Paulo Anaendelea Kwenda Uyunani
Paulo anaendelea kutoka Makedonia kwenda Uyunani, au Akaya, na anakaa huko miezi mitatu.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
2 Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani, 3 ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Alipokuwa anakaribia kuanza safari kwa njia ya bahari kwenda Shamu, kwa sababu Wayahudi walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yake, aliamua kurudi kupitia njia ya Makedonia.
Paulo Anawaandikia Wakorintho Tena 58 BK
Paulo, baada ya kusikia jinsi Wakorintho walivyoipokea barua yake ya kwanza, anaandika barua yake ya pili kutoka Filipi, ili kutetea mwenendo wake kama mtume na mamlaka yake, mambo yote mawili ambayo mwalimu wa uongo alikuwa ameyatilia shaka.
Paulo Anawasalimu Wakorintho Tena
Utangulizi na baraka za Paulo.
1 Barua hii ni kutoka kwangu mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu,
Kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko Akaya yote:
2 Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo iwe nanyi.
Paulo Anamhimidi Mungu kwa Faraja Yake
Paulo anamhimidi Mungu kwa kumtegemeza na kumwokoa katika taabu na hatari zake zote, kwa sababu kupitia mfano wake wengine wanaweza kufarijiwa katika mateso kama hayo kwa faraja ileile.
3 Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote. 4 Yeye hutufariji katika taabu zetu, ili tuweze kuwafariji walio katika taabu yoyote kwa faraja ambayo sisi wenyewe tumepokea kutoka kwa Mungu. 5 Kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi ndani ya maisha yetu, hivyo ndivyo faraja yetu inavyofurika kwa njia ya Kristo. 6 Kama tunataabika, ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu; kama tukifarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu, iwaleteayo saburi ya mateso yale yale yanayotupata. 7 Nalo tumaini letu kwenu ni thabiti, kwa sababu tunajua kwamba kama vile mnavyoshiriki mateso yetu, ndivyo pia mnavyoshiriki katika faraja yetu.
Mungu Anamwokoa Paulo Huko Efeso
Paulo anaeleza jinsi nguvu za Mungu zilivyomwokoa kutoka katika hatari ya papo hapo iliyomkabili huko Efeso. Anatambua sala zao kwa ajili yake.
8 Ndugu wapendwa, hatutaki mkose kujua kuhusu zile taabu tulizopata huko Asia. Kwa maana tulilemewa na mizigo sana, kiasi cha kushindwa kuvumilia, hata tulikata tamaa ya kuishi. 9 Kwa kweli, mioyoni mwetu tulihisi tumekabiliwa na hukumu ya kifo, ili tusijitegemee sisi wenyewe bali tumtegemee Mungu afufuaye wafu. 10 Yeye aliyetuokoa kwenye hatari kubwa ya kifo na atatuokoa tena. Kwake yeye tumeweka tumaini letu kwamba ataendelea kutuokoa. 11 Kama vile mlivyoungana kusaidiana nasi katika maombi, hivyo wengi watatoa shukrani kwa niaba yetu kwa ajili ya baraka za neema tulizopata kwa majibu ya maombi ya wengi.
Unyofu wa Paulo kwa Wakorintho
Akigusia kashfa za mwalimu wa uongo, Paulo anafurahia unyofu wake na usafi wa mwenendo wake kwa Wakorintho, ambao anatangaza kwamba haukuwa na nia zozote za ubinafsi au za kujinufaisha. Anaamini kwamba wote watamtambua na kujivunia yeye, kama wengine walivyofanya tayari, kwa kuwa watakuwa furaha yake katika siku ya Bwana.
12 Basi haya ndiyo majivuno yetu: Dhamiri yetu inatushuhudia kwamba tumeenenda katika ulimwengu na hasa katika uhusiano wetu na ninyi, katika utakatifu na uaminifu utokao kwa Mungu. Hatukufanya hivyo kwa hekima ya kidunia bali kwa neema ya Mungu. 13 Kwa maana hatuwaandikii mambo ambayo hamwezi kusoma au kuyaelewa. Natumaini kwamba, 14 kama vile mlivyotuelewa kwa sehemu, mtakuja kuelewa kwa ukamilifu ili mweze kujivuna kwa ajili yetu, kama na sisi tutakavyojivuna kwa ajili yenu katika siku ya Bwana Yesu.
Kwa Nini Paulo Aliahirisha Ziara Yake
Mwalimu wa uongo alikuwa amemshtaki Paulo kwa kusitasita katika kufanya maamuzi na kufuata mambo ya kidunia kwa sababu hakufanya ziara aliyokuwa amewaahidi Wakorintho. Paulo anaonyesha uthabiti wake katika mafundisho yasiyobadilika aliyofundisha, na anatumia kutiwa mafuta kwa Roho Mtakatifu kama uthibitisho wa mamlaka yake, ambayo Mungu alikuwa ameimarisha miongoni mwao kwa njia hiyo. Anatangaza kwa uzito kwamba sababu yake halisi ya kuahirisha ziara yake ilikuwa nia yake ya kuwaepushia uchungu. Anawahakikishia kwamba, badala ya kuja kuwaadhibu, aliwaandikia akiwa katika dhiki kubwa sana, ili afurahie kutubu kwao na kuwasadikisha jinsi upendo wake ulivyo mkuu.
15 Kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mambo haya, nilitaka nije kwenu kwanza, ili mpate faida mara mbili. 16 Nilipanga kuwatembelea nikiwa safarini kwenda Makedonia na kurudi tena kwenu nikitoka Makedonia, ili mnisafirishe katika safari yangu ya kwenda Uyahudi. 17 Nilipopanga jambo hili, je, nilikuwa kigeugeu? Au ninafanya mipango yangu kwa hali ya mwili, ili niseme, “Ndiyo, ndiyo” na “Siyo, siyo” wakati huo huo?
18 Hakika kama Mungu alivyo mwaminifu, maneno yetu kwenu hayajawa “Ndiyo na Siyo.” 19 Kwa kuwa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ambaye tulimhubiri kwenu: Mimi, Silvano na Timotheo, hakuwa “Ndiyo” na “Siyo,” bali kwake yeye siku zote ni “Ndiyo.” 20 Kwa maana ahadi zote za Mungu zilizo katika Kristo ni “Ndiyo.” Kwa sababu hii ni kwake yeye tunasema “Amen” kwa utukufu wa Mungu. 21 Basi ni Mungu atufanyaye sisi pamoja nanyi kusimama imara katika Kristo. Ametutia mafuta 22 kwa kututia muhuri wake na kutupa Roho wake mioyoni mwetu kuwa rehani kwa ajili ya kututhibitishia kile kijacho.
23 Mungu ni shahidi wangu kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kuwahurumia ninyi sikurudi Korintho. 24 Si kwamba tunatawala imani yenu, bali twatenda kazi pamoja nanyi kwa ajili ya furaha yenu, kwa sababu ni kwa imani mwasimama imara.
2:1 Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi. 2 Kwa kuwa kama nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha? 3 Niliandika hivyo kama nilivyofanya, ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao wangenifanya nifurahi. Nina uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu. 4 Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana kwa moyo wangu tena kwa machozi mengi, shabaha yangu si ili niwasababishe mhuzunike bali kuwaonyesha kina cha upendo wangu kwenu.
Msameheni na Mrudisheni Mkosaji
Paulo anawaagiza wampokee tena mtu aliyetengwa na kanisa ambaye wamemhuzunikia, kwa kuwa sasa anatubu kwa unyofu, na waonyeshe upendo wao kwake kwa kumtendea kwa wema na urafiki, ili Shetani asimsukume kukata tamaa. Paulo anatarajia wamtii katika kuondoa hukumu hiyo, kama walivyomtii katika kuitoa. Anatangaza kwamba katika yote mawili alitenda kwa jina na mamlaka ya Kristo.
5 Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi. 6 Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha. 7 Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi. 8 Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake. 9 Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo. 10 Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, 11 ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.
Wasiwasi wa Paulo Kuhusu Tito
Kama sababu nyingine ya kutokuja Korintho kwa wakati uliopangwa, Paulo anataja wasiwasi wake kuhusu Tito. Anaeleza mafanikio yake huko Makedonia, na kutangaza matokeo makubwa ya mahubiri yake, kwa wale wanaoipokea injili na kwa wale wanaoikataa. Anamalizia kwa kauli kali kuhusu mwalimu wa uongo na tamko la unyofu wake mwenyewe na kutokuwa na ubinafsi.
12 Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Kristo na kukuta kwamba Bwana alikuwa amenifungulia mlango, 13 bado nilikuwa sina utulivu akilini mwangu kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao nikaenda Makedonia.
14 Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye. 15 Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea. 16 Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo? 17 Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na Neno la Mungu kwa ajili ya kupata faida. Kinyume chake, katika Kristo tunalisema Neno la Mungu kwa unyoofu, kama watu tuliotumwa kutoka kwa Mungu.