Daudi huko Keila
1060 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Daudi alipoambiwa kuwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,”
20 Lakini Abiathari, mwana wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, akatoroka, akakimbia na kujiunga na Daudi. 21 Akamwambia Daudi kuwa Sauli amewaua makuhani wa Bwana. 22 Kisha Daudi akamwambia Abiathari: “Siku ile, wakati Doegi Mwedomu alipokuwa pale, nilijua atahakikisha amemwambia Sauli. Mimi ninawajibika kwa vifo vya jamaa ya baba yako yote. 23 Kaa pamoja nami; usiogope. Mtu anayeutafuta uhai wako anautafuta uhai wangu pia. Ukiwa pamoja nami utakuwa salama.”
6 (Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kisibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila.)
2 akauliza kwa Bwana, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?”
Bwana akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.”
3 Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Si zaidi sana, kama tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!”
4 Daudi akauliza kwa Bwana tena, naye Bwana akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” 5 Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila.
7 Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa amekwenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” 8 Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi.
9 Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kisibau.” 10 Daudi akasema, “Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. 11 Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.”
Naye Bwana akasema, “Ndiyo, atashuka.”
12 Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?”
Naye Bwana akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.”
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, nimekukimbilia wewe,
usiache nikaaibika kamwe,
kwa haki yako uniokoe.
2 Nitegee sikio lako,
uje uniokoe haraka;
uwe kwangu mwamba wa kimbilio,
ngome imara ya kuniokoa.
3 Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu,
uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako.
4 Uniepushe na mtego niliotegewa,
maana wewe ndiwe kimbilio langu.
5 Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,
unikomboe Ee Bwana, uliye Mungu wa kweli.
6 Ninawachukia wale wanaongʼangʼania sanamu batili;
mimi ninamtumaini Bwana.
7 Nitafurahia na kushangilia upendo wako,
kwa kuwa uliona mateso yangu
na ulijua maumivu ya nafsi yangu.
8 Hukunikabidhi kwa adui yangu
bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.
9 Ee Bwana unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;
macho yangu yanafifia kwa huzuni,
nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.
10 Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,
naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;
nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,
na mifupa yangu inachakaa.
11 Kwa sababu ya adui zangu wote,
nimedharauliwa kabisa na jirani zangu,
hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho,
wale wanionao barabarani hunikimbia.
12 Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,
nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.
13 Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi;
vitisho viko pande zote;
kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu,
na kula njama kuniua.
14 Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Bwana;
nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
15 Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako,
uniokoe mikononi mwa adui zangu
na wale wanifuatiao.
16 Mwangazie mtumishi wako uso wako,
uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.
17 Usiniache niaibike, Ee Bwana,
kwa maana nimekulilia wewe,
bali waovu waaibishwe
na kunyamazishwa Kuzimu.
18 Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe,
kwa maana kwa kiburi na dharau
wao husema kwa majivuno
dhidi ya wenye haki.
19 Tazama jinsi ulivyo mkuu wema wako,
uliowawekea akiba wakuchao,
ambao huwapa wale wakukimbiliao
machoni pa watu.
20 Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako
kutokana na hila za wanadamu;
katika makao yako huwaweka salama
kutokana na ndimi za mashtaka.
21 Atukuzwe Bwana,
kwa kuwa amenionyesha upendo wake wa ajabu
nilipokuwa katika mji uliozingirwa.
22 Katika hofu yangu nilisema,
“Nimekatiliwa mbali na macho yako!”
Hata hivyo ulisikia kilio changu
ukanihurumia nilipokuita unisaidie.
23 Mpendeni Bwana ninyi watakatifu wake wote!
Bwana huwahifadhi waaminifu,
lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.
24 Kuweni hodari na mjipe moyo,
ninyi nyote mnaomtumaini Bwana.