Yohana Anatuma Ujumbe na Yesu Anamsifu

Ujumbe kutoka kwa Yohana Mbatizaji, na sifa za Yesu kwake.

Galilaya

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 11:2–19

11:2 Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake 3 ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

4 Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona: 5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema.

6 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

7 Wale wanafunzi wa Yohana walipokuwa wanaondoka, Yesu akaanza kusema na makutano kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?

8 Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme.

9 Basi mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.

10 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako.’

11 Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji. Lakini aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni ni mkuu kuliko Yohana. 12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa, Ufalme wa Mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka. 13 Kwa maana manabii wote na Sheria walitabiri mpaka wakati wa Yohana. 14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Eliya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja.

15 Yeye aliye na masikio, na asikie.

16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,

17 “ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza;

tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,

lakini hamkuomboleza.’

18 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’

19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”

Luka 7:18–35

7:18 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakamweleza Yohana mambo haya yote. Hivyo Yohana akawaita wanafunzi wake wawili 19 na kuwatuma kwa Bwana ili kumuuliza, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

20 Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?’ ”

21 Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, na pia akawafungua vipofu wengi macho wakapata kuona.

22 Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mnayoyaona na kuyasikia: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa habari njema.

23 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

24 Wajumbe wa Yohana walipoondoka, Yesu akaanza kusema na makutano kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?

25 Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya kifahari na kuishi maisha ya anasa wako katika majumba ya kifalme.

26 Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii.

27 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,

atakayetengeneza njia mbele yako.’

28 Nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hakuna aliye mkuu kuliko Yohana. Lakini yeye aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”

29 (Watu wote hata watoza ushuru waliposikia maneno ya Yesu, walikubali kwamba mpango wa Mungu ni haki, maana walikuwa wamebatizwa na Yohana. 30 Lakini Mafarisayo na wataalamu wa sheria walikataa mpango wa Mungu kwao kwa kutokubali kubatizwa na Yohana.)

31 Yesu akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini?

32 Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao, wakisema:

“ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza;

tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,

lakini hamkulia.’

33 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali mkate wala hanywi divai, nanyi mkasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’

34 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’

35 Nayo hekima huthibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”