Mahubiri ya Mlimani

Mahubiri ya Mlimani: mapendeleo na matakwa ya utawala wa Masiya, na kiwango cha haki cha Kristo.

Mahali tambarare mlimani, si mbali na Kapernaumu

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 5:1–8:1

Mahali na Wasikilizaji

5:1 Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. 2 Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:

Heri na Ole

Utangulizi: matamko ya heri na ole, mapendeleo ya watawaliwa wa Masiya.

3 “Heri walio maskini wa roho,

maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

4 Heri wale wanaohuzunika,

maana hao watafarijiwa.

5 Heri walio wapole,

maana hao watairithi nchi.

6 Heri wenye njaa na kiu ya haki,

maana hao watatoshelezwa.

7 Heri wenye huruma,

maana hao watapata rehema.

8 Heri walio na moyo safi,

maana hao watamwona Mungu.

9 Heri walio wapatanishi,

maana hao wataitwa wana wa Mungu.

10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,

maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu.

12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

Kiwango cha Haki cha Kristo

Mada ya mahubiri: kiwango cha haki cha Kristo, tofauti na kile cha waandishi na Mafarisayo.

13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

Maadili ya Kristo Yanazidi Mafundisho ya Waandishi

Mafundisho ya Kristo kuhusu maadili ni bora kuliko yale ya waandishi (Agano la Kale na sheria ya mapokeo ya mdomo), katika mambo au vielelezo sita: mauaji, uzinzi, talaka, viapo, kulipiza kisasi, na kuwapenda adui.

21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

25 “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26 Amin, nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.

27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29 Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa jehanamu. 30 Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ 32 Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.

33 “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ 34 Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; 35 au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36 Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37 ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39 Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40 Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41 Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’

44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi,

45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?

47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo?

48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Haki ya Kweli Dhidi ya Unafiki wa Kujionyesha

Kutenda haki ya kweli, tofauti na unafiki wa kujionyesha wa Mafarisayo, kama katika kuwapa wahitaji, kuomba, na kufunga.

6:1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

5 “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.

9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:

“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,

Jina lako litukuzwe.

10 Ufalme wako uje.

Mapenzi yako yafanyike

hapa duniani kama huko mbinguni.

11 Utupatie riziki yetu

ya kila siku.

12 Utusamehe deni zetu,

kama sisi nasi tulivyokwisha

kuwasamehe wadeni wetu.

13 Usitutie majaribuni,

bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu

[kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu,

na utukufu, hata milele. Amen].’

14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

16 “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. 17 Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu 18 ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri; naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

Kujitoa kwa Mungu kwa Moyo Wote

Kujitoa kwa Mungu kwa moyo wote, badala ya kufuatilia malengo na mahangaiko ya kidunia.

19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!

24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.

25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?

28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

Kutafuta Makosa, au Kuwahukumu Wengine

7:1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa. 2 Kwa maana jinsi unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa, na kwa kipimo kile upimiacho, ndicho utakachopimiwa.

3 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?

4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako,’ wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe? 5 Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.

6 “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu; wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyagakanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.

Maombi na Kanuni ya Dhahabu

7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?

12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.

Mahubiri Yanamalizika kwa Mifano ya Mafumbo Yenye Nguvu

Hitimisho la mahubiri: somo la haki ya mtu binafsi, linalosisitizwa kwa mifano ya mafumbo yenye nguvu.

13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. 14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali. 16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma? 17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.

18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.

19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.

21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba.

25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba.

26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

28 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake, 29 kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.

8:1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata.

Luka 6:17–30, 32–42, 31, 43–49

Mahali na Wasikilizaji

6:17 Akashuka pamoja nao, akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Uyahudi, kutoka Yerusalemu, na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni. 18 Walikuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya. 19 Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.

Heri na Ole

Utangulizi: matamko ya heri na ole, mapendeleo ya watawaliwa wa Masiya.

20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:

“Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,

kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu.

21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,

kwa sababu mtashibishwa.

Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,

kwa sababu mtacheka.

22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,

watakapowatenga na kuwatukana

na kulikataa jina lenu kama neno ovu,

kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

24 “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,

kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.

25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,

maana mtaona njaa.

Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,

maana mtaomboleza na kulia.

26 Ole wenu watu watakapowasifu,

kwani ndivyo baba zao walivyowasifu

manabii wa uongo.

Maadili ya Kristo Yanazidi Mafundisho ya Waandishi

Mafundisho ya Kristo kuhusu maadili ni bora kuliko yale ya waandishi (Agano la Kale na sheria ya mapokeo ya mdomo), katika mambo au vielelezo sita: mauaji, uzinzi, talaka, viapo, kulipiza kisasi, na kuwapenda adui.

27 “Lakini nawaambia ninyi mnaonisikia: Wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia.

28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya. 29 Kama mtu akikupiga shavu moja, mgeuzie na la pili pia. Mtu akikunyangʼanya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia. 30 Mpe kila akuombaye, na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie.

32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwapenda wale wawapendao.

33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo.

34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha ‘wenye dhambi’ wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote. 35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na kwa wale waovu. 36 Kuweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Kutafuta Makosa, au Kuwahukumu Wengine

37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa. 38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

39 Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni? 40 Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

41 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe?

42 Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, acha nitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako,’ wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.

Maombi na Kanuni ya Dhahabu

31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.

Mahubiri Yanamalizika kwa Mifano ya Mafumbo Yenye Nguvu

Hitimisho la mahubiri: somo la haki ya mtu binafsi, linalosisitizwa kwa mifano ya mafumbo yenye nguvu.

43 “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri.

44 Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba, wala zabibu kwenye michongoma.

45 Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo maovu kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.

46 “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia?

47 Nitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda.

48 Yeye ni kama mtu aliyejenga nyumba, akachimba chini sana, na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yaliipiga ile nyumba, lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri.

49 Lakini yeye anayesikia maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”