Demetrio Anachochea Umati Wenye Ghasia Huko Efeso

Paulo anaendelea kukaa Efeso. Demetrio anachochea umati wenye ghasia huko.

57 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Matendo 19:23–41

23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana. 24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa, 25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii! 26 Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote, huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu. 27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”

28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” 29 Mara mji wote ukajaa ghasia. Wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, na watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja. 30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati huo, lakini wanafunzi hawakumruhusu. 31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi.

32 Ule umati ulikuwa na taharuki. Wengine walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko. 33 Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu. 34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”

35 Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni? 36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka. 37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike. 38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka. 39 Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali. 40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.” 41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

Paulo Anaondoka Efeso Kwenda Makedonia

Matendo 20:1

1 Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia.

Paulo Anamwandikia Timotheo

Paulo anamwandikia Timotheo barua yake ya kwanza ili kumwelekeza jinsi ya kukomesha mafundisho ya uongo na upotovu ambao washupavu wa Wayahudi walikuwa wakijaribu kuanzisha katika kanisa la Efeso, ambalo alikuwa ameteuliwa kulisimamia.

Paulo Anamsalimu Timotheo

Salamu.

1 Timotheo 1:1–2

1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na ya Kristo Yesu tumaini letu.

2 Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani:

Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Kwa Nini Paulo Alimwacha Timotheo Efeso

Paulo anamkumbusha Timotheo kwa nini alikuwa amemwacha huko Efeso: ili kuwapinga Wayahudi wenye bidii kali ya kidini, waliokuwa wakijaribu kuchanganya nasaba na mapokeo katika mafundisho ya Kikristo.

1 Timotheo 1:3–4

3 Kama nilivyokusihi wakati nilipokwenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili kwamba upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo 4 wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani.

Kusudi na Matumizi ya Sheria

Paulo anaeleza kusudi na matumizi ya Sheria, ambayo anaonyesha kuwa inapatana kikamilifu na Ukristo, kwa kuwa inadai watu waishi kwa maadili mema na kulaani kila aina ya uovu.

1 Timotheo 1:5–11

5 Kusudi la maagizo haya ni upendo utokao katika moyo safi, dhamiri njema na imani ya kweli. 6 Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, 7 wanataka kuwa walimu wa sheria, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.

8 Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa. 9 Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji, 10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli, 11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.

Rehema ya Kristo Katika Kumfanya Paulo Kuwa Mtume

Paulo anageukia kutafakari wema wa Kristo katika kumfanya kuwa mtume wa injili hii yenye utukufu. Kutokana na rehema ambazo Mungu amemwonyesha, anawaalika wenye dhambi wote watubu.

1 Timotheo 1:12–17

12 Namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu.

15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Kristo Yesu apate kuonyesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.

Timotheo Anaagizwa Kuishika Imani

Paulo anamkumbusha Timotheo kwamba alikuwa ameteuliwa kwa njia ya unabii kwa ajili ya huduma ya Kikristo, na anamhimiza ashikilie imani safi na dhamiri njema. Aleksanda na Himenayo, ambao hawakushikilia imani safi wala dhamiri njema, wanaadhibiwa kwa kutomcha Mungu.

1 Timotheo 1:18–20

18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vita vizuri, 19 ukiishikilia imani na dhamiri njema, ambazo wengine wamevikataa, na hivyo wakaangamia kwa habari ya imani yao. 20 Miongoni mwao wako Himenayo na Aleksanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.

Paulo Anaagiza Sala kwa Ajili ya Watu Wote

Kinyume na Wakristo wanaotaka kufuata desturi za Kiyahudi, Paulo anawaamuru waongofu Wakristo, kwa roho ya wema ya injili, wawaombee watu wote, wawe Wayahudi au watu wa Mataifa, na hasa wafalme na wenye mamlaka wa kila taifa na nchi. Anatangaza kwamba jambo hili linampendeza Mungu, ambaye anataka watu wote waokolewe, na kwamba kuna Mpatanishi mmoja tu kati ya Mungu na watu wa mataifa yote. Paulo ameteuliwa kuwajulisha watu wa Mataifa na pia Wayahudi kweli hizi.

1 Timotheo 2:1–7

1 Awali ya yote, nasihi kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: 2 kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. 3 Jambo hili ni jema, tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu, 4 anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. 5 Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani mwanadamu Kristo Yesu, 6 aliyejitoa mwenyewe kuwa fidia kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake ufaao. 7 Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu wa Mataifa katika imani na kweli.