Paulo Anawaelekeza Wanaume na Wanawake Katika Ibada
Wajibu wa kusali unasisitizwa tena. Wanaume wanaagizwa kutoa sala za hadharani, ambazo hazipaswi kuwekewa mipaka ya sinagogi au hekalu la Yerusalemu; zikitolewa kwa moyo wa ibada, zinakubalika kila mahali. Wanawake Wakristo wanahimizwa kutenda matendo mema na kukaa kimya. Mavazi yao yanapaswa kulingana na imani takatifu wanayoikiri. Kwa sababu ya kosa lake, mwanamke anapaswa kuwa chini ya mamlaka ya mwanamume. Laana iliyotamkwa juu yake itapunguzwa kwa sharti la imani na utakatifu.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
8 Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.
9 Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, 10 bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.
11 Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utiifu wote. 12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. 13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. 14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji. 15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake, kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.
Sifa za Maaskofu na Wahudumu
Sifa za askofu, anayesimamia makutaniko kadhaa, na za mhudumu anayesimamia kutaniko moja zinaelezwa.
1 Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. 2 Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, 3 asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. 4 Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. 5 (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) 6 Asiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi. 7 Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.
Jinsi Mashemasi na Wake Zao Wanavyolazimika Kuwa
Sifa za mashemasi zimeorodheshwa. Wake zao wanapaswa kuwa mifano kwa watu.
8 Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. 9 Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. 10 Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.
11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.
12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. 13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.
Paulo Anamtia Timotheo Moyo Katika Wajibu Wake
Paulo anamtia Timotheo moyo katika wajibu wake kama askofu na mhudumu kwa kumkumbusha mafundisho ya hali ya juu ya dini ya Kikristo.
14 Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba, 15 kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli. 16 Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa:
Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu,
akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,
akaonekana na malaika,
akahubiriwa miongoni mwa mataifa,
akaaminiwa ulimwenguni,
akachukuliwa juu katika utukufu.
Paulo Anatabiri Kuasi Imani kwa Kanisa
Kwa Roho wa Mungu, Paulo anatabiri kuanguka kwa kanisa la Kikristo na kuiacha imani, na anaeleza namna ya upotovu wake, akidokeza kwamba walimu waliowashawishi watu kufuata desturi za Kiyahudi walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakiuandalia njia. Timotheo anaonywa dhidi ya kila mwelekeo kuelekea upotovu huo, na anahimizwa kufundisha kuishi kwa wema na utauwa kuwa ndiyo huduma pekee yenye faida na inayokubalika kwa Mkristo. Anaambiwa kusisitiza ukweli huu muhimu, hata ingawa atashutumiwa na kuteswa kwa kufanya hivyo.
1 Roho asema waziwazi kwamba katika siku za mwisho baadhi ya watu wataiacha imani na kufuata roho zidanganyazo na mafundisho ya mashetani. 2 Mafundisho kama hayo huja kupitia kwa waongo ambao ni wanafiki, hali dhamiri zao zikiungua kwa kuchomwa moto. 3 Wao huwakataza watu wasioe na kuwaagiza wajiepushe na vyakula fulani, ambavyo Mungu aliviumba ili vipokewe kwa shukrani na wale wanaoamini na kuijua kweli. 4 Kwa maana kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, wala hakuna kitu chochote cha kukataliwa kama kikipokewa kwa shukrani, 5 kwa sababu kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.
6 Kama ukiwakumbusha ndugu mambo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, uliyelelewa katika kweli ya imani na yale mafundisho mazuri uliyoyafuata. 7 Usijishughulishe kamwe na hadithi za kipagani na masimulizi ya uongo ya wanawake wazee; badala yake, jizoeze kuwa mtauwa. 8 Kwa maana mazoezi ya mwili yana faida kwa sehemu, lakini utauwa una faida katika mambo yote, yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa na ya ule ujao.
9 Hili ni neno la kuaminiwa tena lastahili kukubaliwa kabisa, 10 (nasi kwa ajili ya hili tunajitaabisha na kujitahidi), kwamba tumeweka tumaini letu kwa Mungu aliye hai, ambaye ni Mwokozi wa watu wote, hasa wale waaminio.
11 Mambo haya yaagize na kuyafundisha.
Paulo Anaelekeza Mwenendo Binafsi wa Timotheo
Paulo anampa Timotheo maelekezo kuhusu mwenendo wake mwenyewe, na anataka aache mada zote za kubashiri katika mafundisho yake. Anapaswa kuwa mfano kwa kanisa na kujitolea kwa huduma, kusoma, kujifunza, kutafakari na kujitawala. Kwa kufanya hivyo atajiokoa mwenyewe na kuwa njia ya wokovu kwa wengine.
12 Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi. 13 Fanya bidii kusoma Maandiko hadharani, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14 Usiache kutumia kipawa kilicho ndani yako, ambacho ulipewa kwa neno la unabii wakati wazee walikuwekea mikono.
15 Uwe na bidii katika mambo haya; ujitolee kwa ajili ya mambo haya kikamilifu, ili kila mtu aone kuendelea kwako. 16 Jilinde sana nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika hayo, kwa maana kwa kufanya hivyo, utajiokoa wewe mwenyewe pamoja na wale wanaokusikia.