Tabiri za Mwisho za Zekaria (continued)
457 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Hili ni neno la Bwana kuhusu Israeli. Bwana, yeye azitandaye mbingu, awekaye misingi ya dunia na aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake, asema: 2 “Nitakwenda kufanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbisha mataifa yote yanayoizunguka. Yuda utazingirwa kwa vita na Yerusalemu pia. 3 Katika siku hiyo, wakati mataifa yote ya dunia yatakapokusanyika dhidi yake, nitaufanya Yerusalemu kuwa jabali lisilosogezwa kwa mataifa yote. Wote watakaojaribu kulisogeza watajiumiza wenyewe. 4 Katika siku hiyo nitampiga kila farasi kwa hofu ya ghafula, naye ampandaye nitampiga kwa uwazimu,” asema Bwana. “Nitalielekeza jicho langu la ulinzi juu ya nyumba ya Yuda, nami nitawapofusha farasi wote wa mataifa. 5 Kisha viongozi wa Yuda watasema mioyoni mwao, ‘Watu wa Yerusalemu wana nguvu kwa sababu Bwana Mwenye Nguvu Zote ni Mungu wao.’
6 “Katika siku hiyo nitawafanya viongozi wa Yuda kuwa kama kigae cha moto ndani ya lundo la kuni, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watateketeza kulia na kushoto mataifa yote yanayowazunguka, lakini Yerusalemu utabaki salama mahali pake.
7 “Bwana atayaokoa makao ya Yuda kwanza, ili heshima ya nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu isiwe kubwa zaidi kuliko ile ya Yuda. 8 Katika siku hiyo, Bwana atawakinga wale waishio Yerusalemu, ili kwamba aliye dhaifu kupita wote miongoni mwao awe kama Daudi, nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama Malaika wa Bwana akiwatangulia. 9 Katika siku hiyo nitatoka kuangamiza mataifa yote yatakayoshambulia Yerusalemu.
10 “Nami nitamiminia nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu roho ya neema na maombi. Watanitazama mimi, yule waliyemchoma. Nao watamwombolezea kama mtu anayemwombolezea mwanawe wa pekee na kusikitika kwa uchungu kama anayemsikitikia mzaliwa wake wa kwanza wa kiume. 11 Katika siku hiyo kilio kitakuwa kikubwa Yerusalemu, kama kilio cha Hadad-Rimoni katika tambarare ya Megido. 12 Nchi itaomboleza, kila ukoo peke yake, nao wake zao peke yao. Ukoo wa nyumba ya Daudi na wake zao, ukoo wa nyumba ya Nathani na wake zao, 13 ukoo wa nyumba ya Lawi na wake zao, ukoo wa Shimei na wake zao, 14 na koo zote zilizobaki na wake zao.
13:1 “Katika siku hiyo, chemchemi itafunguliwa kwa nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu, kuwatakasa dhambi na unajisi.
2 “Katika siku hiyo, nitayakatilia mbali majina ya sanamu kutoka nchi, nayo hayatakumbukwa tena,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. “Nitaondoa manabii wao pamoja na roho ya uchafu katika nchi. 3 Ikiwa yupo yeyote atakayeendelea kutabiri, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Ni lazima ufe, kwa sababu umesema uongo kwa jina la Bwana.’ Atakapotabiri, wazazi wake mwenyewe watampasua tumbo.
4 “Katika siku hiyo, kila nabii ataaibika kwa maono ya unabii wake. Hatavaa vazi la kinabii la nywele ili apate kudanganya watu. 5 Atasema, ‘Mimi sio nabii. Mimi ni mkulima; ardhi imekuwa kazi yangu tangu ujana wangu.’ 6 Ikiwa mtu atamuuliza, ‘Majeraha haya yaliyo mwilini mwako ni ya nini?’ Atajibu, ‘Ni majeraha niliyoyapata katika nyumba ya rafiki zangu.’
7 “Amka, ee upanga, dhidi ya mchungaji wangu,
dhidi ya mtu aliye karibu nami!”
asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
“Mpige mchungaji,
nao kondoo watatawanyika,
nami nitageuza mkono wangu
dhidi ya walio wadogo,
8 katika nchi yote,” asema Bwana,
“theluthi mbili watapigwa na kuangamia;
hata hivyo theluthi moja watabaki ndani yake.
9 Hii theluthi moja nitaileta katika moto;
nitawasafisha kama fedha isafishwavyo
na kuwajaribu kama dhahabu.
Wataliitia Jina langu
nami nitawajibu;
nitasema, ‘Hawa ni watu wangu,’
nao watasema, ‘Bwana ni Mungu wetu.’ ”
14:1 Siku ya Bwana inakuja ambayo nyara zilizotekwa kwenu zitagawanywa miongoni mwenu.
2 Nitayakusanya mataifa yote huko Yerusalemu kupigana dhidi yake, mji utatekwa, nyumba zitavamiwa na kuporwa na wanawake watanajisiwa. Nusu ya mji watakwenda uhamishoni, lakini watakaobaki hawataondolewa kutoka mjini.
3 Kisha Bwana atatoka na kupigana dhidi ya watu wa yale mataifa, kama apiganavyo siku ya vita. 4 Siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni, mashariki mwa Yerusalemu, nao Mlima wa Mizeituni utagawanyika mara mbili kuanzia mashariki hadi magharibi, ukifanya bonde kubwa, nusu ya mlima ukisogea kuelekea kaskazini na nusu kuelekea kusini. 5 Nanyi mtakimbia kupitia katika bonde hilo la mlima wangu kwa kuwa litaenea hadi Aseli. Mtakimbia kama mlivyokimbia tetemeko la ardhi katika siku za Uzia mfalme wa Yuda. Kisha Bwana Mungu wangu atakuja na watakatifu wote pamoja naye.
6 Siku hiyo hakutakuwepo nuru, baridi wala theluji. 7 Itakuwa siku ya kipekee, isiyo na mchana wala usiku, siku ijulikanayo na Bwana. Jioni inapofika nuru itakuwepo.
8 Siku hiyo, maji yaliyo hai yatatiririka kutoka Yerusalemu, nusu kwenda kwenye bahari ya mashariki, na nusu kwenda kwenye bahari ya magharibi wakati wa kiangazi na wakati wa masika.
9 Bwana atakuwa mfalme juu ya dunia yote. Katika siku hiyo atakuwepo Bwana mmoja na jina lake litakuwa jina pekee.
10 Nchi yote kuanzia Geba, kaskazini mwa Yuda, hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itakuwa kama Araba. Lakini Yerusalemu utainuliwa juu na kubaki mahali pake, toka Lango la Benyamini hadi mahali pa Lango la Kwanza, mpaka kwenye Lango la Pembeni na kutoka Mnara wa Hananeli hadi kwenye mashinikizo ya divai ya mfalme. 11 Utakaliwa na watu, kamwe hautaharibiwa tena, Yerusalemu utakaa salama.
12 Hii ndiyo tauni ambayo Bwana atapiga nayo mataifa yote ambayo yalipigana dhidi ya Yerusalemu: Nyama ya miili yao itaoza wangali wamesimama kwa miguu yao, macho yao yataoza kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza vinywani mwao. 13 Katika siku hiyo Bwana atawatia wanaume hofu kuu. Kila mwanaume atakamata mkono wa mwenzake nao watashambuliana. 14 Yuda pia atapigana katika Yerusalemu. Utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka Yerusalemu utakusanywa, wingi wa dhahabu, fedha na nguo. 15 Tauni ya aina iyo hiyo itapiga farasi na nyumbu, ngamia na punda, nao wanyama wote walioko kwenye kambi za adui.
16 Kisha walionusurika katika mataifa yote ambayo yaliushambulia Yerusalemu watakuwa wakipanda Yerusalemu kila mwaka kumwabudu Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote na kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. 17 Ikiwa taifa lolote la dunia hawatakwenda Yerusalemu kumwabudu Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote, mvua haitanyesha kwao. 18 Ikiwa watu wa Misri nao hawatakwenda kushiriki, hawatapata mvua. Bwana ataleta juu yao tauni ile ambayo itawapiga mataifa yale ambayo hayatakwenda kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda. 19 Hii itakuwa adhabu ya Misri na adhabu ya mataifa yote yale ambayo hayatakwenda Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Vibanda.
20 Katika siku hiyo, kengele zilizofungwa kwenye farasi zitaandikwa maneno haya: Takatifu kwa Bwana, navyo vyungu vya kupikia katika nyumba ya Bwana vitakuwa kama bakuli takatifu mbele ya madhabahu. 21 Kila chungu kilichoko Yerusalemu na Yuda kitakuwa kitakatifu kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote na wote wanaokuja kutoa dhabihu watachukua baadhi ya vyungu hivyo na kupikia. Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote.
Mordekai Afichua Njama dhidi ya Artashasta
21 Wakati Mordekai alikuwa ameketi kwenye lango la mfalme, Bigthana na Tereshi, maafisa wawili wa mfalme waliokuwa walinzi wa lango, walikasirika na kupanga njama ya kumuua Mfalme Ahasuero. 22 Lakini Mordekai aligundua hila hii na kumwambia Malkia Esta, ambaye baadaye alimwarifu mfalme, huku akimsifu Mordekai. 23 Taarifa hiyo ilipochunguzwa na kuonekana kuwa kweli, maafisa hao wawili waliangikwa juu ya miti ya kunyongea. Haya yote yaliandikwa katika kitabu cha kumbukumbu mbele ya mfalme.