Paulo Anahimiza Utoaji wa Ukarimu kwa Ajili ya Uyahudi

Kwa mfano wa makanisa ya Makedonia, yaliyokuwa katika hali ngumu sana, Paulo anawahimiza Wakorintho kutoa kwa ukarimu ili kuwasaidia ndugu Wakristo wa Uyahudi. Anasema kwamba hasemi hayo kama amri, kwa sababu matendo ya fadhili yanapaswa kuwa ya hiari, lakini anatumaini kwamba watazidi kuyatenda kwa kufuata mfano wa Kristo na upendo wake. Anawataka wakamilishe bila kukawia michango ambayo tayari wameanza, kulingana na uwezo wao, kwa kuwa Mungu anathamini utayari wa mtoaji kuliko ukubwa wa zawadi. Wanachotoa kitatumiwa kwa ajili ya ndugu maskini wa Uyahudi tu, ambao nao huenda wakaweza kutimiza mahitaji ya Wakorintho.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wakorintho 8:1–15

1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia. 2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu. 3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe, 4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu. 5 Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu. 6 Kwa hiyo tulimsihi Tito, kwa kuwa ndiye alianzisha jambo hili, akamilishe tendo hili la neema kwa upande wenu. 7 Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.

8 Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine. 9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

10 Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo. 11 Sasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu. 12 Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.

13 Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano. 14 Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu. 15 Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”

Tito na Ndugu Wawili Watumwa Korintho

Paulo anamshukuru Mungu kwa kumfanya Tito awajali kama yeye mwenyewe anavyowajali. Shauku ya Tito ilimfanya apeleke barua hii. Paulo anawaambia kwamba pamoja na Tito anamtuma ndugu mwenye sifa nzuri sana, aliyechaguliwa na makanisa ya Wamakedonia kuwa shahidi wa jinsi zawadi zao zilivyosimamiwa, ili kusiwe na shaka yoyote inayoweza kusababisha lawama kuhusu jinsi kiasi kikubwa cha fedha walichokabidhiwa kilivyotumika. Mfanyakazi mwenzao mwingine pia anatumwa, ambaye ana shauku kubwa isivyo kawaida katika tukio hili kwa sababu ya habari alizopata kuhusu moyo wao mzuri. Paulo anawaelekeza jinsi ya kujibu maswali ya kikundi kinachojitenga, na anawahimiza wawape wajumbe hawa na makanisa uthibitisho wa upendo wao na wa imani ambayo Paulo anayo kwao.

2 Wakorintho 8:16–24

16 Ninamshukuru Mungu ambaye amemtia Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali. 17 Si kwamba Tito amekubali tu ombi letu, bali anakuja kwenu akiwa na shauku kuliko wakati mwingine, tena kwa hiari yake mwenyewe. 18 Nasi tunamtuma pamoja naye ndugu ambaye anasifiwa na makanisa yote kwa huduma yake ya kuhubiri Injili. 19 Zaidi ya hayo, alichaguliwa na makanisa ili asafiri pamoja nasi tulipokuwa tunapeleka matoleo ya ukarimu, kwa ajili ya utukufu wa Bwana mwenyewe, na ili kuonyesha hisani yetu kuwasaidia. 20 Tunataka kuepuka lawama yoyote kuhusu jinsi tunavyosimamia matoleo haya ya ukarimu. 21 Kwa kuwa tunakusudia kufanya kile kilicho haki si machoni mwa Bwana peke yake, bali pia machoni mwa watu wengine.

22 Pamoja nao, tunamtuma ndugu yetu ambaye mara kwa mara ametuthibitishia kwa njia nyingi kwamba ana shauku, naam, zaidi sana sasa kwa sababu analo tumaini kuu kwenu. 23 Kwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtendakazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makanisa, na utukufu kwa Kristo. 24 Kwa hiyo waonyesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, mbele ya makanisa, ili yapate kuona.

Tito Atumwa Mapema Kuandaa Mchango

Paulo anaendelea kuwakumbusha Wakorintho kwamba alikuwa amejivunia utayari wao kwa watu wa Makedonia mwaka mmoja uliopita. Tangu wakati huo, baada ya kujulishwa na Tito kwamba walikuwa wamezembea katika jambo hili, anawatuma Tito na wenzake waandae michango kabla hajafika, ili asione aibu kwa kujivunia kwake juu yao, na ili walichotoa kitolewe kwa hiari, si kana kwamba kililazimishwa kutoka kwa watu wenye uchoyo.

2 Wakorintho 9:1–5

1 Hakuna haja yangu kuwaandikia kuhusu huduma hii itolewayo kwa ajili ya watakatifu. 2 Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa watu wa Makedonia, nikiwaambia kuwa ninyi wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa. 3 Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari. 4 Kwa maana kama nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamjawa tayari, tutaona aibu kusema chochote juu yenu katika matoleo. 5 Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu.

Pandeni kwa Ukarimu, Toeni kwa Furaha

Paulo anawahimiza Wakorintho wawe wakarimu, kwa kuwa tutathawabishwa katika ulimwengu mwingine kulingana na matendo yetu hapa. Anawahimiza watoe kwa furaha. Mungu ana uwezo wa kubariki kazi zao na kuwapa mali za ulimwengu huu za kutosha, kwa ajili ya mahitaji yao wenyewe na kwa ajili ya matendo yao ya hisani. Wale wanaosaidiwa hufurahi, humshukuru Mungu, na kuwaombea wale waliotoa.

2 Wakorintho 9:6–15

6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. 8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. 9 Kama ilivyoandikwa:

“Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

akawapa maskini;

haki yake hudumu milele.”

10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. 11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu. 13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote. 14 Nao katika maombi yao kwenu mioyo yao itawaonea shauku kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu. 15 Ashukuriwe Mungu kwa karama yake isiyoelezeka.

Paulo Anaonya Kwamba Anaweza Kuwa Jasiri Akiwapo

Sasa Paulo anamzungumzia hasa mwalimu wa uongo na wafuasi wake, ambao walikuwa wamemchongea kwa kusema kwamba alikuwa mpole tu alipokuwa pamoja nao, lakini jasiri katika barua zake alipokuwa mbali. Ingawa yuko mbali, sasa anawasihi kwa kinaya wale wanaomshtaki kuwa anaishi kwa kufuata mwili wasimpe sababu ya kuthibitisha ujasiri wake atakapokuwa pamoja nao. Anatangaza nguvu za ajabu ambazo Mungu alimpa za kubomoa kila kitu kinachopinga injili, na anasisitiza kwamba alikuwa tayari kuonyesha nguvu zake za kufanya miujiza ili kuadhibu kutotii, mara tu utii wa wale waliotubu miongoni mwao utakapokuwa umetimia.

2 Wakorintho 10:1–6

1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! 2 Nawaomba nitakapokuja kwenu nisiwe na ujasiri dhidi ya watu fulani, kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata namna ya ulimwengu huu. 3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo, 6 tena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, kutii kwenu kutakapokamilika.