Yesu Anatuliza Dhoruba Anapovuka Ziwa

Siku hiyohiyo. Bahari ya Galilaya

27 hadi 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 8:18, 23–27

8:18 Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ngʼambo ya ziwa.

23 Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata.

24 Ghafula, kukainuka dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi.

25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.

27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

Marko 4:35–41

4:35 Siku hiyo ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo.”

36 Wakauacha ule umati wa watu, na wakamchukua vile alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye.

37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji.

38 Yesu alikuwa katika shetri, akiwa analala juu ya mto. Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

Luka 8:22–25

8:22 Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Tuvukeni twende mpaka ngʼambo ya ziwa.” Nao wakaondoka.

23 Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.

24 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!”

Yeye akaamka, akaukemea ule upepo na yale mawimbi; dhoruba ikakoma, nako kukawa shwari.

25 Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?”

Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni nani, ambaye anaamuru hata upepo na maji, navyo vikamtii?”

Yesu Anamponya Mgerasi Mwenye Pepo

Ng'ambo ya ziwa, Yesu anamponya mtu mwenye pepo wa Wagerasi.

Gerasa (Kursi). Siku hiyo hiyo

Mathayo 8:28–34

8:28 Walipofika ngʼambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile.

29 Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”

30 Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha.

31 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.”

32 Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji.

33 Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.

34 Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.

Marko 5:1–20

5:1 Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika nchi ya Wagerasi.

2 Yesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye. 3 Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo. 4 Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. 5 Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.

6 Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake.

7 Akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!”

8 Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”

9 Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tuko wengi.”

10 Akamsihi Yesu sana asiwapeleke nje ya nchi ile.

11 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima.

12 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.”

13 Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.

14 Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia.

15 Walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu legioni akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa.

16 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia.

17 Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.

18 Yesu alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Yesu waende pamoja. 19 Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokuhurumia.” 20 Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Yesu aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.

Luka 8:26–39

8:26 Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, ambayo iko upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya.

27 Yesu aliposhuka kutoka mashua na kukanyaga ufuoni, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali aliishi makaburini.

28 Alipomwona Yesu, alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!”

29 Wakati huo Yesu alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa, na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi, alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.

30 Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Legioni,” kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.

31 Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda katika Shimo.

32 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo likilisha kando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu.

33 Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremkia gengeni kwa kasi, likatumbukia ziwani na kuzama.

34 Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani.

35 Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Yesu, wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Yesu, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa.

36 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa.

37 Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Yesu aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua, akaondoka zake.

38 Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Yesu afuatane naye, lakini Yesu akamuaga, akamwambia: 39 “Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu ambayo Yesu alimtendea.