Yesu Anafundisha na Kuponya Makundi Makubwa ya Watu Kando ya Bahari
Yesu anafundisha na kuponya makundi makubwa ya watu kando ya Bahari ya Galilaya.
Hapa tunamwona Kristo akiwachagua mitume kumi na wawili na kuwahubiria wao pamoja na makundi ya watu Mahubiri ya Mlimani.
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 12:15–21
12:15 Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wagonjwa wao wote,
16 akiwakataza wasiseme yeye ni nani. 17 Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema:
18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua,
mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Nitaweka Roho wangu juu yake,
naye atatangaza haki kwa mataifa.
19 Hatagombana wala hatapiga kelele,
wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.
20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
na utambi unaofuka moshi hatauzima,
mpaka atakapoifanya haki ishinde.
21 Katika Jina lake mataifa
wataweka tumaini lao.”
Marko 3:7–12
3:7 Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata. 8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni. 9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.
10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”
12 Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.
Yesu Anachagua Mitume Kumi na Wawili
Baada ya usiku wa maombi, Yesu anachagua mitume kumi na wawili.
Marko 3:13–19
3:13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.
14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye, na awatume kwenda kuhubiri 15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.
16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro); 17 Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo); 18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo,
19 na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.
Luka 6:12–16
6:12 Ikawa katika siku hizo Yesu alikwenda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu.
13 Kulipopambazuka, akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume:
14 Simoni aliyemwita Petro, Andrea nduguye, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartholomayo, 15 Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Zelote,
16 Yuda mwana wa Yakobo, na Yuda Iskariote ambaye alikuwa msaliti.