Daudi huko En-Gedi
1058 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
29 Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.
24:1 Baada ya Sauli kurudi kuwafuatia Wafilisti, akaambiwa kwamba, “Daudi yuko katika Jangwa la En-Gedi.” 2 Basi Sauli akachukua watu hodari 3,000 kutoka Israeli yote kwenda kumsaka Daudi na watu wake karibu na Majabali ya Mbuzi-Mwitu.
3 Akaja mpaka kwenye mazizi ya kondoo kando ya njia, hapo palikuwa na pango, na Sauli akaingia ndani kujipumzisha. Daudi na watu wake walikuwa wamo mle pangoni kwa ndani zaidi. 4 Watu wa Daudi wakasema, “Hii ndiyo siku aliyonena Bwana akikuambia, ‘Nitamtia adui yako mikononi mwako ili wewe umtendee utakavyo.’ ” Basi Daudi akanyemelea bila kuonekana na kukata upindo wa joho la Sauli.
5 Baada ya hilo, dhamiri ya Daudi ikataabika kwa kukata upindo wa joho la Sauli. 6 Akawaambia watu wake, “Bwana na apishie mbali nisije nikafanya jambo kama hilo kwa bwana wangu, yeye ambaye ni mpakwa mafuta wa Bwana, au kuinua mkono wangu dhidi yake; kwani yeye ni mpakwa mafuta wa Bwana.” 7 Kwa maneno haya Daudi akawaonya watu wake na hakuwaruhusu wamshambulie Sauli. Naye Sauli akaondoka pangoni na kwenda zake.
8 Ndipo Daudi naye akatoka pangoni na kumwita Sauli akisema, “Mfalme, bwana wangu!” Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama na kusujudu uso wake mpaka nchi. 9 Akamwambia Sauli, “Kwa nini unasikiliza wakati watu wanapokuambia, ‘Daudi amenuia kukudhuru’? 10 Leo umeona kwa macho yako mwenyewe jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu huko pangoni. Watu wengine walisisitiza nikuue, lakini nilikuacha, nikisema, ‘Sitainua mkono wangu dhidi ya bwana wangu, kwa sababu yeye ni mpakwa mafuta wa Bwana.’ 11 Tazama, baba yangu, ona kipande hiki cha joho lako mkononi mwangu! Nilikata upindo wa joho lako lakini sikukuua. Basi ujue na kutambua kuwa sina hatia ya kutenda mabaya wala ya kuasi. Wewe sijakukosea, lakini wewe unaniwinda mimi ili kuuondoa uhai wangu. 12 Bwana na ahukumu kati yangu na wewe. Naye Bwana alipize mabaya unayonitendea, lakini mkono wangu hautakugusa. 13 Kama msemo wa kale usemavyo, ‘Kutoka kwa watenda maovu hutoka matendo maovu,’ kwa hiyo mkono wangu hautakugusa wewe.
14 “Je, mfalme wa Israeli ametoka dhidi ya nani? Ni nani unayemfuatia? Je, ni mbwa mfu? Ni kiroboto? 15 Bwana na awe mwamuzi wetu, yeye na aamue kati yetu. Yeye na anitetee shauri langu; anihesabie haki kwa kuniokoa mkononi mwako.”
16 Daudi alipomaliza kusema haya, Sauli akamuuliza, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Ndipo Sauli akalia kwa sauti kuu, akisema, 17 “Wewe ni mwenye haki kuliko mimi; umenitendea mema, lakini mimi nimekutendea mabaya. 18 Sasa umeniambia juu ya mema uliyonitendea. Bwana alinitia mikononi mwako, lakini wewe hukuniua. 19 Je, mtu ampatapo adui yake, humwacha aende zake bila kumdhuru? Bwana na akulipe mema kwa jinsi ulivyonitenda leo. 20 Ninajua kwamba hakika utakuwa mfalme na ya kwamba ufalme wa Israeli utakuwa imara mikononi mwako. 21 Sasa niapie kwa Bwana kwamba hutakatilia mbali uzao wangu wala kulifuta jina langu kutoka jamaa ya baba yangu.”
22 Basi Daudi akamwapia Sauli. Kisha Sauli akarudi zake nyumbani, lakini Daudi na watu wake wakapanda kwenda ngomeni.
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Baada ya kumponyoka Sauli pangoni.
1 Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,
kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.
Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia
mpaka maafa yapite.
2 Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,
Mungu atimizaye makusudi yake kwangu.
3 Hutumana kutoka mbinguni na kuniokoa,
akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;
Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.
4 Niko katikati ya simba,
nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kuu:
watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,
ambao ndimi zao ni panga kali.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.
6 Waliitegea miguu yangu nyavu,
nikainamishwa chini na dhiki.
Wamechimba shimo katika njia yangu,
lakini wametumbukia humo wao wenyewe.
7 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
8 Amka, nafsi yangu!
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
9 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa;
nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni,
uaminifu wako unazifikia anga.
11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,
utukufu wako na uwe duniani pote.
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi.
58:1 Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki?
Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu?
2 La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu,
na mikono yenu hupima jeuri duniani.
3 Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao,
toka tumboni mwa mama zao
ni wakaidi na husema uongo.
4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka,
kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake,
5 ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi,
hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani.
6 Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao;
Ee Bwana, vunja meno makali ya hao simba!
7 Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi,
wavutapo pinde zao, mishale yao na iwe butu.
8 Kama konokono ayeyukavyo akitembea,
kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu,
wasilione jua.
9 Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba,
zikiwa mbichi au kavu,
waovu watakuwa
wamefagiliwa mbali.
10 Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi,
watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu.
11 Ndipo wanadamu watasema,
“Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu,
hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”
Zaburi ya Daudi. Wakati alipokuwa katika Jangwa la Yuda.
1 Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu,
nakutafuta kwa moyo wote;
nafsi yangu inakuonea kiu,
mwili wangu unakuonea wewe shauku,
katika nchi kame na iliyochoka
mahali ambapo hapana maji.
2 Nimekuona katika mahali patakatifu
na kuuona uwezo wako na utukufu wako.
3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai,
midomo yangu itakuadhimisha.
4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu,
na kwa jina lako nitainua mikono yangu.
5 Nafsi yangu itatoshelezwa
kama kwa wingi wa vyakula;
kwa midomo iimbayo
kinywa changu kitakusifu wewe.
6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe,
ninawaza juu yako makesha yote ya usiku.
7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu,
chini ya uvuli wa mbawa zako naimba.
8 Nafsi yangu inaambatana nawe,
mkono wako wa kuume hunishika.
9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa,
watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia.
10 Watatolewa wafe kwa upanga,
nao watakuwa chakula cha mbweha.
11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu,
wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu,
bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa.