Yesu Anamponya Mtumishi wa Akida huko Kapernaumu
Hapa tunaona kuenea kwa kasi kwa ushawishi wa Kristo na swali kutoka kwa Yohana Mbatizaji akiwa gerezani.
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 8:5–13
8:5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada,
6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”
7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”
8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
9 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
10 Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”
13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.
Luka 7:1–10
7:1 Baada ya Yesu kumaliza kusema haya yote watu wakiwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu. 2 Mtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu kufa. 3 Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari.
4 Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili,
5 kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.” 6 Hivyo Yesu akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue, kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. 7 Ndiyo maana sikujiona hata ninastahili kuja kwako wewe. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.
8 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”
9 Yesu aliposikia maneno haya, alishangazwa naye sana. Akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.” 10 Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.
Yesu Anamfufua Mwana wa Mjane huko Naini
Luka 7:11–17
7:11 Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye. 12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke. 13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”
14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.” 15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.
16 Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” 17 Habari hizi za mambo aliyoyafanya Yesu zikaenea Uyahudi wote na sehemu zote za jirani.