Wanafunzi Wanachuma Nafaka Siku ya Sabato

Mabishano mengine kuhusu Sabato na Mafarisayo, wakati wanafunzi wanapochuma masuke ya nafaka mashambani.

Yaelekea huko Galilaya njiani kurudi kutoka Yerusalemu

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 12:1–8

12:1 Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala.

2 Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”

3 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa?

4 Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. 5 Au hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? 6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa.

7 Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia,

8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Marko 2:23–28

2:23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.

24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”

25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa, wakahitaji chakula?

26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, wakati Abiathari alikuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.”

27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.

28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Luka 6:1–5

6:1 Ikawa siku moja ya Sabato Yesu alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake.

2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?”

3 Yesu akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa?

4 Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake.”

5 Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Yesu Anauponya Mkono Uliokauka Siku ya Sabato

Mabishano ya tatu kuhusu Sabato na Mafarisayo, juu ya kuponywa kwa mtu mwenye mkono uliokauka katika sinagogi.

Huko Galilaya

Mathayo 12:9–14

12:9 Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, 10 na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”

11 Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa?

12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”

13 Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine.

14 Lakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua.

Marko 3:1–6

3:1 Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na huko palikuwa na mtu aliyepooza mkono.

2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.

3 Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”

4 Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.

5 Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa kabisa!

6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya shauri la kumuua Yesu wakiwa na Maherode.

Luka 6:6–11

6:6 Ikawa siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia ndani ya sinagogi na akawa anafundisha. Huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.

7 Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu. Kwa hivyo wakawa wanamwangalia sana ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato.

8 Lakini Yesu alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka usimame mbele ya watu wote.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.

9 Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato? Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyoosha mkono wako!” Akaunyoosha na mkono wake ukaponywa kabisa.

11 Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao ni nini watakachomtendea Yesu.