Binti ya Yairo na Mwanamke Anayegusa Vazi la Kristo
Anaporudi, Yesu anamponya binti ya Yairo, na mwanamke aliyegusa tu vazi la Kristo.
Yaelekea Kapernaumu
27 hadi 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 9:18–26
9:18 Yesu alipokuwa akiwaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye atakuwa hai.”
19 Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.
20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake,
21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”
22 Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.
23 Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele,
24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. 25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka.
26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.
Marko 5:21–43
5:21 Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ngʼambo, umati mkubwa wa watu ukamzunguka yeye akiwa hapo kando ya bahari.
22 Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Yesu, akapiga magoti miguuni pake, 23 akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye atakuwa hai.”
24 Hivyo Yesu akaenda pamoja naye.
Umati mkubwa wa watu ukamfuata, nao watu wakawa wanamsonga.
25 Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26 Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya.
27 Alikuwa amesikia habari za Yesu, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28 kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitaponywa.” 29 Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.
30 Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”
31 Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”
32 Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa.
33 Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote.
34 Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
35 Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
36 Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37 Hakumruhusu mtu mwingine yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.
38 Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa.
39 Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.”
40 Wale watu wakamcheka kwa dharau.
Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto.
41 Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake ni, “Msichana, nakuambia: amka!”)
42 Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43 Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.
Luka 8:40–56
8:40 Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea.
41 Kisha mtu mmoja, jina lake Yairo, aliyekuwa kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake,
42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.
Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.
43 Katika umati huo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa na tatizo la kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna yeyote aliyeweza kumponya.
44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma ya Yesu na kugusa upindo wa vazi lake. Mara kutokwa damu kwake kukakoma.
45 Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”
Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”
46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”
47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu. Akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara.
48 Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”
49 Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”
50 Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope. Amini tu, naye binti yako atapona.”
51 Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu yeyote aingie ndani naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, pamoja na baba na mama wa yule binti.
52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa, ila amelala.”
53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa.
54 Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!”
55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara moja. Akaamuru apewe kitu cha kula. 56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote juu ya yale yaliyotukia.
Yesu Anawaponya Wanaume Wawili Vipofu na Mwanaume Bubu
Yesu anawaponya wanaume wawili vipofu na mwanaume bubu aliyepagawa na pepo, na anakabiliwa na shtaka lenye kukufuru.
Mathayo 9:27–34
9:27 Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”
28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”
Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”
29 Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” 31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.
32 Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu. 33 Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”
34 Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”
Yesu Anatembelea Nazareti kwa Mara ya Mwisho
Mathayo 13:54–58
13:54 Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?”
55 “Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Maria, nao ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?”
57 Wakachukizwa naye.
Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”
58 Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Marko 6:1–6
6:1 Yesu akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiwa amefuatana na wanafunzi wake. 2 Ilipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.
Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!
3 Huyu si yule seremala, mwana wa Maria? Na ndugu zake si Yakobo, Yose, Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini.
4 Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani kwake.” 5 Hakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya.
6 Naye akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani.
Kisha Yesu akawa anakwenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha.