Ole kwa Miji Iliyopewa Fursa

Ole kwa miji iliyopewa fursa, na madai ya Kristo akiwa mwalimu anayefundisha kuhusu Baba.

Galilaya

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 11:20–30

11:20 Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu. 21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwepo hadi leo. 24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”

25 Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

Mwanamke Mwenye Dhambi Anaipaka Miguu ya Kristo Mafuta

Mwanamke mwenye dhambi anaipaka miguu ya Kristo mafuta katika nyumba ya Simoni, Farisayo. Mfano wa wadeni wawili.

Galilaya

Luka 7:36–50

7:36 Basi Farisayo mmoja alimwalika Yesu nyumbani kwake kwa chakula. Hivyo Yesu akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kukaa katika nafasi yake mezani. 37 Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marhamu yenye manukato. 38 Yule mwanamke akasimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake, akaibusu na kuimiminia manukato.

39 Yule Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa, na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani, na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.”

40 Yesu akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.”

Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.”

41 “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500 na mwingine dinari hamsini. 42 Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?”

43 Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.”

Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.”

44 Kisha akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake, na kunifuta kwa nywele zake. 45 Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia. 46 Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato. 47 Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”

49 Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”

50 Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Yesu Anazuru Galilaya kwa Mara ya Pili

Hapa Yesu anafanya ziara ya pili ya Galilaya (kati ya ziara tatu kwa jumla), safari hii akiwa na wale Kumi na Wawili wote. Kazi hiyo inachochea uadui mkali wa Mafarisayo. Wanatoa shtaka la kufuru kwamba Yesu anashirikiana na Shetani. Hata familia ya Yesu mwenyewe inahofia kwamba amerukwa na akili kwa sababu ya msisimko na mashtaka hayo.

Luka 8:1–3

8:1 Baada ya haya Yesu alikwenda, akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye, 2 pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa. Miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba; 3 Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode; Susana; na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.