Paulo Anakemea Kuhukumu kwa Mwonekano wa Nje
Paulo anamkaripia mwalimu wa uongo kwa kuhukumu kwa mwonekano wa nje. Pia anaomba atambuliwe kuwa mtumishi wa Kristo, na anajivunia uwezo aliopewa kwa ajili ya kuwajenga. Kwa mara nyingine anataja kwa kejeli taarifa za kashfa za mpinzani wake, na kumtaka ahitimishe, kutokana na matokeo ya uwezo wa Paulo yaliyokuwa tayari yameonekana alipokuwa hayupo katika kuadhibiwa kwa yule mtu aliyefanya uasherati na jamaa yake wa karibu, kwamba uwezo huo ungekuwa mkubwa vivyo hivyo atakapokuwepo.
58 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
7 Angalieni yale yaliyo machoni penu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Kristo, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Kristo, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. 8 Basi hata kama nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana alitupa ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya. 9 Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. 10 Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni dhaifu na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” 11 Watu kama hao wajue ya kuwa, yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi, ndivyo tulivyo na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.
Kujisifu Ndani ya Mipaka Anayoweka Mungu
Akiendelea kutumia kejeli, Paulo anasema kwamba hathubutu kujilinganisha na mwalimu wa uongo, ambaye hujipima kwa kujitumia mwenyewe tu kama kipimo na kujisifu kwa yale aliyoyafanya huko Korintho. Paulo, kinyume chake, anataka tu kufurahi ndani ya mipaka ambayo Mungu alimwekea, naye kwa kuitii alikuwa sasa amewafikia Wakorintho. Anakataa kujisifu kwa kazi za watu wengine kama anavyofanya mwalimu wa uongo, na anatumaini kuhubiri injili katika nchi ambako haijawahi kuhubiriwa. Kwa maana anayekubaliwa si yule anayejivunia kazi za wengine, bali yule anayehubiri kwa utukufu wa Mungu na kupokea sifa kutoka kwa Mungu, zinazoonekana kupitia karama za Roho.
12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara. 13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. 14 Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama vile ambavyo ingekuwa kama hatukuwa tumekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Kristo. 15 Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, 16 ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. 17 Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.” 18 Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Bwana humsifu.
Paulo Anaogopa Kwamba Wakorintho Wanapotoshwa
Akishtakiwa kwa kujisifu, Paulo anawasihi Wakorintho wamvumilie kwa jambo hilo wakati huu, kwa sababu anaogopa kwamba wale aliowavuta kwa Kristo, ambao alitamani kuwawasilisha wakati wa hukumu kama bikira safi kwa mume waliyeahidiwa, wamevutwa kutoka kwake na mwalimu wa uongo. Anatoa hoja kwamba kama huyo anayeitwa mtume wao angewahubiria Mwokozi mwingine au injili nyingine, au kuwapa Roho mwingine, wangeweza kuvumilia madai yake. Anathibitisha kwamba yeye ni sawa na walio wakuu kati ya mitume wa Kristo, na kwamba, ingawa hana ustadi wa kuzungumza, amewaonyesha kwamba hakukosa maarifa anayohitaji mtumishi wa injili.
1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo. 2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi. 3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo. 4 Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi. 5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.” 6 Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.
Kwa Nini Paulo Hakupokea Malipo Kutoka Korintho
Paulo anaeleza kwa nini hakukubali msaada wa mahitaji yake kutoka kwa Wakorintho. Anasema kwamba sababu haikuwa ukosefu wa wema, kama maadui zake walivyodokeza, bali upendo wake kwao, na kumzuia mwalimu wa uongo kudai kwamba Paulo alifanya kazi kwa ajili ya faida ya kidunia. Pia alikusudia kumlazimisha mwalimu wa uongo, aliyepokea zawadi kwa siri, kuacha tabia hiyo na kufuata mfano wa Paulo. Kwa kuwa Shetani mwenyewe anajifanya aonekane kama malaika wa nuru, haipaswi kushangaza kwamba watumishi wa Shetani wanajipa cheo cha watumishi au mitume wa Kristo.
7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo? 8 Niliyanyangʼanya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi. 9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia. 10 Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili. 11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda! 12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.
13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo. 14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.
Paulo Anajivunia Kazi na Mateso Yake
Paulo anawasihi tena Wakorintho wavumilie kujisifu kwake. Kwa kuwa wale ambao si mitume wanajisifu kwa mambo ya mwili, yeye pia lazima ajisifu kwa kutahiriwa kwake na asili yake ya Kiyahudi ili kutetea hadhi yake kama mtume. Anaonyesha kwamba Wakorintho walikuwa wamevumilia kupita kiasi kutawaliwa na wengine, na anaeleza jinsi mwalimu wa uongo alivyowatendea. Dhidi ya shtaka kwamba alikuwa mtu wa hali ya chini kwa kuzaliwa, dhaifu, na asiyefaa kuwa mtume, anathibitisha kwamba ikiwa yeyote alikuwa na sababu ya kujisifu, yeye pia alikuwa nayo. Anajilinganisha katika mambo haya na mwalimu wa uongo, na anaonyesha ubora wake mwenyewe kwa kutaja taabu na mateso yake, pamoja na kujali kwake sana makanisa na watu binafsi, akiwahurumia walio dhaifu na kufanya kazi kwa bidii ili kuwarejesha waliopotoshwa. Anajisifu katika udhaifu wake, hasa katika kutoroka kwake kutoka Dameski, ili nguvu za Mungu zionekane.
16 Nasema tena, mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. 17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga. 18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. 19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! 20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyangʼanya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya. 21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!
Lakini chochote ambacho mtu mwingine yeyote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo. 22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu. 23 Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. 24 Mara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja. 25 Mara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa, 26 katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. 27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. 28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote. 29 Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?
30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu. 31 Mungu na Baba wa Bwana Yesu, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. 32 Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. 33 Lakini nilishushwa kwa kapu kubwa kupitia katika dirisha ukutani, nikatoroka kutoka mikononi mwake.