Maono na Mafunuo ya Paulo
Paulo anasema kwamba, akilazimika kujisifu kwa ajili yao, atajisifu kuhusu mafunuo na maono aliyopokea. Kwa upande wake mwenyewe, ameazimia kujisifu kuhusu udhaifu na mateso yake tu. Ingawa angeweza kujisifu kwa kusema ukweli mtupu, anajizuia ili mtu yeyote asimwone kuwa mkuu kuliko alivyo.
58 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Yanipasa nijisifu, ingawa haifaidi kitu. Nitaenda kwenye maono na ufunuo kutoka kwa Bwana. 2 Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. 3 Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, 4 alinyakuliwa hadi Paradiso. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia. 5 Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu kuhusu mimi mwenyewe ila mimi nitajisifia udhaifu wangu. 6 Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema.
Uwezo wa Mungu Unakamilishwa Katika Udhaifu
Paulo anathibitisha kwamba ugonjwa wake wa mwili, ambao lile kundi lilimshutumu kwa sababu yake, ulitumwa na Mungu ili asijikweze kupita kiasi kwa sababu ya mafunuo matukufu aliyopewa. Ugonjwa huo hautaondolewa, kwa sababu nguvu za Mungu zinakamilishwa kupitia udhaifu wake. Kwa sababu hiyo anafurahia dhuluma anazopata kwa ajili ya imani, udhaifu, na mambo kama hayo, kwa maana kadiri anavyokuwa dhaifu, ndivyo neema ya Mungu inayokaa ndani yake inavyompa nguvu. Mwenendo wa Wakorintho umemlazimisha kujisifu kinyume cha mapenzi yake. Walipaswa kuutetea utume wake, wakijua kwamba hakuwa duni kwa namna yoyote kuliko mitume walio wakuu zaidi.
7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. 8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. 9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.
11 Nimekuwa mjinga, lakini ninyi mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora,” ingawa mimi si kitu.
Ziara Ijayo ya Paulo na Hofu Zake
Paulo anaendelea kuthibitisha utume wake kwa miujiza yake na karama za kiroho alizowapa. Anawauliza ni kwa namna gani aliwafanya kuwa duni kuliko makanisa mengine, isipokuwa kwamba yeye mwenyewe hakuwa mzigo kwao. Anasema kwamba anakusudia kuwatembelea na bado hatakuwa mzigo, kwa maana akiwa baba yao wa kiroho hatafuti mali za watoto wake wa kiroho bali wokovu wao. Anakanusha madokezo ya wapinzani wake kwamba alikataa kwa hila kuchukua fedha kutoka kwao, kwa kutaja mwenendo usio na ubinafsi wa Tito na msaidizi wake. Anathibitisha kwamba alimtuma Tito kwao si kama kisingizio cha kutokuja mwenyewe (2 Wakorintho 1:23), bali kuwapa wasiotii muda wa kurekebisha maisha yao. Anaogopa kwamba atakapowatembelea italazimu awahuzunikie na kuwaadhibu wale ambao hawajatubu dhambi na mambo machafu waliyofanya.
12 Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani, ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi. 13 Je, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili!
14 Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara hii ya tatu, nami sitawalemea, kwa sababu sitahitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi, kwa kuwa hata hivyo watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. 15 Hivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Hata ingawa inaonekana ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua. 16 Iwe iwavyo, kwa vyovyote vile mimi sikuwalemea. Lakini kwa mimi kuwa mwerevu naliwapata. 17 Je, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu? 18 Nilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatuenendi kwa roho moja, na hatuchukui hatua zile zile?
19 Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Kristo. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu. 20 Kwa kuwa nina hofu ya kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko. 21 Nina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.
Paulo Hatawaachilia Wale Wanaotenda Dhambi
Paulo anaendelea kuwahakikishia Wakorintho kwamba atakapowatembelea tena watahukumiwa, kulingana na Sheria na injili, kwa ushuhuda wa mashahidi wawili au watatu. Anawakumbusha onyo lake la awali na adhabu ya yule mwanamume aliyefanya uasherati na jamaa yake. Anawahakikishia wote ambao tayari wametenda dhambi, na wote wanaoendelea kutenda dhambi, kwamba hatawaachilia wao pia, hasa kwa kuwa wanadai uthibitisho kwamba Kristo anasema kupitia kwake; Kristo tayari amejidhihirisha kupitia Paulo, si kwa udhaifu bali kwa nguvu, kwa matendo makuu ambayo amemwezesha kufanya. Kristo, ingawa alisulubiwa katika udhaifu wa asili yake ya kibinadamu, bado anaishi kwa nguvu za Mungu. Sisi pia ni dhaifu kimwili pamoja naye, lakini Paulo ataonyesha kwamba wanaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu, zinazodhihirishwa katika adhabu yao.
1 Hii ndiyo mara ya tatu mimi kuja kwenu. “Shtaka lolote lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu.” 2 Nimekwisha kuwaonya nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili. Sasa narudia wakati sipo, kwamba nikija tena sitawahurumia wale waliokuwa wametenda dhambi hapo awali na wengine wote, 3 kwa kuwa mnadai uthibitisho kwamba Kristo anazungumza kwa kunitumia mimi. Yeye si dhaifu katika kushughulika nanyi, bali ana nguvu kati yenu. 4 Kwa kuwa alisulubiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Vivyo hivyo, sisi tu dhaifu kupitia kwake, lakini katika kuwashughulikia ninyi tutaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu.
Wakorintho Wanaambiwa Wajichunguze
Kwa kuwa kundi hilo lilitaka uthibitisho kwamba Kristo alikuwa pamoja na Paulo, sasa anawataka wajichunguze wenyewe waone kama wana karama za kiroho zinazothibitisha kuwapo kwa Kristo. Anatumaini kwamba, hata kama hawatakuwa na uthibitisho huo, yeye hatakutwa amepungukiwa na nguvu zisizo za kawaida, ikiwa atahitaji kuzitumia kuwaadhibu atakapokuja. Anamwomba Mungu kwamba watende yaliyo sawa, akitamani zaidi watubu kuliko kupata nafasi ya kutumia uthibitisho wake na kuonyesha nguvu zake. Anathibitisha kwamba nguvu zisizo za kawaida zinaweza kutumiwa tu kuunga mkono ukweli. Paulo anaandika mambo haya ili wafikie ukamilifu, kusudi atakapokuwa pamoja nao asilazimike kutumia kwa ukali nguvu za kimiujiza alizopewa kwa ajili ya kulijenga kanisa.
5 Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho! 6 Natumaini mtaona kuwa sisi hatukushindwa. 7 Lakini tunamwomba Mungu msije mkatenda kosa lolote, si ili sisi tuonekane kuwa tumeshinda hilo jaribio, bali ili ninyi mtende lililo haki, hata kama tutaonekana kuwa tumeshindwa. 8 Kwa maana hatuwezi kufanya lolote kinyume na kweli, bali kuithibitisha kweli tu. 9 Tunafurahi wakati wowote sisi tunapokuwa dhaifu, lakini ninyi mkawa na nguvu. Nayo maombi yetu ni kwamba mpate kuwa wakamilifu. 10 Hii ndiyo sababu nawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa.
Maneno ya Kuaga na Baraka ya Paulo
Baada ya kumaliza kulikemea lile kundi, Paulo anazungumza na kanisa lote na kuwapa maelekezo mbalimbali. Anamalizia kwa salamu na baraka yake kama mtume.
11 Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, mkafarijike, kuweni wa nia moja, kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.
12 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu. 13 Watakatifu wote wanawasalimu.
14 Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.
Paulo Anarudi Kutoka Korintho Kwenda Makedonia
Paulo anarudi kutoka Akaya na Korintho kwenda Makedonia, akiwatuma wenzake watangulie kwenda Troa.
4 Paulo alikuwa amefuatana na Sopatro mwana wa Piro, Mberoya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike na Gayo, mtu wa Derbe, Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka sehemu ya Asia. 5 Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa.