Daudi huko Mispa (continued)

1060 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Zaburi 109

Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mungu, ambaye ninakusifu,

usiwe kimya,

2 kwa maana watu waovu na wadanganyifu

wamefungua vinywa vyao dhidi yangu;

wasema dhidi yangu

kwa ndimi za udanganyifu.

3 Wamenizunguka kwa maneno ya chuki,

wananishambulia bila sababu.

4 Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki,

lakini mimi ninawaombea.

5 Wananilipiza mabaya kwa mema,

chuki badala ya urafiki wangu.

6 Agiza mtu mwovu ampinge,

mshtaki asimame mkono wake wa kuume.

7 Anapohukumiwa, apatikane na hatia,

nayo maombi yake yamhukumu.

8 Siku zake za kuishi na ziwe chache,

nafasi yake ya uongozi ichukuliwe na mtu mwingine.

9 Watoto wake na waachwe yatima,

mke wake na awe mjane.

10 Watoto wake na watangetange wakiomba,

na wafukuzwe kwenye magofu ya nyumba zao.

11 Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo,

matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni.

12 Asiwepo mtu yeyote wa kumtendea mema

wala wa kuwahurumia yatima wake.

13 Uzao wake na ukatiliwe mbali,

majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho.

14 Maovu ya baba zake na yakumbukwe

mbele za Bwana,

dhambi ya mama yake

isifutwe kamwe.

15 Dhambi zao na zibaki daima mbele za Bwana,

ili apate kukatilia mbali kumbukumbu lao duniani.

16 Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema,

bali alimfukuza mnyonge na mhitaji,

aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo.

17 Alipenda kulaani,

nayo laana ikampata;

hakupenda kubariki,

kwa hiyo baraka na ikae mbali naye.

18 Alivaa kulaani kama vazi lake,

nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji,

kwenye mifupa yake kama mafuta.

19 Na iwe kama joho alilozungushiwa,

kama mshipi aliofungiwa daima.

20 Haya na yawe malipo ya Bwana kwa washtaki wangu,

kwa wale wanaoninenea mabaya.

21 Lakini wewe, Ee Bwana Mwenyezi,

unitendee wema kwa ajili ya jina lako,

uniokoe kwa wema wa pendo lako.

22 Maana mimi ni maskini na mhitaji,

moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.

23 Ninafifia kama kivuli cha jioni,

nimerushwa-rushwa kama nzige.

24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga,

mwili wangu umedhoofika na kukonda.

25 Nimekuwa kitu cha kudharauliwa kwa washtaki wangu,

wanionapo, hutikisa vichwa vyao.

26 Ee Bwana, Mungu wangu nisaidie,

niokoe sawasawa na upendo wako.

27 Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako,

kwamba wewe, Ee Bwana, umetenda hili.

28 Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki,

watakaposhambulia wataaibishwa,

lakini mtumishi wako atashangilia.

29 Washtaki wangu watavikwa fedheha,

na kufunikwa na aibu kama joho.

30 Kwa kinywa changu nitamtukuza sana Bwana,

katika umati mkubwa nitamsifu.

31 Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji,

kuokoa maisha yake kutoka kwa wale wanaomhukumu.

Zaburi 17

Sala ya Daudi.

1 Sikia, Ee Bwana, kusihi kwangu kwa haki,

sikiliza kilio changu.

Tega sikio kwa ombi langu,

halitoki kwenye midomo ya udanganyifu.

2 Hukumu yangu na itoke kwako,

macho yako na yaone yale yaliyo haki.

3 Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku,

ingawa umenijaribu, hutaona chochote.

Nimeamua kwamba kinywa changu

hakitatenda dhambi.

4 Kuhusu matendo ya wanadamu:

kwa neno la midomo yako,

nimejiepusha

na njia za wenye jeuri.

5 Hatua zangu zimeshikamana na njia zako;

nyayo zangu hazikuteleza.

6 Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu,

nitegee sikio lako na usikie ombi langu.

7 Uonyeshe ajabu ya upendo wako mkuu,

wewe uokoaye kwa mkono wako wa kuume

wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.

8 Nilinde kama mboni ya jicho lako,

unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako

9 kutokana na waovu wanaonishambulia,

kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.

10 Huifunga mioyo yao iliyo migumu,

vinywa vyao hunena kwa majivuno.

11 Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira,

wakiwa macho, waniangushe chini.

12 Wamefanana na simba mwenye njaa awindaye,

kama simba mkubwa anyemeleaye mafichoni.

13 Inuka, Ee Bwana, pambana nao, uwaangushe,

niokoe kutokana na waovu kwa upanga wako.

14 Ee Bwana, mkono wako uniokoe na watu wa jinsi hii,

kutokana na watu wa ulimwengu huu

ambao fungu lao liko katika maisha haya.

Na wapate adhabu ya kuwatosha.

Watoto wao na wapate zaidi ya hayo,

hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao.

15 Na mimi katika haki nitauona uso wako,

niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.