Kwa Nini Paulo Anahubiri kwa Bidii Sana

Akijua hofu ya hukumu inayokuja, Paulo alizidi kuwa na bidii katika kuhubiri injili na kuwashawishi watu wawe Wakristo. Anatimiza wajibu wake akiwa wazi mbele za Mungu na, kama alivyotumaini, akiwa wazi pia katika dhamiri za Wakorintho. Kisha anajitetea dhidi ya mashambulizi ya walimu wa uongo, ili wale aliowaongoa wawe na sababu za kujivunia yeye kama mtume. Anatangaza kwamba iwe alihubiri injili akihatarisha maisha yake, na hivyo kuonwa kuwa mwenye wazimu na kundi lililompinga, au alitenda kwa busara kwa kuepuka mateso, yote yalikuwa kwa ajili ya wanafunzi wake.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wakorintho 5:11–15

11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Bwana, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia. 12 Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu mweze kuwajibu hao wanaoona fahari juu ya mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni. 13 Kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu. 14 Kwa kuwa upendo wa Kristo unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa. 15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.

Kiumbe Kipya, Aliyepatanishwa na Mungu

Kutokana na ukweli kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya wanadamu wote, Paulo anaendelea kueleza kwamba tangu sasa hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, kwa maana Kristo haangaliwi tena kama Myahudi kwa jinsi ya mwili. Wote wanaounganishwa na Kristo kwa imani huwa viumbe vipya, na mazoea yao ya zamani na yenye dhambi yamekoma. Faida na baraka za hali hii mpya hutoka kwa Mungu pekee, ambaye ameupatanisha ulimwengu na nafsi yake kwa njia ya Kristo Yesu na amewakabidhi mitume ujumbe wa upatanisho. Paulo, kwa niaba ya Kristo, anawahimiza watu wote wamjie Mungu na kukubali msamaha walionunuliwa kwa njia ya kafara ya upatanisho ya Mwana wake, ambaye alifanywa kuwa dhabihu ya dhambi kwa ajili ya wanadamu.

2 Wakorintho 5:16–21

16 Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Kristo kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo. 17 Kwa hiyo kama mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kwa njia ya Yesu Kristo na kutupata sisi huduma ya upatanisho: 19 Kwamba Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kwake yeye.

Alama za Mhudumu Mwaminifu

Akiwa balozi wa Kristo, Paulo anawasihi Wakorintho wasiipokee neema ya Mungu bure, bali wafanye yote ambayo injili inawataka kufanya. Kwa kueleza mateso yake mwenyewe, Paulo anaonyesha jinsi mtumishi mwaminifu wa injili alivyo, na hivyo anathibitisha kwamba mwalimu wa uongo yuko chini yake.

2 Wakorintho 6:1–10

1 Kama watendakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msipokee neema ya Mungu bure. 2 Kwa maana asema:

“Wakati wangu uliokubalika nilikusikia,

siku ya wokovu nilikusaidia.”

Tazama, wakati uliokubalika ndio huu, siku ya wokovu ndiyo sasa.

3 Hatuweki kitu cha kukwaza katika njia ya mtu yeyote, ili huduma yetu isionekane kuwa na lawama. 4 Bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida; 5 katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga; 6 katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, na katika utu wema; katika Roho Mtakatifu na upendo wa kweli; 7 katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu, kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; 8 katika utukufu na katika kudharauliwa; katika sifa mbaya na katika sifa nzuri; tukiwa kama wadanganyaji, lakini tukiwa wakweli; 9 tukiwa maarufu, lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana; tukiwa kama wanaokufa, lakini tunaishi; tukipigwa, lakini hatuuawi; 10 tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.

Paulo Anakataza Uhusiano wa Karibu na Wasioamini

Paulo anaeleza upendo wake mkuu na mapenzi yake kwa Wakorintho. Anawakemea kwa kukosa upendo, na kuwasihi, kama watoto wake, wamfungulie mioyo yao kikamilifu akiwa baba yao wa kiroho. Anawakataza kuoana na wasioamini, kufanya urafiki nao, au kuingia katika uhusiano wowote wa karibu nao. Ahadi ya Mungu kwa wale wanaojitenga na miungano hiyo isiyo mitakatifu inapaswa kuwa kichocheo chao kikuu cha kujitahidi kufikia ukamilifu.

2 Wakorintho 6:11–7:1

11 Tumesema nanyi wazi, enyi Wakorintho na kuwafungulieni mioyo yetu wazi kabisa. 12 Sisi hatujizuii kuwapenda, bali ninyi mmeuzuia upendo wenu kwetu. 13 Sasa nasema, kama na watoto wangu: Ninyi pia ifungueni mioyo yenu kabisa.

14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza? 15 Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari? Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini? 16 Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”

17 “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao,

mkatengwe nao,

asema Bwana.

Msiguse kitu chochote kilicho najisi,

nami nitawakaribisha.”

18 “Mimi nitakuwa Baba kwenu,

nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu,

asema Bwana Mwenyezi.”

7:1 Wapenzi, kwa kuwa tunazo ahadi hizi, basi na tujitakase nafsi zetu kutokana na kila kitu kitiacho mwili na roho unajisi, tukitimiza utakatifu kwa kumcha Mungu.

Paulo Anaomba Apokewe Kama Mtume

Paulo anawasihi Wakorintho wamtambue kuwa mtume, na kwa kutaja sababu zinazostahili kuwafanya wampende, anadokeza mwenendo wa kinyume wa mwalimu wa uongo. Anawahakikishia kwamba hasemi haya ili awahukumu, bali kwa upendo mkuu sana alio nao kwao. Anafurahia moyo wao mwema na utii wao.

2 Wakorintho 7:2–4

2 Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote. 3 Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo, kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja. 4 Mara nyingi najivuna kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.

Furaha ya Paulo kwa Habari Anazoleta Tito

Kama uthibitisho wa upendo wake, Paulo anawaambia Wakorintho kuhusu wasiwasi wake juu yao, akihofia kwamba mwalimu wa uongo alikuwa amewapotosha. Anasimulia furaha yake wakati Tito alipofika na habari za utii na upendo wao. Anazungumza nao kuhusu barua yake ya kwanza, na kuwahakikishia kwamba aliagiza yule mtu aliyefanya uasherati na jamaa yake wa karibu atengwe na kanisa ili kuonyesha jinsi alivyowajali sana. Anasifu utii wao, bidii yao, na toba yao. Anasimulia faraja aliyoipata kutokana na mwenendo wao, na furaha ya Tito alipoona umoja na utii wao.

2 Wakorintho 7:5–16

5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na raha. Tulisumbuliwa kila upande, kwa nje kulikuwa na mapigano na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu. 6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito. 7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.

8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu, 9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.

10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti. 11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo. 12 Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu. 13 Kwa ajili ya haya tumefarijika.

Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote. 14 Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kila kitu tulichowaambia ninyi, kilikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia. 15 Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, na kumpokea kwa hofu na kutetemeka. 16 Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.