Mashahidi wa Ufufuo wa Kristo
Paulo anaendelea kukanusha dhana potovu ya Kiyahudi kuhusu ufufuo iliyokuwa imeenea miongoni mwa Wakorintho. Anatumia ushuhuda wa waliojionea wenyewe kuwa uthibitisho bora zaidi wa ufufuo wa Kristo.
57 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. 2 Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.
3 Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemavyo Maandiko, 4 ya kuwa alizikwa na alifufuliwa siku ya tatu, kama yasemavyo Maandiko, 5 na kwamba alimtokea Kefa, kisha akawatokea wale kumi na wawili. 6 Baadaye akawatokea wale ndugu waumini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. 7 Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. 8 Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.
9 Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. 11 Hivyo basi, kama ilikuwa mimi au wao, hili ndilo tunalohubiri, na hili ndilo mliloamini.
Kufufuka kwa Kristo Kunathibitisha Kwamba Wafu Watafufuka
Kwa ufufuo wa Kristo, Paulo anathibitisha kwamba wafu watafufuliwa hakika. Wanadamu waliwekwa chini ya mauti kupitia Adamu na wanafufuliwa wapate uzima kupitia Kristo.
12 Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuliwa kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? 13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuliwa. 14 Tena ikiwa Kristo hakufufuliwa kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili. 15 Zaidi ya hayo, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo kuhusu Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Kristo kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi. 16 Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Kristo hajafufuka. 17 Tena kama Kristo hajafufuliwa, imani yenu ni batili; nanyi bado mko katika dhambi zenu. 18 Hivyo basi, wote waliolala katika Kristo wamepotea. 19 Ikiwa tumaini letu ndani ya Kristo ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wote.
20 Lakini kweli Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala. 21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai.
Mpangilio wa Ufufuo
Paulo anafunua mpangilio wa ufufuo. Kristo anakabidhi ufalme wake akiwa mpatanishi baada ya wanadamu kufufuliwa kutoka kaburini na dhambi na mauti kuangamizwa.
23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. 24 Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. 25 Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. 27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. 28 Atakapokuwa amekwisha kuyafanya haya, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.
Kukana Ufufuo Kunapingana na Ubatizo
Kutokuamini ufufuo kunapingana na kile tunachokiri katika ubatizo, na kunahimiza maisha yasiyo na maadili. Anawahimiza wasidanganywe.
29 Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao? 30 Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? 31 Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku. 32 Kama kwa sababu za kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani? Kama wafu hawafufuliwi,
“Tuleni na kunywa,
kwa kuwa kesho tutakufa.”
33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” 34 Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, wala msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.
Kama Mbegu, Mwili Utafufuka Ukiwa Umebadilika
Paulo anajibu hoja za kifalsafa zinazopinga ufufuo wa wafu kwa kuulinganisha na mmea unaochipuka kutoka katika mbegu yake. Anaonyesha kwamba mwili wa binadamu, unaozikwa ardhini, utafufuka tena vivyo hivyo wakati wa ufufuo, ukiwa umebadilika katika sifa zake na kuwa mzuri zaidi katika umbo lake.
35 Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. 37 Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. 38 Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. 39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. 40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na fahari wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine. 41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.
42 Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika, 43 unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, 44 unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.
Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia.