Adamu wa Kwanza na wa Pili

Ukweli wa ufufuo unathibitishwa kwa Wayahudi kupitia mfanano kati ya Adamu wa kwanza na wa pili.

57 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wakorintho 15:45–49

45 Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. 46 Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. 49 Kama vile tulivyochukua mfano wa mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.

Ushindi Dhidi ya Dhambi na Mauti

Paulo anasisitiza kwamba miili yetu ya sasa haiwezi kuingia katika hali ya kiroho. Anaeleza jinsi ufufuo utakavyotokea na mabadiliko ya utukufu yatakayotokea katika hali ya kutokufa, pamoja na ushindi kamili dhidi ya dhambi na mauti. Kwa misingi hii Wakorintho wanahimizwa kuwa na imani yenye matendo na iliyo thabiti.

1 Wakorintho 15:50–58

50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika. 51 Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa 52 ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. 53 Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.”

55 “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako?

Uko wapi, ee mauti, uchungu wako?”

56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu katika Bwana si bure.

Paulo Anatoa Maagizo ya Kukusanya Michango kwa Maskini

Akijibu swali la mwisho la Wakorintho, Paulo anatoa maagizo kuhusu jinsi Wakristo wanavyopaswa kuwasaidia maskini, na anaahidi kutuma michango yao Yerusalemu.

1 Wakorintho 16:1–4

1 Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo. 2 Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango. 3 Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu. 4 Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.

Ujumbe na Salamu za Mwisho za Paulo

Paulo anamalizia barua yake kwa ujumbe na salamu mbalimbali. Anawaeleza kuhusu mwanawe Timotheo, na kwamba Apolo anakusudia kuja kuwaona. Anamkabidhi Timotheo kwao kwa maneno ya sifa. Anawahimiza kuwa na imani na upendo. Anawasifu Stefana, Fortunato na Akaiko mbele yao. Anamalizia kwa salamu na heri njema.

1 Wakorintho 16:5–24

5 Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia. 6 Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo. 7 Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda. 8 Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste, 9 kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.

10 Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo. 11 Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.

12 Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.

13 Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari. 14 Fanyeni kila kitu katika upendo.

15 Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, 16 mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. 17 Nilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. 18 Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.

19 Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana. 20 Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.

21 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.

22 Kama mtu yeyote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo.

23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.

24 Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.