Kundi Kubwa la Kwanza la Mifano

Hapa tuna kundi kubwa la kwanza la mifano, pamoja na ziara huko Gerasa na kurudi Nazareti.

Siku hiyohiyo. Kando ya Bahari ya Galilaya

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 13:1–53

Utangulizi wa Kundi la Mifano

13:1 Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari.

2 Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari.

3 Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

Mfano wa Mpanzi

Kwa makutano kando ya bahari: mfano wa mpanzi.

4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.

5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba.

6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini.

9 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

10 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

11 Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao hawajapewa.

12 Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. 13 Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano:

“Ingawa wanatazama, hawaoni;

wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi.

14 Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema:

“ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa;

na pia mtatazama lakini hamtaona.

15 Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu;

hawasikii kwa masikio yao,

na wamefumba macho yao.

Wasije wakaona kwa macho yao,

na wakasikiliza kwa masikio yao,

wakaelewa kwa mioyo yao,

na kugeuka nami nikawaponya.’

16 Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. 17 Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.

18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: 19 Mtu yeyote anaposikia neno la Ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia.

20 Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha.

21 Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye mara huchukizwa.

22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.

23 Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

Mfano wa Magugu

24 Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25 Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26 Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.

27 “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’

28 “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’

“Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’

29 “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. 30 Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”

Mfano wa Mbegu ya Haradali

31 Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. 32 Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.”

Mfano wa Chachu na Mifano Mingine Mingi Kama Huo

33 Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.”

34 Yesu alinena mambo haya yote kwa makutano kwa mifano. Wala hakuwaambia lolote pasipo mfano.

35 Hii ilikuwa ili kutimiza lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii aliposema:

“Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano;

nitahubiri mambo yaliyofichika

tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.”

Yesu Anafafanua Mfano wa Magugu

Kwa wanafunzi ndani ya nyumba: ufafanuzi wa mfano wa magugu.

36 Kisha Yesu akaagana na makutano, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”

37 Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. 38 Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. 39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.

40 “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

Mfano wa Hazina Iliyofichwa

44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

Mfano wa Lulu ya Thamani

45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

Mfano wa Wavu

47 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. 48 Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. 49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

Mfano wa Mwenye Nyumba

51 Yesu akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?”

Wakamjibu, “Ndiyo.”

52 Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”

53 Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka.

Marko 4:1–34

Utangulizi wa Kundi la Mifano

4:1 Yesu akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Umati wa watu uliokuwa umekusanyika kumzunguka ulikuwa mkubwa, kiasi kwamba ilimbidi Yesu aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari.

2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema:

Mfano wa Mpanzi

Kwa makutano kando ya bahari: mfano wa mpanzi.

3 “Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.

5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba.

6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”

9 Kisha Yesu akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

10 Alipokuwa peke yake, watu waliokuwepo naye pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili wakamuuliza kuhusu mifano yake.

11 Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa kujua siri ya Ufalme wa Mungu. Lakini kwa wale walioko nje, kila kitu husemwa kwao kwa mifano,

12 ili,

“ ‘daima waone lakini wasitambue,

daima wasikie lakini wasielewe;

wasije wakageuka, wakatubu na kusamehewa!’ ”

13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine? 14 Yule mpanzi hupanda neno.

15 Hawa ndio wale walio kando ya njia ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulinyakua lile neno lililopandwa ndani yao. 16 Nazo zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, ni wale wanaolisikia neno, na mara hulipokea kwa furaha.

17 Lakini kwa kuwa hawana mizizi, wao hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, mara wao huiacha imani.

18 Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno; 19 lakini masumbufu ya maisha haya, na udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae.

20 Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kuzaa mazao. Wao huzaa mara thelathini, au mara sitini, au mara mia ya mbegu iliyopandwa.”

21 Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake?

22 Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lolote la siri ambalo halitaletwa nuruni.

23 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

24 Naye akawaambia, “Kuweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa ninyi, hata na zaidi. 25 Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa.”

Mfano wa Mbegu Inayoota Yenyewe

26 Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani. 27 Akiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo. 28 Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke. 29 Lakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia, maana mavuno yamekuwa tayari.”

Mfano wa Mbegu ya Haradali

30 Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza? 31 Ni kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini. 32 Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani wanaweza kujenga viota kwenye matawi yake.”

Mfano wa Chachu na Mifano Mingine Mingi Kama Huo

33 Kwa mifano mingine mingi kama hii Yesu alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa.

34 Hakusema nao neno lolote pasipo mfano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Luka 8:4–18

Utangulizi wa Kundi la Mifano

8:4 Umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka kila mji, akawaambia mfano huu:

Mfano wa Mpanzi

Kwa makutano kando ya bahari: mfano wa mpanzi.

5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila.

6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu.

7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.”

Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

9 Wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano huo.

10 Naye akasema, “Ninyi mmepewa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili,

“ ‘ingawa wanatazama, wasione;

ingawa wanasikiliza, wasielewe.’

11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu.

12 Zile zilizoanguka kando ya njia ni wale ambao husikia neno, naye ibilisi anakuja na kuliondoa neno kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka.

13 Zile mbegu zilizoanguka kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa muda mfupi, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.

14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.

15 Lakini zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu wa utiifu, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

16 “Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga.

17 Kwa maana hakuna jambo lolote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lolote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi.

18 Kwa hiyo, kuweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa zaidi. Lakini yule asiye na kitu, hata kile anachodhani anacho atanyangʼanywa.”