Yesu Anashtakiwa kwa Kushirikiana na Beelzebuli
Shtaka la kufuru kwamba Yesu anashirikiana na Beelzebuli.
Zingatia kwamba matukio yote yanayofuata yalitokea siku ileile, inayoitwa Siku Yenye Shughuli Nyingi.
Galilaya
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 12:22–37
12:22 Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. 23 Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”
24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo wachafu.”
25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. 26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.
28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.
29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.
30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. 31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
32 Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.
33 “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake. 34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. 35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. 36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. 37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”
Marko 3:20–30
3:20 Kisha Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula. 21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”
22 Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Anatoa pepo wachafu kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu!”
23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24 Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.
25 Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia.
27 Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali zake.
28 Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa. 29 Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”
30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”
Waandishi na Mafarisayo Wanadai Ishara
Siku ileile. Galilaya
Mathayo 12:38–45
12:38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”
39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. 41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”
43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. 44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri. 45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”
Mama na Ndugu wa Kristo Wanatafuta Kumpeleka Nyumbani
Siku ileile. Galilaya
Mathayo 12:46–50
12:46 Wakati alikuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye.
47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”
48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?”
49 Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu!
50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”
Marko 3:31–35
3:31 Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakasimama nje, wakamtuma mtu kumwita.
32 Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”
33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”
34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.
35 Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”
Luka 8:19–21
8:19 Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu.
20 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”
21 Yesu akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulifanya.”