Kuijua Sheria Hakuwezi Kumhesabia Myahudi Haki

Paulo anaonyesha kwamba maarifa ya dini peke yake hayangeweza kumhesabia Myahudi haki. Kwamba Sheria ya Mose haina uwezo wa kuokoa kunathibitishwa na kuvunjwa kwake waziwazi katika mwenendo wa waandishi na watawala wa Wayahudi, ambao walikuwa walimu walioteuliwa kuwafundisha watu. Anathibitisha shtaka hilo kwa Maandiko yao wenyewe.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Warumi 2:17–24

17 Tazama, wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu, 18 kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria, 19 kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, 20 mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria, 21 basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? 22 Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? 23 Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria? 24 Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.”

Tohara Haina Thamani Bila Utii

Paulo anaendelea kuonyesha kwamba tohara, ambayo Wayahudi walijivunia kama ishara ya kuwa wazao wa Abrahamu na ya mapendeleo yao maalumu kama watu waliochaguliwa na Mungu, isingewafaidi chochote wasipoishika Sheria. Kwa kuivunja Sheria, Myahudi alipoteza mapendeleo yake na hakuwa na hali bora kuliko mtu wa Mataifa asiyetahiriwa. Watu wa Mataifa wanaotimiza matakwa ya Sheria watakubaliwa na Mungu na kuingizwa miongoni mwa watu wake waliochaguliwa. Mtu anayeikiri dini kwa nje tu si mwana wa Abrahamu; mwana wa kweli ni yule tu aliye safi kiroho.

Warumi 2:25–29

25 Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. 26 Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? 27 Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii sheria watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja.

28 Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. 29 Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu wa namna hiyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.

Faida ya Myahudi na Uaminifu wa Mungu

Sasa kwa kuwa Paulo amewathibitishia Wayahudi na watu wa Mataifa pia kwamba wana dhambi, anaendelea kukanusha mitazamo ya upendeleo ya Wayahudi. Anamleta mtu anayeuliza ni kwa njia gani basi watoto wa Abrahamu wamependelewa zaidi kuliko watu wa Mataifa. Paulo anajibu, “Wamekabidhiwa maneno yenyewe ya Mungu.” Kisha Myahudi anauliza ikiwa kutokuamini kwa baadhi ya watu wa taifa lao ambao hawakuyaamini maneno hayo kungezibatilisha ahadi za Mungu. Katika kujibu, Paulo anasisitiza kwamba ukweli wa Mungu na ahadi zake vilithibitishwa na kutokuamini kwao, kwa kuwa udhaifu wa kibinadamu ulikuwa umevunja masharti ambayo ahadi hizo zilitegemea. Kisha Myahudi anauliza, “Ikiwa kutokuamini kwao kunadhihirisha haki ya Mungu hata zaidi, je, Mungu hangekuwa dhalimu kwa kuwaadhibu?” Paulo anaonyesha kwamba Mungu hawezi kuwa dhalimu, kwa maana kama angekuwa hivyo, angewezaje kuuhukumu ulimwengu? Myahudi anarudia hoja hiyo. Paulo anaikataa, akisema kwamba mwenendo huo ungekuwa kuwafundisha watu kutenda maovu ili mema yatokee. Wale wenye maoni hayo wanahukumiwa kwa haki.

Warumi 3:1–8

1 Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara? 2 Kuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa lile Neno halisi la Mungu. 3 Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu? 4 La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa:

“Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena,

na ukashinde utoapo hukumu.”

5 Ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.) 6 La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angehukumuje ulimwengu? 7 Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonyesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?” 8 Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja?” Wao wanastahili hukumu yao.

Wayahudi na Watu wa Mataifa Wote Chini ya Dhambi

Sasa Myahudi anauliza kama Wayahudi hawana haki zaidi kuliko watu wa Mataifa. Paulo anathibitisha tena alichokwisha kusema, kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote walikuwa chini ya dhambi. Dhambi ya Wayahudi inathibitishwa kwa Maandiko yao wenyewe, ambayo walikubali kuwa yamevuviwa kiungu. Hakuna mtu anayeweza kuhesabiwa haki kwa sheria, iwe ya Mose au ya maumbile, ambayo ingeweza kutoa tu ujuzi wa dhambi na hukumu yake.

Warumi 3:9–20

9 Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuwaliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. 10 Kama ilivyoandikwa:

“Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja.

11 Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu,

hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu.

12 Wote wamepotoka,

wote wameoza pamoja;

hakuna atendaye mema,

naam, hakuna hata mmoja.”

13 “Makoo yao ni makaburi wazi;

kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.”

“Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.”

14 “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.”

15 “Miguu yao ina haraka kumwaga damu;

16 maangamizi na taabu viko katika njia zao,

17 wala njia ya amani hawaijui.”

18 “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”

19 Basi tunajua ya kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. 20 Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi.

Kuhesabiwa Haki Bure kwa Imani katika Yesu Kristo

Kwa kuwa Sheria imeshindwa kabisa kuwahesabia watu haki, Paulo anatangaza kwamba njia pekee ya kuhesabiwa haki ni kwa imani katika Yesu Kristo. Hili linafundishwa katika Sheria na Manabii, na linatolewa kwa usawa kwa Myahudi na mtu wa Mataifa, ambao wote walikuwa wamethibitishwa kwa usawa kuwa wenye dhambi, kwa maana Mungu hana upendeleo. Kuhesabiwa haki ni zawadi ya bure ya Mungu kwa wote, kwa njia ya imani, kupitia dhabihu ya upatanisho na ukombozi wa Kristo Yesu, na hivyo majivuno yote yameondolewa.

Warumi 3:21–27

21 Lakini sasa, haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. 22 Haki hii itokayo kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wamwaminio. Kwa maana hapo hakuna tofauti, 23 kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. 25 Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. 26 Alifanya hivyo ili kuonyesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

27 Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La hasha, bali kwa ile sheria ya imani.

Imani Pekee Huhesabia Haki na Kuithibitisha Sheria

Paulo anahitimisha hoja kwa kutangaza kwamba chini ya injili, si Myahudi wala mtu wa Mataifa anayeweza kuhesabiwa haki isipokuwa kwa imani pekee, bila msaada wowote wa matendo ya Sheria. Kwa kuwa Mungu anawaona watu wa Mataifa na Wayahudi kwa usawa, njia ileile ya kuhesabiwa haki imewekwa kwa wote wawili. Sheria inathibitishwa, au kufanywa kamilifu, kwa imani.

Warumi 3:28–31

28 Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa njia ya imani wala si kwa matendo ya sheria. 29 Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. 30 Basi kwa kuwa tuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani iyo hiyo. 31 Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.