Mageuzi ya Ezra
457 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Baada ya mambo haya kutendeka, viongozi walinijia na kusema, “Watu wa Israeli, wakiwemo makuhani na Walawi, hawakujitenga na majirani zao katika kufanya machukizo, kama yale ya Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wayebusi, Waamoni, Wamoabu, Wamisri na Waamori. 2 Wamewaoa baadhi ya binti zao kuwa wake zao na wake za wana wao, nao wamechanganya taifa takatifu na watu waliowazunguka. Nao viongozi na maafisa wamekuwa mstari wa mbele katika njia hii potovu.”
3 Niliposikia jambo hili nilirarua koti langu na joho langu, nikazingʼoa nywele za kichwa changu na ndevu zangu na kuketi nikishangaa. 4 Kisha kila mmoja aliyetetemeshwa na maneno ya Mungu wa Israeli alikusanyika kunizunguka kwa sababu ya upotovu huu wa hao watu waliorudi kutoka utumwani. Nami niliketi pale nikishangaa mpaka wakati wa dhabihu ya jioni.
5 Ndipo wakati wa kutoa dhabihu ya jioni nikainuka kutoka kujidhili kwangu nikiwa na koti na joho langu lililoraruka, nikapiga magoti mikono yangu ikiwa imeinuliwa kwa Bwana Mungu wangu. 6 Nami nikaomba:
“Ee Mungu wangu, natahayari na kuona aibu kukuinulia uso wangu Mungu wangu, kwa sababu dhambi zetu zimejikusanya hata kupita juu ya vichwa vyetu na hatia yetu imefika mbinguni. 7 Tokea siku za babu zetu mpaka sasa, hatia yetu imekuwa kubwa. Kwa sababu ya dhambi zetu, sisi na wafalme wetu na makuhani wetu tumekabiliwa na vita, utumwa, kutekwa na kudhiliwa katika mikono ya wafalme wa kigeni, kama ilivyo leo.
8 “Lakini sasa, kwa muda mfupi, Bwana Mungu wetu amekuwa na neema kwa kutuachia mabaki na kutupa mahali imara katika mahali pake patakatifu, hivyo Mungu wetu atupa mwanga machoni petu na unafuu katika utumwa wetu. 9 Ingawa tu watumwa, Mungu wetu hajatuacha katika kufungwa kwetu. Ametuonyesha huruma mbele ya wafalme wa Uajemi: Ametujalia maisha mapya kwa kujenga upya nyumba ya Mungu wetu na kukarabati magofu yake, naye ametupa ukuta wa ulinzi katika Yuda na Yerusalemu.
10 “Lakini sasa, Ee Mungu wetu, tunaweza kusema nini baada ya hili? Kwa maana tumedharau maagizo 11 uliyoyatoa kupitia watumishi wako manabii uliposema: ‘Nchi mnayoiingia kuimiliki ni nchi iliyochafuliwa na uovu wa watu wake. Kwa matendo yao ya machukizo wameijaza nchi kwa unajisi wao kutoka mwisho mmoja hadi mwingine. 12 Kwa hiyo, msiwaoze binti zenu kwa wana wao wala binti zao kwa wana wenu. Msitafute mkataba wa urafiki nao kwa wakati wowote. Ndipo mtakapofanikiwa na kula mema ya nchi na kuwaachia watoto wenu nchi hiyo kama urithi wao wa milele.’
13 “Yale yaliyotupata ni matokeo ya matendo yetu mabaya, pia hatia yetu kubwa. Hata hivyo, wewe Mungu wetu, umetuadhibu kidogo kuliko dhambi zetu zilivyostahili na umetupa mabaki kama haya. 14 Je, tutavunja maagizo yako tena na kuoana na watu ambao hufanya mambo ya machukizo? Je, hutakuwa na hasira ya kutosha juu yetu na kutuangamiza, bila kutuachia mabaki wala atakayenusurika? 15 Ee Bwana, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki! Leo hii tumeachwa kama mabaki. Tupo hapa mbele zako na hatia yetu, ingawa katika hali hii hakuna hata mmoja wetu anayeweza kusimama mbele zako.”
10:1 Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama, huku akilia na kujitupa chini mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa Waisraeli, wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kumzunguka. Nao pia wakalia sana. 2 Kisha Shekania mwana wa Yehieli, mmoja wa wazao wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni kutoka mataifa yanayotuzunguka. Lakini pamoja na hili, bado liko tumaini kwa ajili ya Israeli. 3 Sasa na tufanye agano mbele za Mungu wetu kuwafukuza hawa wanawake wote pamoja na watoto wao, kulingana na maonyo ya bwana wangu pamoja na wale ambao wanaogopa amri za Mungu wetu. Hili na lifanyike sawasawa na hii Sheria. 4 Inuka, suala hili lipo mikononi mwako. Sisi tutaungana nawe, uwe na ujasiri ukatende hili.”
5 Basi Ezra akainuka na kuwaapisha makuhani viongozi, Walawi na Israeli yote kufanya lile lililokuwa limependekezwa. Nao wakaapa. 6 Ndipo Ezra akaondoka hapo mbele ya nyumba ya Mungu akaenda kwenye chumba cha Yehohanani mwana wa Eliashibu. Wakati alipokuwa hapo, hakula chakula wala hakunywa maji, kwa sababu aliendelea kuomboleza kuhusu kukosa uaminifu kwa watu wa uhamishoni.
7 Ndipo lilipotolewa tangazo Yuda yote na Yerusalemu kwa watu wote waliokuwa uhamishoni kukusanyika Yerusalemu. 8 Yeyote ambaye hangejitokeza kwa muda wa siku tatu angepoteza mali yake yote, kulingana na uamuzi wa maafisa na wazee, naye mtu huyo angefukuzwa kutoka kusanyiko la watu waliokuwa uhamishoni.
9 Katika muda wa siku tatu, watu wote wa Yuda na Benyamini wakawa wamekusanyika huko Yerusalemu. Kwenye siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walikuwa wameketi ndani ya uwanja mbele ya nyumba ya Mungu, wakiwa na majonzi mno kwa tukio hilo na kwa sababu ya mvua kubwa. 10 Ndipo Kuhani Ezra aliposimama akawaambia, “Mmekosa uaminifu, mmeoa wanawake wa kigeni, mkaongezea hatia ya Israeli. 11 Sasa tubuni kwa Bwana, Mungu wa baba zenu mkafanye mapenzi yake. Jitengeni na mataifa wanaowazunguka na wake zenu wa kigeni.”
12 Kusanyiko lote likajibu kwa sauti kubwa: “Uko sawa kabisa! Ni lazima tufanye kama unavyosema. 13 Lakini hapa pana watu wengi na ni wakati wa mvua, hivyo hatuwezi kusimama nje. Hata hivyo, shauri hili haliwezi kumalizika kwa siku moja au mbili, kwa sababu tumefanya dhambi kubwa katika jambo hili. 14 Maafisa wetu na wafanye kwa niaba ya kusanyiko lote. Kisha kila mmoja katika miji yetu ambaye ameoa mwanamke wa kigeni aje kwa wakati uliopangwa, akiwa pamoja na wazee na waamuzi wa kila mji, hadi hasira kali ya Mungu wetu katika shauri hili itakapoondolewa kwetu.” 15 Yonathani mwana wa Asaheli na Yazeya mwana wa Tikwa peke yao, wakiungwa mkono na Meshulamu na Shabethai Mlawi, ndio waliopinga jambo hili.
16 Basi watu wa uhamishoni wakafanya kama ilivyokuwa imependekezwa. Kuhani Ezra akachagua wanaume waliokuwa viongozi wa jamaa, mmoja kutoka kila mgawanyo wa jamaa, nao wote wakachaguliwa kwa majina. Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kumi waliketi kuchunguza mashauri hayo. 17 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wakawa wamemaliza kushughulikia wanaume wote waliokuwa wameoa wanawake wa kigeni.
18 Miongoni mwa wazao wa makuhani, wafuatao walikuwa wameoa wanawake wa kigeni:
Kutoka wazao wa Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zake: Maaseya, Eliezeri, Yaribu na Gedalia. 19 (Wote walitoa nadhiri kwa kuandika kwa mikono yao kuwafukuza wake zao, kwa hatia yao, kila mmoja akatoa kondoo dume kutoka kundini mwake kama sadaka ya hatia.)
20 Kutoka wazao wa Imeri:
Hanani na Zebadia.
21 Kutoka wazao wa Harimu:
Maaseya, Eliya, Shemaya, Yehieli na Uzia.
22 Kutoka wazao wa Pashuri:
Elioenai, Maaseya, Ishmaeli, Nethaneli, Yozabadi na Elasa.
23 Miongoni mwa Walawi:
Yozabadi, Shimei, Kelaya (ndiye Kelita), Pethahia, Yuda na Eliezeri.
24 Kutoka waimbaji:
Eliashibu.
Kutoka mabawabu:
Shalumu, Telemu na Uri.
25 Miongoni mwa Waisraeli wengine:
Kutoka wazao wa Paroshi:
Ramia, Izia, Malkiya, Miyamini, Eleazari, Malkiya na Benaya.
26 Kutoka wazao wa Elamu:
Matania, Zekaria, Yehieli, Abdi, Yeremothi na Eliya.
27 Kutoka wazao wa Zatu:
Elioenai, Eliashibu, Matania, Yeremothi, Zabadi na Aziza.
28 Kutoka uzao wa Bebai:
Yehohanani, Hanania, Zabai na Athlai.
29 Kutoka wazao wa Bani:
Meshulamu, Maluki, Adaya, Yashubu, Sheali na Yeremothi.
30 Kutoka wazao wa Pahath-Moabu:
Adna, Kelali, Benaya, Maaseya, Matania, Bezaleli, Binui na Manase.
31 Kutoka wazao wa Harimu:
Eliezeri, Ishiya, Malkiya, Shemaya, Shimeoni, 32 Benyamini, Maluki, na Shemaria.
33 Kutoka wazao wa Hashumu:
Matenai, Matata, Zabadi, Elifeleti, Yeremai, Manase na Shimei.
34 Kutoka wazao wa Bani:
Maadai, Amramu, Ueli, 35 Benaya, Bedeya, Keluhi, 36 Vania, Meremothi, Eliashibu, 37 Matania, Matenai na Yaasu.
38 Kutoka wazao wa Binui:
Shimei, 39 Shelemia, Nathani, Adaya, 40 Maknadebai, Shashai, Sharai, 41 Azareli, Shelemia, Shemaria, 42 Shalumu, Amaria na Yosefu.
43 Kutoka wazao wa Nebo:
Yeieli, Matithia, Zabadi, Zebina, Yadai, Yoeli na Benaya.
44 Hawa wote walikuwa wameoa wanawake wa kigeni, na baadhi yao walikuwa wamezaa nao watoto.