Abrahamu Alihesabiwa Haki Kabla ya Kutahiriwa

Paulo anathibitisha kwamba Abrahamu hakuhesabiwa haki kwa matendo ya Sheria. Hana kitu cha kujisifia. Alihesabiwa haki kwa imani, kwa neema na fadhili, si kama deni, yaani thawabu aliyostahili kwa matendo yake. Daudi anashuhudia njia hiyo hiyo ya kuhesabiwa haki, kama inavyoonyeshwa na ukweli kwamba Abrahamu alihesabiwa haki alipokuwa bado hajatahiriwa, na kwamba baadaye alipokea ishara ya tohara kama muhuri wa kuhesabiwa kwake haki kwa imani, ili awe baba wa kiroho wa Myahudi na mtu wa Mataifa, ambao wangekuwa na haki sawa ya kuhesabiwa haki kwa sharti moja la imani pekee.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Warumi 4:1–12

1 Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili? 2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu. 3 Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”

4 Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili. 5 Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki. 6 Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:

7 “Wamebarikiwa wale

ambao wamesamehewa makosa yao,

ambao dhambi zao zimefunikwa.

8 Heri mtu yule

Bwana hamhesabii dhambi zake.”

9 Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.” 10 Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa. 11 Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki. 12 Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.

Ahadi kwa Abrahamu Inawahusisha Watu wa Mataifa

Paulo anaendeleza hoja yake kwa kuwatangazia Wayahudi kwamba ahadi aliyopewa Abrahamu yenyewe ilionyesha kuwa ulimwengu wote ungekuwa warithi wake kupitia imani yake. Lakini ikiwa ni Wayahudi pekee ambao wangekuwa warithi wa ahadi yake, imani inakuwa batili, na ahadi iliyotolewa kwa sharti la imani inafutwa. Kwa maana Sheria, bila rehema, humweka mwenye dhambi chini ya adhabu, na bila Sheria hakuwezi kuwa na kanuni ya wajibu, na hivyo hakuna dhambi. Kwa sababu hii ahadi hutolewa kwa msingi wa imani, huku neema ya Mungu inayotolewa bure ikiwajumuisha watoto wa Abrahamu wa kimwili na wa kiroho. Kuhesabiwa haki kwa Abrahamu alipokuwa hajatahiriwa kunathibitisha kwamba watu wa Mataifa wanakubaliwa. Ahadi yenyewe, iliyothibitishwa kwa Abrahamu akiwa baba wa mataifa mengi, inathibitisha haki ya watu wa Mataifa ya kupata baraka zote za ukombozi.

Warumi 4:13–22

13 Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani. 14 Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu, 15 kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.

16 Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote. 17 Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.

18 Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.” 19 Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara. 20 Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu, 21 akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi. 22 Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”

Imani ya Abrahamu Iliandikwa kwa Ajili Yetu

Habari ya Abrahamu kukubaliwa na Mungu kwa njia ya imani iliandikwa kwa ajili yetu. Inatuonyesha kwamba njia pekee ya kupata wokovu mbele za Mungu ni kwa imani katika Mwana wake, ambaye aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu na kufufuka kama dhamana ya kupatanishwa kwetu, au kuhesabiwa kwetu haki.

Warumi 4:23–25

23 Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake, 24 bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu. 25 Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.

Baraka Zinazofuata Kuhesabiwa Haki

Paulo anaendelea kuorodhesha baraka kuu na fadhila zinazotokana na kuhesabiwa haki kwa imani. Roho Mtakatifu waliyepewa watu wa Mataifa anaonyesha upendo wa Mungu kwao, ambao unathibitishwa na Kristo kufa kwa ajili yao walipokuwa bado wapagani. Kwa hiyo, watu wa Mataifa wana tumaini lilelile la wokovu kupitia Kristo, na sababu zilezile za kufurahi katika Mungu, kama walivyo wazao wa Abrahamu kwa mwili, kwa kuwa wamepatanishwa na Mungu kwa upatanisho uleule.

Warumi 5:1–11

1 Kwa hiyo, kwa kuwa tumekwisha kuhesabiwa haki kwa imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, 2 ambaye kwa kupitia kwake tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo ndani yake sasa tunasimama, nasi twafurahia katika tumaini letu la kushiriki utukufu wa Mungu. 3 Si hivyo tu, bali twafurahi pia katika mateso, kwa sababu tunajua kuwa mateso huleta saburi, 4 nayo saburi huleta uthabiti wa moyo, na uthabiti wa moyo huleta tumaini, 5 wala tumaini halitukatishi tamaa, kwa sababu Mungu amekwisha kumimina pendo lake mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye ametupatia.

6 Kwa maana hata tulipokuwa dhaifu, wakati ulipowadia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi. 7 Hakika, ni vigumu mtu yeyote kufa kwa ajili ya mwenye haki, ingawa inawezekana mtu akathubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. 8 Lakini Mungu anaudhihirisha upendo wake kwetu kwamba: Tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.

9 Basi, kwa kuwa sasa tumehesabiwa haki kwa damu yake, si zaidi sana tutaokolewa kutoka ghadhabu ya Mungu kupitia kwake! 10 Kwa kuwa kama tulipokuwa adui wa Mungu tulipatanishwa naye kwa njia ya kifo cha Mwanawe, si zaidi sana tukiisha kupatanishwa, tutaokolewa kwa uzima wake. 11 Lakini zaidi ya hayo, pia tunafurahi katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia kwake tumepata upatanisho.

Dhambi ya Asili kwa Njia ya Adamu, Uzima kwa Njia ya Kristo

Sasa Paulo anaeleza fundisho la dhambi ya asili. Anaonyesha kwamba kwa kosa la mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na hukumu ya kifo ikawafikia watu wote, kwa sababu wote waliozaliwa baadaye walizaliwa na asili yenye dhambi. Kifo kilitawala kwa njia ya uharibifu wa asili yetu kabla ya Sheria ya Mose kujulikana. Adamu, aliyekuwa mfano wa yule ambaye angekuja na kichwa cha kidunia cha wanadamu, aliwarithisha dhambi. Kristo, ambaye ndiye utimilifu wa mfano huo na kichwa cha kiroho, aliwapatia wote uzima na kuhesabiwa haki. Matokeo ya utii wa Kristo ni makubwa kuliko matokeo ya kutotii kwa Adamu. Kwa kosa moja Adamu alileta uasi na kifo ulimwenguni. Kwa utii wake Kristo alibatilisha uovu wa dhambi, na kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani akawarudishia wanadamu wote zawadi ya bure ya uzima na msamaha wa makosa ya kibinadamu, yaani dhambi ya asili na dhambi zinazotendwa. Sheria iliingia ili kuwajulisha watu hatia ya dhambi. Neema na zawadi ya Mungu zinafurika ili kutuokoa kutoka katika hukumu ya Sheria. Kama vile dhambi ilivyowatawala wote, ikiwatia wanadamu wote chini ya kifo cha kiroho na cha kimwili, vivyo hivyo neema ya Mungu itatawala, ikileta utakatifu unaoongoza kwenye uzima wa milele.

Warumi 5:12–21

12 Kwa hiyo kama vile dhambi ilivyoingia ulimwenguni kupitia kwa mtu mmoja, na kupitia dhambi hii mauti ikawafikia watu wote, kwa sababu wote wamefanya dhambi: 13 kwa maana kabla sheria haijatolewa, dhambi ilikuwepo ulimwenguni. Lakini dhambi haihesabiwi wakati hakuna sheria. 14 Hata hivyo, tangu wakati wa Adamu hadi wakati wa Mose, mauti ilitawala watu wote, hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa kuvunja amri, kama alivyofanya Adamu, ambaye alikuwa mfano wa yule atakayekuja.

15 Lakini ile karama iliyotolewa haikuwa kama lile kosa. Kwa maana ikiwa watu wengi walikufa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja, zaidi sana neema ya Mungu na ile karama iliyokuja kwa neema ya mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo, imezidi kuwa nyingi kwa ajili ya wengi. 16 Tena, ile karama ya Mungu si kama matokeo ya ile dhambi. Hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja, ikaleta adhabu, bali karama ya neema ya Mungu ilikuja kwa njia ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. 17 Kwa maana ikiwa kutokana na kosa la mtu mmoja, mauti ilitawala kupitia huyo mtu mmoja, zaidi sana wale wanaopokea wingi wa neema ya Mungu na karama yake ya kuhesabiwa haki, watatawala katika uzima kwa njia ya huyo mtu mmoja, yaani, Yesu Kristo.

18 Kwa hiyo, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta adhabu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la haki la mtu mmoja lilileta kuhesabiwa haki ambako huleta uzima kwa wote. 19 Kwa maana kama vile kwa kutokutii kwa yule mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, vivyo hivyo kwa kutii kwa mtu mmoja wengi watafanywa wenye haki.

20 Zaidi ya hayo, sheria ilikuja, ili uvunjaji wa sheria uongezeke. Lakini dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi, 21 ili kwamba kama vile dhambi ilivyotawala kwa njia ya mauti, vivyo hivyo neema iweze kutawala kwa njia ya kuhesabiwa haki hata kuleta uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu.