Paulo Anawaandikia Warumi

Akiwa njiani kutoka Akaya kwenda Makedonia, Paulo anaandika akiwa Korintho barua yake kwa Wayahudi na watu wa Mataifa wa Rumi. Kwa watu wa Mataifa, anathibitisha kwamba hawangeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa falsafa yao inayosifiwa sana, wala kwa maadili yao mema, wala kwa nuru ya akili ya mwanadamu. Kwa Wayahudi, anathibitisha kwamba hawangeweza kuhesabiwa haki kwa ujuzi wao wa Sheria ya Mose wala kwa kuitii. Imani katika Kristo pekee ndiyo njia ya pekee ya wokovu kwa wanadamu wote, na imekuwa hivyo sikuzote.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Paulo Anawasalimu Warumi

Paulo anathibitisha mamlaka yake kama mtume. Anaonyesha asili ya kibinadamu ya Kristo kwa kuwa alitokana na ukoo wa Daudi, na asili yake ya kimungu kwa ufufuo wake. Anasema kwamba alipokea utume wake kutoka kwa Kristo ili kuwahubiria injili watu wa Mataifa, ambao walikuwa wengi wa washiriki wa kanisa la Rumi, na hivyo ana mamlaka ya kuzungumza nao.

Warumi 1:1–7

1 Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu, 2 Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu, 3 yaani, Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi, 4 na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani, Yesu Kristo, Bwana wetu. 5 Kwa kupitia kwake na kwa ajili ya Jina lake, tumepokea neema na utume ili kuwaita watu miongoni mwa watu wa mataifa yote, waje kwenye utii utokanao na imani. 6 Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili mpate kuwa mali ya Yesu Kristo.

7 Kwa wote walioko Rumi wapendwao na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu:

Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.

Paulo Anatamani Kuwatembelea Warumi

Paulo anafurahia imani yao. Anaeleza shauku yake kubwa ya kuwatembelea, ili awaimarishe kwa kuwapa karama fulani ya kiroho, uthibitisho ambao kwa huo yeye na wao wangeimarishana na kufarijiana katika imani ya Kristo. Akiwa ameteuliwa kuhubiri injili kwa mataifa yote, bado anataka kuihubiri kwa Warumi, kwa sababu tatu. Kwanza, anathibitisha kwamba injili ni nguvu ya Mungu iletayo wokovu kwa Myahudi na pia kwa mtu wa Mataifa. Pili, katika injili pekee ndipo haki ya Mungu inapofunuliwa, pamoja na sharti pekee la kuhesabiwa haki na kukubaliwa naye, yaani kwa imani wala si kwa matendo. Tatu, injili ni kuu kuliko Sheria ya Mose, au nuru au sheria ya dhamiri, ambazo zote huwahukumu kifo, bila sharti lolote, wote waliotenda dhambi.

Warumi 1:8–18

8 Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote. 9 Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka 10 katika maombi yangu siku zote, nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nije kwenu.

11 Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuweka juu yenu karama za rohoni ili mwe imara, 12 au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi. 13 Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa mpaka sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa wengine ambao ni watu wa Mataifa wasiomjua Mungu.

14 Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima. 15 Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.

16 Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. 17 Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”

18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao,

Watu wa Mataifa Walimjua Mungu lakini Wakamwacha

Paulo anaonyesha kwamba watu wa Mataifa walikuwa na ushahidi wa kutosha wa Mungu na wa ukamilifu wake wenye utukufu katika kazi za uumbaji. Ili kuonyesha kwamba hakuna mtu ambaye angeweza kupata wokovu kwa sheria ya asili, anaorodhesha maovu ya Wayunani, ambao walikuwa wamefikia kiwango cha juu kabisa cha maarifa na hekima ya kibinadamu. Anasisitiza kwamba walimjua Mungu lakini wakaficha maarifa yao kumhusu, mpaka mioyo yao wenyewe ikapoteza uwezo wa kuona ukweli, nao wakaanzisha ibada ya kiumbe badala ya Muumba. Maarifa yao juu ya Mungu yaliwahakikishia adhabu iliyokuwa ikingojea maovu yao, lakini waliendelea kuyatenda na kuwahimiza wengine kufanya vivyo hivyo.

Warumi 1:19–32

19 kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao. 20 Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru.

21 Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. 22 Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga 23 na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.

24 Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao. 25 Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen.

26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa. 27 Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.

28 Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. 29 Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, 30 wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, 31 wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. 32 Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.

Wayahudi Wana Hatia ya Dhambi Hizohizo

Paulo anajua vizuri jinsi Wayahudi walivyo tayari kuungana katika kuwahukumu watu wa Mataifa kwa sababu ya dhambi zao. Sasa anajaribu kuwasadikisha Wayahudi kwamba wana dhambi, akitangaza kwamba wao pia wana hatia ya makosa hayohayo. Hukumu ya Mungu dhidi ya makosa hayo, iliyotolewa katika Sheria yao wenyewe, inajulikana kuwa ya kweli, na wote wanaoyatenda, wawe Wayahudi au watu wa Mataifa, hawataepuka hukumu ya mwisho ya Mungu.

Warumi 2:1–3

1 Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. 2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. 3 Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu?

Mungu Humhukumu Myahudi na Myunani kwa Usawa

Paulo anawaonya Wayahudi kwamba mapendeleo yao yatazidisha hukumu yao ya adhabu ikiwa hawatatubu. Anakanusha kwamba hukumu ya Mungu inawatofautisha Wayahudi na watu wa Mataifa, na anathibitisha kwamba adhabu zilezile na thawabu zilezile zitatolewa kwa usawa kwa Myahudi na kwa Myunani, kwa maana Mungu hana upendeleo.

Warumi 2:4–11

4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?

5 Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7 Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8 Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.

Kuhukumiwa kwa Nuru Ambayo Kila Mmoja Ameipokea

Paulo anaendelea kutangaza kwamba watu wote watahukumiwa kulingana na kiwango cha nuru na maarifa walichopokea. Si Wayahudi wanaoikiri Sheria lakini hawaitekelezi, bali watu wa Mataifa na wote wanaoishi kulingana nayo bila kuwa wamepokea maarifa yake yaliyokuja baadaye, ndio watakaopata kibali mbele za Mungu siku ile kuu, wakati watu wote watakapohukumiwa kwa sheria ya dhamiri na ya imani, kulingana na injili ya Mungu.

Warumi 2:12–16

12 Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria. 13 Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki. 14 (Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria. 15 Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) 16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.