli akajibu, “Bwana awabariki kwa kunifikiria. 22 Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali ambapo Daudi huenda mara kwa mara na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mwerevu sana. 23 Jueni kila mahali anapojificha mrudi na kunipa taarifa kamili. Kisha nitakwenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.”
Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za uimbaji. Utenzi wa Daudi. Wakati Wazifu walimwendea Sauli na kumjulisha, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu?”
1 Ee Mungu uniokoe kwa jina lako,
unifanyie hukumu kwa uwezo wako.
2 Ee Mungu, sikia maombi yangu,
usikilize maneno ya kinywa changu.
3 Wageni wananishambulia,
watu wakatili wanayatafuta maisha yangu,
watu wasiomjali Mungu.
4 Hakika Mungu ni msaada wangu,
Bwana ndiye anayenitegemeza.
5 Mabaya na yawarudie wale wanaonisingizia,
kwa uaminifu wako uwaangamize.
6 Nitakutolea dhabihu za hiari;
Ee Bwana, nitalisifu jina lako
kwa kuwa ni vyema.
7 Kwa maana ameniokoa katika shida zangu zote,
na macho yangu yamewatazama adui zangu kwa ushindi.
24 Basi wakaondoka na kwenda mpaka Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni. 25 Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka mpaka mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi.
26 Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Wakati Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, 27 mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.” 28 Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi.