Wakorintho Ni Barua ya Paulo

Paulo anauliza kwa kejeli ikiwa yeye pia, kama yule mwalimu wa uongo, anahitaji kuja kwao akiwa na barua za kumtambulisha. Anatangaza kwamba wao wenyewe ndio barua zake za kumtambulisha, zilizoandikwa si kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, na hivyo walikuwa ushahidi wa mamlaka ambayo Mungu alikuwa amemkabidhi katika huduma ya agano jipya.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wakorintho 3:1–6

1 Je, tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji kupata barua za utambulisho kwenu au kutoka kwenu, kama watu wengine? 2 Ninyi wenyewe ndio barua yetu iliyoandikwa katika mioyo yetu, inayojulikana na kusomwa na kila mtu. 3 Nanyi mwadhihirisha wazi kwamba ninyi ni barua itokayo kwa Kristo, matokeo ya huduma yetu, ambayo haikuandikwa kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai, si katika vibao vya mawe, bali katika vibao ambavyo ni mioyo ya wanadamu.

4 Hili ndilo tumaini tulilo nalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo. 5 Si kwamba sisi tunafikiri kuwa tunaweza kufanya jambo lolote wenyewe, lakini nguvu yetu inatoka kwa Mungu. 6 Ndiye alituwezesha sisi kuwa wahudumu wa Agano Jipya: si wa andiko, bali wa Roho; kwa kuwa andiko huua bali Roho hutia uzima.

Utukufu Mkuu Zaidi wa Injili

Akimpinga mwalimu wa uongo, Paulo anatangaza ukuu wenye utukufu wa injili. Utaji uliofunika utukufu wa nje wa Mose uliokuwa ukipita ulikuwa ishara ya kutokuwa wazi kwa agano la mauti na hali yake ya kimfano. Wahudumu wa agano la Roho, kwa utukufu wa kudumu na ulio mkuu zaidi katika karama za kudumu na uvuvio wa Roho Mtakatifu, waliwezeshwa kulifunua, kulieleza, na kulihubiri kila mahali agano la haki lenye utukufu mkuu zaidi.

2 Wakorintho 3:7–18

7 Basi ikiwa ile huduma iliyoleta mauti, iliyoandikwa kwa herufi juu ya jiwe ilikuja kwa utukufu, hata Waisraeli wakawa hawawezi kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya ule utukufu wake ingawa ulikuwa ni wa kufifia, 8 je, huduma ya Roho haitakuwa na utukufu zaidi? 9 Ikiwa huduma ile inayowahukumu wanadamu ina utukufu, je, ile huduma iletayo haki haitakuwa ya utukufu zaidi? 10 Kwa maana kile kilichokuwa na utukufu sasa hakina utukufu ukilinganisha na huu utukufu unaozidi wa Agano Jipya. 11 Ikiwa kile kilichokuwa kinafifia kilikuja kwa utukufu, je, si zaidi utukufu wa kile kinachodumu?

12 Kwa hiyo, kwa kuwa tunalo tumaini hili, tuna ujasiri sana. 13 Sisi si kama Mose, ambaye ilimpasa kuweka utaji ili kufunika uso wake ili Waisraeli wasiuone ule mngʼao uliokuwa juu yake hadi ulipofifia na hatimaye kutoweka. 14 Lakini akili zao zilipumbazwa, kwa maana mpaka leo utaji ule ule hufunika wakati Agano la Kale linasomwa. Huo utaji haujaondolewa, kwa maana ni katika Kristo peke yake unaondolewa. 15 Hata leo Sheria ya Mose inaposomwa, utaji hufunika mioyo yao. 16 Lakini wakati wowote mtu anapomgeukia Bwana, utaji unaondolewa. 17 Basi Bwana ndiye Roho. Mahali alipo Roho wa Bwana hapo pana uhuru. 18 Nasi sote, tukiwa na nyuso zisizotiwa utaji tunadhihirisha utukufu wa Bwana, kama kwenye kioo. Nasi tunabadilishwa ili tufanane naye, toka utukufu hadi utukufu mkuu zaidi, utokao kwa Bwana, ambaye ndiye Roho.

Paulo Anamhubiri Kristo, Si Yeye Mwenyewe

Paulo anaonyesha kwamba huduma yenye utukufu aliyokabidhiwa inamjaza tumaini na bidii. Anataka kujithibitisha kwa kuziweka wazi kikamilifu kweli za Injili, ambazo zinaweza kufichika kwa wale tu wenye mawazo ya kidunia, waliopofushwa na tamaa na ashiki zao. Paulo anatangaza kwamba hatafuti utukufu wake mwenyewe, kwa maana Mungu ameuangazia moyo wake ili aweze kuwafikishia wengine ujuzi na utukufu wa Mungu, uliofunuliwa katika Yesu Kristo.

2 Wakorintho 4:1–6

1 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii kwa rehema za Mungu, hatukati tamaa. 2 Tumekataa mambo ya siri na ya aibu, wala hatufuati njia za udanganyifu, tukichanganya Neno la Mungu na uongo. Kinyume cha hayo, tunadhihirisha kweli waziwazi na kujitambulisha wenyewe kwenye dhamiri ya kila mtu mbele za Mungu. 3 Hata nayo Injili yetu kama imetiwa utaji, ni kwa wale tu wanaopotea. 4 Kwa habari yao, mungu wa dunia hii amepofusha akili za wasioamini, ili wasione nuru ya Injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu. 5 Kwa maana hatujihubiri sisi wenyewe ila tunamhubiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Kwa kuwa Mungu, yeye aliyesema, “Nuru na ingʼae gizani,” ameifanya nuru yake ingʼae mioyoni mwetu ili kutupatia nuru ya maarifa ya utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo.

Mitume Kama Vyombo vya Udongo

Akiwalinganisha wahudumu wa Injili na vyombo vya udongo, Paulo anatangaza kwamba Mungu aliwachagua watu wasio na elimu wala hadhi kuwa mitume wake, ili kuonyesha kwamba nguvu kuu iliyoiwezesha dini yake kuenea ilitoka kwa Mungu wala si kwa wanadamu. Anaorodhesha taabu walizokabili, kama uthibitisho kwamba kuokolewa kwao kutoka katika taabu hizo hakukutokana na wao wenyewe bali na Mungu.

2 Wakorintho 4:7–12

7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu wala si kwetu. 8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Yesu ili kwamba uzima wa Yesu uweze kudhihirika katika miili yetu. 11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili kwamba uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti. 12 Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.

Imani na Tumaini Vinamwezesha Paulo Kustahimili

Paulo anaonyesha kwamba kupitia imani katika Kristo na tumaini la kutokufa katika utukufu, anaweza kushinda taabu na hatari zote za huduma yake ya Kikristo. Anawaambia kwamba alivumilia mateso hayo kwa ajili yao, ili wao, wakiwa wamesadiki unyofu wake, wamshukuru Mungu. Anatangaza usadikisho wake kwamba mateso yake kwa ajili ya injili yatampatia thawabu inayolingana nayo mbinguni. Kwa sababu hiyo, hatafuti faida za muda mfupi za ulimwengu huu, bali utukufu wa milele wa ulimwengu usioonekana.

2 Wakorintho 4:13–18

13 Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema, 14 kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka kwa wafu, atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake. 15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili kwamba neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi, ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.

16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi, 18 kwa sababu hatuangalii yale yanayoweza kuonekana bali yale yasiyoweza kuonekana. Kwa maana yale yanayoweza kuonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoweza kuonekana ni ya milele.

Makao ya Mbinguni Yatakayokuja

Paulo anaendeleza hoja yake kwa kuonyesha jinsi makao yetu ya mbinguni yatakavyokuwa bora zaidi kuliko yale tunamoishi sasa. Anasisitiza kwamba Mungu hutuandaa kwa ajili ya hali hii ya kutokufa na hutupa Roho wake kama dhamana yake. Hilo humpa ujasiri katika mahubiri yake na kumfanya awe tayari kuuacha mwili huu ili awe pamoja na Bwana. Lakini awe hai au amekufa, lengo lake ni kukubaliwa na Mungu, ambaye kila mtu lazima atoe hesabu kwake.

2 Wakorintho 5:1–10

1 Kwa maana twajua kama hema yetu ya dunia tunayoishi ikiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 2 Katika hema hii twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, 3 kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena kuwa uchi. 4 Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hii twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kwamba kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. 5 Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo naye ametupa Roho Mtakatifu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.

6 Kwa hiyo siku zote tunalo tumaini, hata ingawa tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana, 7 kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. 8 Naam, tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana. 9 Kwa hiyo, kama tuko katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.