Tabiri za Mwisho za Zekaria
457 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Neno:
Neno la Bwana liko kinyume na nchi ya Hadraki
na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika,
kwa kuwa macho ya watu na ya kabila zote
za Israeli yako kwa Bwana,
2 pia juu ya Hamathi inayopakana nayo,
juu ya Tiro na Sidoni,
ingawa wana ujuzi mwingi sana.
3 Tiro amejijengea ngome imara,
amelundika fedha kama mavumbi
na dhahabu kama taka za mitaani.
4 Lakini Bwana atamwondolea mali zake
na kuuangamiza uwezo wake wa baharini,
naye atateketezwa kwa moto.
5 Ashkeloni ataona hili na kuogopa;
Gaza atagaagaa kwa maumivu makali,
pia Ekroni, kwa sababu
matumaini yake yatanyauka.
Gaza atampoteza mfalme wake
na Ashkeloni ataachwa pweke.
6 Wageni watakalia mji wa Ashdodi,
nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
7 Nitaondoa damu vinywani mwao,
chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao.
Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu,
nao watakuwa viongozi katika Yuda,
naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi.
8 Lakini nitailinda nyumba yangu
dhidi ya majeshi ya wanyangʼanyi.
Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena,
kwa maana sasa ninawachunga.
9 Shangilia sana, ee Binti Sayuni!
Piga kelele, Binti Yerusalemu!
Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,
ni mwenye haki, naye ana wokovu,
ni mpole, naye amepanda punda,
mwana-punda, mtoto wa punda.
10 Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu
na farasi wa vita kutoka Yerusalemu,
nao upinde wa vita utavunjwa.
Atatangaza amani kwa mataifa.
Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari,
na kutoka Mto Frati hadi mwisho wa dunia.
11 Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya Agano langu nawe,
nitawaacha huru wafungwa wako
watoke kwenye shimo lisilo na maji.
12 Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini;
hata sasa ninatangaza kwamba
nitawarejesheeni maradufu.
13 Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu,
nitamfanya Efraimu mshale wangu.
Nitawainua wana wako, ee Sayuni,
dhidi ya wana wako, ee Uyunani,
na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.
14 Kisha Bwana atawatokea;
mshale wake utamulika
kama umeme wa radi.
Bwana Mwenyezi atapiga tarumbeta,
naye atatembea katika tufani za kusini,
15 na Bwana Mwenye Nguvu Zote atawalinda.
Wataangamiza na kushinda
kwa mawe ya kutupa kwa kombeo.
Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo;
watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia
kwenye pembe za madhabahu.
16 Bwana Mungu wao atawaokoa siku hiyo
kama kundi la watu wake.
Watangʼara katika nchi yake
kama vito vya thamani kwenye taji.
17 Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri!
Nafaka itawastawisha vijana wanaume,
nayo divai mpya vijana wanawake.
10:1 Mwombeni Bwana mvua wakati wa vuli;
ndiye Bwana atengenezaye mawingu ya tufani.
Huwapa watu manyunyu ya mvua,
pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu.
2 Sanamu huzungumza udanganyifu,
waaguzi huona maono ya uongo;
husimulia ndoto ambazo si za kweli,
wanatoa faraja batili.
Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo
walioonewa kwa kukosa mchungaji.
3 “Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji,
nami nitawaadhibu viongozi;
kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote
atalichunga kundi lake,
nyumba ya Yuda,
naye atawafanya kuwa kama farasi
mwenye kiburi akiwa vitani.
4 Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni,
kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema,
kutoka kwake utatoka upinde wa vita,
kutoka kwake atatoka kila mtawala.
5 Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa
wanaokanyaga barabara za matope
wakati wa vita.
Kwa sababu Bwana yu pamoja nao,
watapigana na kuwashinda wapanda farasi.
6 “Nitaiimarisha nyumba ya Yuda
na kuiokoa nyumba ya Yosefu.
Nitawarejesha kwa sababu
nina huruma juu yao.
Watakuwa kama watu ambao
sijawahi kuwakataa
kwa sababu mimi ndimi Bwana Mungu wao,
nami nitawajibu.
7 Waefraimu watakuwa kama mashujaa,
mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai.
Watoto wao wataona na kufurahi,
mioyo yao itashangilia katika Bwana.
8 Nitawaashiria na kuwakusanya ndani.
Hakika nitawakomboa,
nao watakuwa wengi
kama walivyokuwa mwanzoni.
9 Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa,
hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali
watanikumbuka mimi.
Wao na watoto wao watanusurika katika hatari
nao watarudi.
10 Nitawarudisha kutoka Misri
na kuwakusanya toka Ashuru.
Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni,
na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha.
11 Watapita katika bahari ya mateso;
bahari iliyochafuka itatulizwa
na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka.
Kiburi cha Ashuru kitashushwa,
nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka.
12 Nitawaimarisha katika Bwana,
na katika jina lake watatembea,”
asema Bwana.
11:1 Fungua milango yako, ee Lebanoni,
ili moto uteketeze mierezi yako!
2 Piga yowe, ee mti wa msunobari,
kwa kuwa mwerezi umeanguka;
miti ya fahari imeharibiwa!
Piga yowe, enyi mialoni ya Bashani,
msitu mnene umefyekwa!
3 Sikiliza yowe la wachungaji;
malisho yao manono yameangamizwa!
Sikia ngurumo za simba;
kichaka kilichostawi sana
cha Yordani kimeharibiwa!
4 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu wangu: “Lilishe kundi lililokusudiwa kuchinjwa. 5 Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘Bwana asifiwe, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii. 6 Kwa kuwa sitawahurumia tena watu wa nchi,” asema Bwana. “Nitawakabidhi kila mtu mkononi mwa jirani yake na mfalme wake. Wataitenda jeuri nchi, nami sitawaokoa kutoka mikononi mwao.”
7 Kwa hiyo nikalilisha kundi lililotiwa alama kwa kuchinjwa, hasa kundi lililoonewa sana. Kisha nikachukua fimbo mbili, moja nikaiita Fadhili na nyingine Umoja, nami nikalilisha kundi. 8 Katika mwezi mmoja nikawaondoa wachungaji watatu.
Kundi la kondoo likanichukia, nami nikachoshwa nao, 9 nikasema, “Sitakuwa mchungaji wenu. Waache wanaokufa wafe na wanaoangamia waangamie. Wale waliobakia kila mmoja na ale nyama ya mwenzake.”
10 Kisha nikachukua fimbo yangu inayoitwa Fadhili nikaivunja, kutangua Agano nililofanya na mataifa yote. 11 Likatanguka siku hiyo, kwa hiyo wale waliodhurika katika kundi, waliokuwa wakiniangalia wakajua kuwa hilo lilikuwa neno la Bwana.
12 Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha.
13 Naye Bwana akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya Bwana.
14 Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Umoja, kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli!
15 Kisha Bwana akaniambia, “Vitwae tena vifaa vya mchungaji mpumbavu. 16 Kwa maana ninakwenda kumwinua mchungaji juu ya nchi ambaye hatamjali aliyepotea, wala kuwatafuta wale wachanga au kuwaponya waliojeruhiwa, wala kuwalisha wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo wanono na kuzirarua kwato zao.
17 “Ole wa mchungaji asiyefaa,
anayeliacha kundi!
Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume!
Mkono wake na unyauke kabisa,
jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”