Mwenendo wa Timotheo kwa Wazee na Wajane
Timotheo anapewa maelekezo zaidi ili mafundisho yake yafanikiwe zaidi. Anaelekezwa jinsi ya kuwatendea wazee, vijana wa kiume na wa kike, na wajane wanaotegemezwa na misaada ya kanisa. Hakuna mjane mwenye umri wa chini ya miaka sitini aliyepaswa kupokelewa, kwa sababu wanawake wadogo zaidi, wakipokelewa na kukatazwa kuolewa, wangeweza kuacha Ukristo au kuliletea jina la Mkristo aibu.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako; 2 nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote.
3 Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. 4 Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu. 5 Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie. 6 Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi. 7 Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo yeyote wa kulaumiwa. 8 Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.
9 Mjane yeyote asiwekwe kwenye orodha ya wajane isipokuwa awe ametimiza umri wa miaka sitini, na ambaye alikuwa mke wa mume mmoja, 10 awe ameshuhudiwa kwa matendo yake mema, aliyewalea watoto wake vizuri, aliye mkarimu, aliyewanawisha watakatifu miguu, aliyewasaidia wenye shida na aliyejitolea kwa ajili ya matendo mema ya kila namna.
11 Lakini kwa habari za wajane vijana usiwaweke kwenye orodha hiyo, maana tamaa zao za kimaumbile zikizidi kule kujitoa kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena. 12 Nao kwa njia hiyo watajiletea hukumu kwa kukiuka ahadi yao ya kwanza. 13 Zaidi ya hayo, wajane kama hao huwa na tabia ya uvivu wakizurura nyumba kwa nyumba, wala hawawi wavivu tu, bali pia huwa wasengenyaji, wajiingizao katika mambo yasiyowahusu na kusema mambo yasiyowapasa kusema. 14 Hivyo nawashauri wajane vijana waolewe, wazae watoto na wasimamie nyumba zao, wasije wakampa adui nafasi ya kutushutumu. 15 Kwa maana kwa kweli wajane wengine wamepotoka ili kumfuata Shetani.
16 Lakini kama mwanamke yeyote aaminiye ana wajane katika jamaa yake, inampasa awasaidie wala si kuwaacha wakililemea kanisa, ili kanisa liweze kuwasaidia wale ambao ni wajane kweli kweli.
Heshima kwa Wazee, Uangalifu Katika Kuwaweka Wakfu
Timotheo anaelekezwa kuhusu mwenendo wake kwa wazee, au wachungaji, wa kanisa. Wahudumu wema wanastahili heshima na malipo maradufu, na kanisa linapaswa kuwatimizia mahitaji yao ipasavyo. Wazee wanapaswa kukemewa tu kukiwa na ushahidi kamili kabisa, na hapo wakemewe hadharani ili kuwa onyo kwa wengine. Timotheo anaagizwa kwa uzito asipendelee kamwe katika uongozi wake, na awaweke wazee wakfu kwa uangalifu na tahadhari kubwa kabisa, baada ya kuchunguza tabia zao kwa uaminifu, ili asishiriki hatia au mwenendo mbaya wowote utakaotokea baadaye. Katika maelezo ya pembeni, Paulo anampa ushauri kuhusu afya yake.
17 Wazee wa kanisa wanaoongoza shughuli za kanisa vizuri wanastahili heshima mara mbili, hasa wale ambao kazi yao ni kuhubiri na kufundisha. 18 Kwa maana Maandiko husema, “Usimfunge maksai kinywa apurapo nafaka,” tena, “Mfanyakazi anastahili mshahara wake.” 19 Usiendekeze mashtaka dhidi ya mzee isipokuwa yawe yameletwa na mashahidi wawili au watatu. 20 Wale wanaodumu katika dhambi uwakemee hadharani, ili wengine wapate kuogopa.
21 Ninakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu na mbele za malaika wateule, shika maagizo haya pasipo ubaguzi wala upendeleo.
22 Usiwe na haraka kumwekea mtu mikono wala usishiriki dhambi za watu wengine. Jilinde nafsi yako uwe safi.
23 Acha kunywa maji peke yake, tumia divai kidogo kwa sababu ya tumbo lako na maumivu yako ya mara kwa mara.
24 Dhambi za watu wengine ni dhahiri nazo zinawatangulia kwenda hukumuni; na dhambi za watu wengine zinawafuata nyuma yao. 25 Vivyo hivyo, matendo mema yako dhahiri, na hata yale ambayo si mema hayawezi kufichika.
Watumwa Wawaheshimu Mabwana Zao
Kwa kuwa Ukristo haubadili mahusiano ya kijamii, watumishi na watumwa wanapaswa kuambiwa wawape heshima inayostahili hata mabwana zao wapagani. Wanaonywa hasa kuwatii vivyo hivyo mabwana zao Wakristo, na kutoruhusu umoja wao wa kindugu kama Wakristo uingilie wajibu wao wanaoujua.
1 Wale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. 2 Wale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao. Fundisha mambo haya na uwahimize kuyafuata.
Paulo Anawalaani Walimu Wanaosisitiza Desturi za Kiyahudi
Walimu wanaosisitiza kufuatwa kwa desturi za Kiyahudi wanalaaniwa, ambao wanashikilia mafundisho mengine na kuwaondolea watu wajibu wao wa kiraia. Wanakemewa kwa mabishano yao na ugomvi kuhusu maneno, na kwa kutanguliza faida yao wenyewe ya kidunia kuliko heshima ya Mungu na kuenea kwa kweli yake. Kuridhika kunahimizwa katika kila hali ya maisha, kwa kuwa mali zote za duniani ni ubatili. Kupenda utajiri kupita kiasi ni hatari kubwa.
3 Ikiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Yesu Kristo na yale ya utauwa, 4 huyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 na kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.
6 Lakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 Kwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 Lakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 Lakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 Kwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.
Timotheo Aagizwa Mbele za Mungu Kusimama Imara
Timotheo, akiwa mtu aliyevuviwa na Mungu, anaitwa kujiepusha na matendo haya maovu na kufuata utauwa. Paulo anamwagiza, kana kwamba yuko mbele za Mungu na akiizingatia siku kuu ya hukumu, kudumu imara katika imani, kutekeleza wajibu wa huduma yake kwa dhamiri safi, na kuepuka nia zote za kidunia na za tamaa ya mali. Paulo anamalizia kwa kueleza utukufu mkuu wa Kristo, utakaofunuliwa baadaye.
11 Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. 12 Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi. 13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, 15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe: yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, 16 yeye peke yake ambaye hapatikani na mauti, na anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.
Matajiri Wamtumaini Mungu, Si Mali
Timotheo anaagizwa kuwaonya matajiri wasitumainie mali zao zisizo na hakika, bali wamtumaini Mungu anayewapa mali hizo. Wanahimizwa kuwa matajiri katika matendo mema, ili wajiwekee akiba ya baraka zinazodumu zaidi na za milele.
17 Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.
Agizo la Mwisho la Paulo la Kuishikilia Imani
Paulo anamalizia barua kama alivyoianza, akimsihi Timotheo tena asimame imara katika mafundisho ya Kikristo na aepuke mawazo yote ya kubashiri ya kifalsafa na yasiyo na faida ambayo walimu wa uongo waliyapigia debe kwa nguvu sana.
20 Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu, 21 ambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.
Neema iwe nanyi. Amen.