Daudi huko Mispa (continued)

1060 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 140

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Bwana, niokoe, kutoka kwa watu waovu;

nilinde na watu wenye jeuri,

2 ambao hupanga mipango mibaya mioyoni mwao,

na kuchochea vita siku zote.

3 Wao hufanya ndimi zao kali kama za nyoka,

sumu ya nyoka iko midomoni mwao.

4 Ee Bwana, niepushe na mikono ya waovu;

nilinde na watu wenye jeuri

wanaopanga kunikwaza miguu yangu.

5 Wenye kiburi wameficha mtego wa kuninasa,

wametandaza kamba za wavu wao,

wametega mitego kwenye njia yangu.

6 Ee Bwana, ninakuambia, “Wewe ni Mungu wangu.”

Ee Bwana, usikie kilio changu na kunihurumia.

7 Ee Bwana Mwenyezi, Mwokozi wangu mwenye nguvu,

unikingaye kichwa changu siku ya vita:

8 Ee Bwana, usiwape waovu matakwa yao,

usiache mipango yao ikafanikiwa,

wasije wakajisifu.

9 Vichwa vya wanaonizunguka vifunikwe

na shida zinazosababishwa na midomo yao.

10 Makaa ya mawe ya moto na yawaangukie!

Na watupwe motoni,

katika mashimo ya matope,

wasiinuke tena kamwe.

11 Wasingiziaji wasifanikiwe katika nchi;

maafa na yawawinde watu wenye jeuri.

12 Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki,

na kuitegemeza njia ya mhitaji.

13 Hakika wenye haki watalisifu jina lako,

na waadilifu wataishi mbele zako.

Zaburi 35

Zaburi ya Daudi.

1 Ee Bwana, pingana na wale wanaopingana nami,

upigane na hao wanaopigana nami.

2 Chukua ngao na kigao.

Inuka unisaidie.

3 Inua mkuki wako na fumo lako

dhidi ya hao wanaonifuatia.

Iambie nafsi yangu,

“Mimi ni wokovu wako.”

4 Wafedheheshwe na waaibishwe

wale wanaotafuta uhai wangu.

Wanaofanya shauri kuniangamiza

warudishwe nyuma kwa hofu.

5 Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,

malaika wa Bwana akiwafukuza.

6 Njia yao na iwe giza na ya utelezi,

malaika wa Bwana akiwafuatilia.

7 Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu,

na bila sababu wamenichimbia shimo,

8 maafa na yawapate ghafula:

wavu walionifichia na uwatege wenyewe,

na waanguke katika shimo hilo,

kwa maangamizo yao.

9 Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Bwana

na kuufurahia wokovu wake.

10 Nitapaza sauti yangu nikisema,

“Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana?

Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao,

maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”

11 Mashahidi wakatili wanainuka,

wananiuliza mambo nisiyoyajua.

12 Wananilipa baya kwa jema

na kuiacha nafsi yangu ukiwa.

13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia

na nikajinyenyekesha kwa kufunga.

Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,

14 niliendelea kuomboleza

kama vile wao ni rafiki au ndugu.

Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni

kama ninayemwombolezea mama yangu.

15 Lakini nilipojikwaa,

walikusanyika kwa shangwe;

washambuliaji walijikusanya dhidi yangu

bila mimi kujua.

Walinisingizia pasipo kukoma.

16 Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki,

wamenisagia meno.

17 Ee Bwana, utatazama mpaka lini?

Niokoe maisha yangu na maangamizi yao,

uhai wangu wa thamani

kutokana na simba hawa.

18 Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa,

nitakusifu katikati ya watu wengi.

19 Usiwaache wale wanaonisimanga,

wale ambao ni adui zangu bila sababu;

usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu

wakonyeze jicho kwa hila.

20 Hawazungumzi kwa amani,

bali wanatunga mashtaka ya uongo

dhidi ya wale wanaoishi

kwa utulivu katika nchi.

21 Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha!

Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”

22 Ee Bwana, umeona hili, usiwe kimya.

Usiwe mbali nami, Ee Bwana.

23 Amka, inuka unitetee!

Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.

24 Nihukumu kwa haki yako, Ee Bwana Mungu wangu,

sawasawa na haki yako;

usiwaache wakusimange.

25 Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!”

Au waseme, “Tumemmeza.”

26 Wote wanaofurahia dhiki yangu

waaibishwe na wachanganyikiwe;

hao wanaojiinua dhidi yangu

wavikwe aibu na dharau.

27 Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki

wapige kelele za shangwe na furaha;

hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe,

ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”

28 Ulimi wangu utanena haki yako

na sifa zako mchana kutwa.

Zaburi 64

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu,

uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.

2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu,

kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya.

3 Wananoa ndimi zao kama panga

na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.

4 Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia,

humrushia ghafula bila woga.

5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake

katika mipango mibaya;

huzungumza juu ya kuficha mitego yao,

nao husema, “Ni nani ataiona?”

6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema,

“Tumebuni mpango mkamilifu!”

Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.

7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale,

nao ghafula wataangushwa.

8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao

na kuwaleta kwenye maangamizi;

wote wawaonao watatikisa vichwa vyao

kwa dharau.

9 Wanadamu wote wataogopa,

watatangaza kazi za Mungu

na kutafakari yale aliyoyatenda.

10 Wenye haki na wafurahi katika Bwana,

na wakimbilie kwake;

wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!